Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia: Hatutasita kutumia vyombo vya dola kuhami wananchi

Muktasari:

  • Rais Samia amesema hayo leo Julai 9, 2026 mjini Unguja, Zanzibar wakati akishuhudia hafla ya utiaji saini wa tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT- Wazalendo.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewaonya watu wanaojiita ‘wanaharakati’ akiyaita matendo yao kuwa ya kigaidi huku akisema Serikali haitasita kutumia vyombo vya dola kuhami wananchi wake na kulinda heshima ya nchi.

Rais Samia amesema hayo leo Julai 9, 2026 mjini Unguja, Zanzibar wakati akishuhudia hafla ya utiaji saini wa tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT- Wazalendo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi akiwa kwenye picha na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa Othman Masoud Othman baada ya kushuhudia utiaji saini wa ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili kwa ajili ya kufanyiwa kazi kufuatia Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar Julai 9, 2026.

Ametumia nafasi hiyo kuwaonya wale aliosema wanaojiita wanaharakati kwa jina ili watambulike duniani, lakini kiuhalisia matendo yao ni ya kigaidi.

Amefafanua kuwa, ugaidi unajumuisha vitendo vya uvunjifu mkubwa wa amani, uharibifu wa mali na miundombinu, vinavyokusudia kuitishia jamii au kuishurutisha Serikali kukubaliana na matakwa ya watu au kundi fulani kwa ajili ya kutimiza haja za kisiasa, kiitikadi au kidini.

Kwa mustakabali wa dunia ya sasa, ugaidi unaweza kutumika kuirudisha nyuma nchi inayoendelea kwa kasi. Watu au kundi hilo, wanakuwa na kauli zinazovaa sura ya kizalendo lakini kwa undani ni masilahi binafsi.

“Mtu anayeipenda nchi yake, kiukweli, huijenga na siyo kuibomoa. Upande huu tumeipenda nchi yetu, tumetofautiana, tumevumiliana, hatukufanya vurugu za kubomoa nchi yetu wala uvunjifu wa amani.

“Nawasihi Watanzania, tushikamane kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu na siyo kulifanya Taifa kuwa duni kwa matakwa ya watu binafsi ambao maisha yao huko waliko na hata hapa nchini, yanategemea malipo yatokanayo na kufanya vurugu au kuivuruga nchi yao kwa maslahi yaw engine,” amesema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi amewahakikishia Watanzania kwamba, Serikali itasimama imara katika ulinzi wa raia wake na mali zao, pia, amewataka wananchi kuungana na Serikali kulinda maeneo yao na mali zao.

“Vitendo vya kigaidi katu havikubaliki, siyo kwa Tanzania tu, bali ulimwengu mzima. Hivyo basi, niwaonye kwa mara nyingine wote wanaojishughulisha na vitendo hivyo, kwamba Taifa lolote duniani hutumia vyombo vya dola kuhami wananchi wake na kulinda heshima yake. Nasi Tanzania kama Taifa hatutasita kufanya hivyo,” amesisitiza.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi, Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa Othman Masoud Othman pamoja na viongozi mbalimbali kwenye hafla ya uwasilishaji wa Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar Julai 9, 2026.

Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zote zenye dhamira ya kulinda amani, kuendeleza umoja wa muungano na kuimarisha ustawi wa wananchi. Amesema Zanzibar ikiwa na amani, Tanzania inakuwa salama.

“Amani ni mtaji, maridhiano ni daraja na wananchi ndiyo sababu ya uongozi wetu, hatuna budi kuwatumikia kwa amani na utulivu,” amesema Rais Samia.


Maridhiano si udhaifu

Rais Samia amesema maridhiano si udhaifu bali ni ukomavu wa kisiasa unaojenga misingi ya umoja na kuheshimiana.

Amesema ni ishara kwamba viongozi wanaweza kutofautiana lakini wakakubaliana katika mambo ya msingi ya uendeshaji wa nchi, kujali masilahi ya wananchi na nchi kwa jumla.

“Mwelekeo huu wa kiungwana tulioshuhudia leo unafungua ukurasa mwingine katika kuimarisha umoja, amani, mshikamano na utulivu wa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla, jitihada hizi zinapaswa kuendelezwa na kuenziwa,” amesema.

Amesema uungwana unatufunza kuwa na siasa za kushindana kwa hekima na si kupaza sauti bila mantiki, unafundisha siasa zinazotanguliza masilahi ya nchi na wananchi wake na siasa zinazotawaliwa na sauti zenye staha, utu, heshima na utulivu ili kufikia mustakabali wa pamoja wa kitaifa.

“Uungwana hautufunzi kiburi na kutosikilizana. Wananchi wetu hawahitaji vurugu wala mivutano ya kisiasa isiyoisha, wananchi wetu wanahitaji amani, usalama na utulivu. Shauku ya wananchi wote, bila kujali vyama vyao, ni kuona Serikali ikiwapa huduma bora za kijamii, ikiimarisha shughuli zao za kiuchumi na kukuza ajira katika mazingira yenye ustawi,” amesema.

Amesema penye siasa za chuki, baraka za maendeleo hutoweka, lakini penye siasa za staha na maelewano, maendeleo hupata nafasi na kuchanua.

 Ametoa wito wa kuendelea kuyaheshimu makubaliano yaliyofikiwa kati ya CCM na ACT- Wazalendo.

“Tuendeleze mazungumzo katika hali ya kuaminiana huku tukizingatia misingi ya umoja, amani, usalama na utulivu wa Taifa letu. Hekina tuliyoionesha leo ikalindwe na matendo mema ya kesho na imani tuliyoijenga kwa muda mrefu isiangushwe na mienendo isiyo na tija,” amesema.


Achambua kauli ya Samia

Wakili na mchambuzi wa siasa, Maduhu William amesema jamii haiwezi kujidanganya kuwa maridhiano hayana faida kwa kuwa duniani kote matatizo ya kisiasa ikiwamo misuguano huwa yanatatuliwa kupitia meza ya mazungumzo.

“Mazungumzo ndio msingi, wanasiasa wanajukumu la kutafuta suluhu kwa njia ya mazungumzo na si vinginevyo. Mazungumzo hayo yawe ya kweli na kuaminiana,” amesema.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi akiwa kwenye picha na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa  Othman Masoud Othman baada ya kushuhudia utiaji saini wa ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili kwa ajili ya kufanyiwa kazi kufuatia Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar  Julai 9, 2026.

Akizungumzia kauli ya Rais kuhusu wanaharakati, amesema nchi inaongozwa kwa Katiba na sheria pamoja na vyombo vyenye mamlaka, hivyo kama kuna mtu anayeonekana kwenda kinyume na Katiba basi uchunguzi utafanyika mtu huyo atakamatwa popote alipo na atafikishwa mahakamani.

“Mahakama itafanya uamuzi wa tuhuma hizo. Rais ana haki ya kutoa hayo maagizo lakini kinachotakiwa tu ni uchunguzi ili kwenda kuthibitishwa kisha Mahakama kutoa hukumu,” amesema wakili huyo.

Ameongeza kuwa mtu yeyote atakayetuhumiwa lazima mchakato wa kisheria ufuatwe, yaani kumpa nafasi ya kumsikiliza kuhusu tuhuma hizo, ndipo Mahakama ipate nafasi ya kutoa hukumu.