Prime
Mwelekeo mpya SUK, viongozi wa dini, wanasiasa watoa kauli
Muktasari:
- Kesho Alhamisi Julai 9, 2026, Rais Hussein Mwinyi na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud kutoa tamko la pamoja.
Unguja. Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT- Wazalendo vikisubiri kutoa tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa Zanzibar, viongozi wa dini, wa siasa na wananchi wa kawaida wamekuwa na maoni mseto juu ya hatua hiyo.
Tamko la pamoja baina ya vyama hivyo viwili vikuu vya siasa Zanzibar litatolewa kesho Alhamisi Julai 9, 2026 Ikulu Zanzibar ikishuhudiwa na viongozi wakuu wa vyama hivyo na serikali, Rais Hussein Mwinyi na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud.
Hatua hiyo inatajwa kuondoa mkwamo wa kisiasa uliodumu kwa takribani miezi minane tangu umalizike uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 ambao kwa mujibu wa Katiba baada ya CCM kuibuka mshindi, nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais ilitakiwa kujazwa na ACT- Wazalendo.
Hata hivyo, chama hicho kiligoma kuingia ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa kile kilichodai kuna mambo hawakubaliani nayo, yanatakiwa kutekelezwe hatua iliyosababisha waingie kwenye mazungumzo ya pande zote mbili.
Mazungumzo hayo yaliongozwa na marais wawili wastaafu wa Zanzibar--Amani Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein (CCM), Juma Duni Haji (mwenyekiti mstaafu wa ACT- Wazalendo) na Othman Masoud mwenyekiti wa sasa wa chama hicho taifa.
Katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Rais Ikulu jana, Julai 7, 2026, imeeleza hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Tanzania na Zanzibar, viongozi wa dini, vyama vya siasa na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na waandishi wa habari.
Novemba 13, 2025, Rais Mwinyi alipotangaza baraza lake la mawaziri, aliahirisha uteuzi wa mawaziri na manaibu wao katika wizara nne, akisubiri upande wa ACT-Wazalendo kupendekeza majina ya watu wanaoona wanastahili kushiriki katika SUK.
Wizara hizo ambazo mpaka sasa zimeendelea kuwa wazi ni Afya, Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Utalii na Mambo ya Kale, pamoja na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
“Hizi nafasi zitabaki wazi kwa mujibu wa Katiba mpaka pale kipindi kitakapokwisha ambacho Kikatiba ni siku 90,” alisema Dk Mwinyi, Novemba 13, 2025.
Kuhusu ACT- Wazalendo kuachiwa wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Dk Mwinyi alisema wamefanya hivyo kwa utashi mwema kuwaachia wenzao wizara hiyo inayoongoza uchumi wa Zanzibar.
“Sekta kuu ya uchumi hapa Zanzibar ni utalii, basi tumeona tuwe na good will (matashi mema), sekta kiongozi tuwape wao,” alisema.
Walichokisema wadau
Jana, Jumanne, Julai 7, 2026, Mwananchi lilizungumza na makundi mbalimbali juu ya taarifa za kurejea tena kwa SUK na mtazamo wao wa hali ya kisiasa visiwani humo na wamekuwa na mitizamo tofauti.
Baadhi wamepongeza hatua hiyo na kutaka kuzingatia utekelezaji wa watakayokubaliana, huku wengine wakisema hakuna jipya kwani kumekuwapo na mazungumzo hayo kwa muda mrefu na Serikali kila baada ya uchaguzi unaibuka mkwamo mpya.
Askofu wa Kanisa la Zanzibar International Christian Centre (ZICC), Dickson Kaganga amesema wamekuwa wakiombea na kushauri uwepo wa SUK.
Amesema hata kabla ya uchaguzi viongozi wa dini walikwenda kumuona Rais Mwinyi na Othman, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kila mmoja kwa wakati wake na kuwasihi na kuwakabidhi kitabu cha amani kilichoandikwa kwamba SUK ndio suluhu ya Zanzibar inawaunganisha watu na kuondoa sintofahamu.
“Sasa tunapopata taarifa hii kwamba wamefikia muafaka, sisi kwetu ni faraja kubwa na tunapongeza,” amesema na kuongeza:
“Amani ndio kila kitu, mahali penye mfarakano hakuwezi kupata maendeleo na kupoteza muda mwingi kuzungumza siasa wakati zilitakiwa ziishe baada ya uchaguzi tuzungumze maendeleo, wanaokosoa wakosoe kwa wema na Serikali isikilize.”
Naye Sheikh Shaib Iddi Ali amesema wanawatakia wahusika mafanikio mema na ushirikiano wa kutosha wakiaminiana jambo hilo litaleta heri.
‘Ukurasa mpya’
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib amepongeza kwa hatua hiyo waliofikia akisema kulikuwa na mkwamo mkubwa na kimya kirefu, lakini hatimaye kinakwenda kupata tiba.
Amesema pamoja na kwamba kulikuwa na mazungumzo, waliokuwa wakijua ni wao na kwamba hatua ya kutangaza maridhiano keshokutwa ni jambo zuri na litafungua ukurasa mpana zaidi kwa Zanzibar.
“Hakuna anayependa kutokuelewana, SUK ilikuwapo kwa mujibu wa katiba moja katika takwa la kikatiba la Zanzibar, kwa hiyo niwapongeze maana jambo hili linakwenda kufungua ukurasa mpya Zanzibar,” amesema.
Ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi waunge mkono na vyama vingine viunge mkono na waombee watakaoteuliwa wafanye kazi kwa uadilifu na wawatumikie wananchi.
Naye mwanasiasa Mbarouk Seif amesema:“Hiki sio kitu kipya ni aina fulani ya ulaghai ACT -Wazalendo wanataka kufungwa macho, lakini mchezo ndio uleule hakuna litakalokuwa, kuna vitu watakubalina na hawatavitekeleza, kwani hii sio mara ya kwanza bali ni mwendelezo.”
Kiongozi mstaafu wa Itifaki na Uthibiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Rajab Mbarouk Mohamed amesema wanatakia heri nchi na lolote litakaloleta muafaka na utulivu wanalikubali.
“Tatizo ni utekelezaji, hata muafaka wa mwanzo baina ya CUF na CCM baada ya kukubalian ndani ya kipindi cha miaka mitano ya mwanzo nchi ilitulia na walikwenda vizuri, lakini baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 mambo yakabadilika,” amesema Rajab.
Mwanasiasa huyo amesema:“Kwa sasa kinachotendeka tunakikubali na tunakitakia heri tuwe na maridhiano, lakini utekelezaji wake usiishie pale wanapomaliza madaraka na kuanza mazungumzo mapya.”
Amesema aina hiyo ya maridhiano kuna hatari mbeleni vijana watachoka na muafaka wa kila siku:“Kwa sababu muafaka ulishakuwepo na ulitakiwa uendelezwe, lakini sasa leo tunarudi tena tunakaa mezani eti tunatafuta maridhiano.”
Amesema katika makubaliano ya awali walitegemea waende mpaka hata katika ngazi za masheha wawe na mgawanyo, lakini jambo hilo halikutokea.
Naye Ashura Khamis Hassan, mkazi wa Amani, amesema jambo hilo lilikuwa likisubiriwa kwa muda mrefu, hivyo matumaini yao ni kuona makubaliano hayo yanakwenda vizuri kwa mustakabali wa wananchi na Taifa kwa ujumla wake.
Mwananchi mwingine wa Mtenddeni, Tatu Mussa Hassan amesema:“Kikubwa makubaliano hayo yawalenge wananchi na kuondoa maslahi ya vyama au viongozi wa vyama, ikiwa lengo ni wananchi basi yanapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote.”