Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SUK Zanzibar kimeeleweka

Muktasari:

  • Baada ya kamati maalumu ya CCM, kupitisha mazungumzo na makubaliano baina ya chama hicho na ACT - Wazalendo, hatua inayofuata ni tamko la pamoja litakalosomwa na viongozi wa vyama hivyo



Dar es Salaam. Kamati Kuu Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, imeridhia mwendelezo wa mazungumzo na makubaliano ya kufikia mwafaka kati ya chama hicho na ACT-Wazalendo, huku ikitarajiwa tamko la pamoja litakalobainisha yaliyokubaliwa baada ya kukamilika kwa taratibu za mwisho.

Hata hivyo, mambo hayo waliyokubaliana bado hayajatangazwa rasmi, ingawa vyanzo vyetu vilivyo ndani ya vyama hivyo vinadai kuwa, miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na uwezekano wa kuandaliwa upya kwa Katiba ya Zanzibar na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchunguzi kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Julai 4, 2026, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto amesema Kamati Kuu Maalumu ilipokea taarifa ya mwenendo wa mazungumzo kati ya CCM na ACT-Wazalendo kuhusu ajenda ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ambayo iliwasilishwa jana Jumamosi, Julai 3, 2026 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

"CCM ilipokea taarifa ya mwenendo wa mazungumzo kati ya chama na ACT-Wazalendo yanayosimamiwa na marais wastaafu," amesema Mbeto.

Amesema baada ya wajumbe wa Kamati Kuu Maalumu kupokea mrejesho huo, walikubaliana kwa kauli moja kuwepo kwa tamko la pamoja litakalotolewa na pande zote mbili ili kueleza hatua iliyofikiwa katika mchakato huo.

"Tumefikia mwafaka kuwapo na tamko la pamoja kati ya ACT-Wazalendo na CCM ambalo litatolewa kwa pamoja na ndilo litakaloeleza mustakabali wa hatua zinazofuata," amesema.

Mbeto amesema tamko hilo litabeba maudhui ya makubaliano yaliyofikiwa, ambayo yatatangazwa hadharani mara litakaposomwa na viongozi wa pande zote mbili.

Hata hivyo, amesema muda wa kutolewa kwa tamko hilo bado haujapangwa, akieleza kuwa taratibu za mwisho za kulisaini zinaendelea.

"Baada ya tamko hilo kutolewa ndipo litaeleza hatua zinazofuata. Kwa sasa tunasubiri kukamilika kwa taratibu za kusaini na utekelezaji wake," amesema.

Wakati hayo yakielezwa na CCM, taarifa kutoka kwa vyanzo vyetu zinaeleza kuwa miongoni mwa mapendekezo yaliyowasilishwa na ACT-Wazalendo katika mazungumzo hayo ni kuundwa kwa Tume Huru ya Uchunguzi itakayochunguza mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, tume hiyo inapendekezwa kuchunguza mchakato mzima wa uchaguzi huo, kubaini changamoto zilizojitokeza na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha mchakato wa uchaguzi wa baadaye.

Aidha, vyanzo hivyo vinaeleza kuwa suala jingine lililojadiliwa ni uwezekano wa kuandikwa upya kwa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2010, ili kuiweka katika mazingira ya sasa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Mazungumzo ya kutafuta mwafaka Zanzibar yalianza Novemba 2025 yakihusisha pande mbili, ambapo kwa upande wa CCM yakisimamiwa na marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein.

Kwa upande wa ACT-Wazalendo, mazungumzo hayo yaliwakilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud Othman pamoja na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Juma Duni Haji.

Inadaiwa kuwa taarifa ya mwenendo wa mazungumzo hayo pia ilijadiliwa na kupitishwa katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika Juni 29, 2026 chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman amedokeza kuwa mazungumzo hayo yamefikia hatua nzuri na kuwataka wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi kusubiri taarifa rasmi.

"Mambo yenu yapo vizuri na tupo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wake. Kwa vile mmetuamini sisi, tunawahakikishia kuwa tutapambania haki zenu," amesema.

Wakati huo huo, Makamu Mwenyekiti wa ACT - Wazalendo, Zanzibar Ismail Jussa amesema wanashukuru kwa hatua iliyofikiwa katika mazungumzo yao na CCM ya kusaka mwafaka katika kisiwa hicho.

“Tunasubiria taarifa kutoka CCM, ili hatua zingine zifuate. Lakini tunashukuru kwa hatua hii, maana sisi tulishavuka huko, tulikuwa tunawasubiria wenzetu wa CCM,” amesema Jussa.

Jussa amefichua kuwa kikao cha Juni 30 cha kamati ya uongozi ya ACT- Wazalendo kilipitisha hatua zilizofikiwa katika mazungumo hayo huku Duni na Othman wakipewa mamlaka ya kukamilisha ngazi zinazofuata.

“Hatua inayofuata ni utekelezaji sasa ambao unahusu kutoa tamko la pamoja ili wananchi kujulishwa,” ameeleza Jussa.