Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Moshi mweupe mwafaka wa SUK Zanzibar

Muktasari:

  • Iwapo SUK haitaundwa, si lazima migogoro itokee mara moja, lakini hatari ya kurejea kwa mvutano wa kisiasa Zanzibar itaongezeka



Dar es Salaam. Mwenyekiti wa ACT - Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema mazungumzo yanayoendelea kuhusu mwafaka wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) yamefikia hatua nzuri, huku akiwataka wanachama na wafuasi wa chama hicho kusubiri taarifa muhimu zinazotarajiwa kutolewa wiki hii.

Othman ametoa kauli hiyo jana, Alhamisi Julai 2, 2026, wakati akizungumza na wanachama wa ACT - Wazalendo na wananchi waliojitokeza katika ukaguzi wa ujenzi wa ofisi ya chama hicho Tawi la Pandani, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

"Najua mnaniuliza mambo yetu vipi sasa? Mambo yetu yapo vizuri. Nyie (ninyi) mlichukua masuala yenu mkawakabidhi watu sahihi, yapo vizuri. Inshallah tupo mwishoni mwa kuyaweka sawa. Wiki hii tegeni sikio," amesema.

Ameongeza kuwa viongozi wa chama hicho wanaendelea kusimamia mazungumzo hayo kwa lengo la kuhakikisha haki na matarajio ya wananchi yanazingatiwa.

"Mambo yenu yapo vizuri, tupo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wake. Kwa vile mmetuamini sisi, tunawahakikishia kuwa tumepambania haki zenu," amesema.

Kauli ya Othman inakuja wakati taarifa mbalimbali zikidai kuwa mazungumzo kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT - Wazalendo kuhusu mwafaka wa SUK yamefikia hatua ya mwisho, baada ya makubaliano yaliyofikiwa katika timu za mazungumzo kudaiwa kupata baraka kutoka vikao vya juu vya CCM.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchiimezipata kutoka vyanzo vya ndani, mchakato wa mazungumzo hayo ulioanza Novemba mwaka jana na kudumu kwa takribani miezi minane, umekamilika katika ngazi ya majadiliano, huku kila upande ukitarajiwa kukamilisha taratibu zake za ndani kabla ya kutolewa kwa taarifa rasmi.

Chanzo kimoja kimeeleza kuwa, kilichobaki ni kila chama kutoa mrejesho kwa vikao vyake, huku CCM ikidaiwa kuwa tayari imewasilisha taarifa hiyo na kupata ridhaa ya kuendelea na hatua zinazofuata.

"Ilibaki kwa kila upande kuripoti kwa chama chake na CCM imeripoti kwenye vikao vyake na vikaridhia mambo yaliyokubaliwa kufanyiwa kazi," kimesema chanzo hicho.

Chanzo hicho kinadai kuwa Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar inatarajiwa kukutana leo, Ijumaa, kwa ajili ya kupokea taarifa ya mazungumzo hayo, ingawa kikao hicho hakikutarajiwa kufanya uamuzi mpya kwa kuwa uamuzi wa msingi tayari umefanyika.

Alipotafutwa na Mwananchi, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Zanzibar, Khamis Mbetto azungumzie hilo, amethibitisha kuwapo kwa kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Zanzibar, kitakachoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Hata hivyo, hakufafanua ajenda za kikao hicho.

"Kuna ajenda zitakazowasilishwa katika kikao. Tusubiri kikao kimalizike, ndipo tutatoa taarifa kwa umma kuhusu yaliyojiri," amesema.

Mbetto amesema iwapo kutakuwa na maelekezo kutoka katika vikao vya chama, CCM itaielekeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kutekeleza makubaliano yatakayokuwa yamefikiwa.

Mazungumzo kati ya CCM na ACT -Wazalendo yanaongozwa na marais wastaafu wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Amani Abeid Karume, huku upande wa ACT - Wazalendo ukiongozwa na Othman Masoud na Juma Duni Haji.

Taarifa ambazo Mwananchiimezipata zinaeleza kuwa, viongozi hao huenda wakakutana kesho Jumamosi, Julai 4, 2026, kwa ajili ya kujadili hatua za mwisho za mchakato huo kabla ya kutolewa kwa tamko rasmi.


SUK na umuhimu wake

Akizungumzia umuhimu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, mchambuzi wa masuala ya siasa, Mbaraka Hamisi Khamis amesema mfumo huo umekuwa chombo muhimu cha kujenga maridhiano ya kisiasa, kuimarisha utulivu na kuongeza imani ya wananchi katika mchakato wa kidemokrasia.

Amesema SUK hutoa nafasi kwa vyama vikuu vya siasa kushiriki katika uongozi na maamuzi yanayohusu mustakabali wa Zanzibar, jambo linalosaidia kupunguza hisia za kutengwa kwa baadhi ya makundi ya kisiasa na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

"SUK haishii kuwa makubaliano ya kugawana madaraka tu. Inajenga amani ya kudumu, inapunguza migawanyiko ya kisiasa na kuweka mazingira yanayowawezesha wananchi kushiriki maendeleo bila hofu ya migogoro ya kisiasa," amesema.

Akirejea kauli ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, kwamba aliwahi kupata wakati mgumu kuiongoza Zanzibar bila Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Khamis amesema mfumo huo ulianzishwa mahsusi kwa lengo la kuimarisha maridhiano ya kisiasa.

Amesema kutokuwapo kwa SUK kunaweza kuongeza taharuki za kisiasa, kuibua malalamiko kuhusu ushirikishwaji katika uongozi na kudhoofisha juhudi za maridhiano zilizojengwa kwa miaka mingi.

Aidha, amesema mazingira ya kutokuaminiana kati ya wadau wa siasa yanaweza kuathiri utulivu wa kijamii, uwekezaji na taswira ya Zanzibar mbele ya jumuiya ya kimataifa, hasa katika kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.

"Iwapo SUK haitaundwa, si lazima migogoro itokee mara moja, lakini hatari ya kurejea kwa mvutano wa kisiasa Zanzibar itaongezeka. Ndiyo maana mazungumzo yanayoendelea yanapaswa kupewa kipaumbele kwa masilahi mapana ya Zanzibar na wananchi wake," amesema.