Kauli ya Serikali kuhusu Julai 7
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na Sheria ya Jeshi la Polisi, mikusanyiko yote ya hadhara inapaswa kufuata taratibu za kisheria na yeyote atakayekiuka atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amewataka wananchi, wakiwamo madereva bodaboda, bajaji na wajasiriamali wadogo nchini, kuendelea na shughuli zao kama kawaida ifikapo Julai 7, 2026 akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unakuwapo.
Katambi ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Julai 4, 2026, jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na makundi ya wajasiriamali wakiwamo bodaboda, waendesha bajaji, Machinga na mamalishe na babalishe, waliokutana kujadili hali ya usalama na kuonesha msimamo wao wa kulinda amani ya nchi.
Amesema kumekuwa na mzaha wa mara kwa mara wa baadhi ya watu kutangaza maandamano yasiyofuata sheria, akieleza kuwa, Serikali haitavumilia vitendo vyovyote vinavyolenga kuvuruga amani ya nchi.
“Bodaboda nchi nzima endeleeni na shughuli zenu, wafanyabiashara fungua biashara zenu mtakuwa salama. Wanaosema hakuna usalama, ni sisi tupo tayari muda wowote na hatuhitaji kupangiwa tarehe,” amesema Katambi.
Amesema matukio ya aina hiyo hayapaswi kuchukuliwa kwa wepesi, akitolea mfano wa matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025, pamoja na madai ya maandalizi ya matukio mengine, akisisitiza kuwa, Serikali imejipanga kuyadhibiti kwa mujibu wa sheria.
“Tumeshashuhudia mzaha wa kuchezea amani ya Taifa. Watu wanapanga maandamano yasiyofuata utaratibu wa kisheria. Hii haikubaliki na Serikali itachukua hatua kali,” amesema.
Katambi amesema kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na Sheria ya Jeshi la Polisi, mikusanyiko yote ya hadhara inapaswa kufuata taratibu za kisheria na yeyote atakayekiuka atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Yeyote atakayetamka kuwa kutakuwa na maandamano bila kufuata utaratibu wa kisheria atakuwa anafanya uchochezi,” amesema.
Amesema pia vipeperushi vinavyosambazwa mitandaoni vikidai kuwa shule zitafungwa Julai 7 si vya kweli, akisisitiza kuwa shughuli zote zitaendelea kama kawaida.
“Shule hazitafungwa, hakuna shughuli yoyote itakayosimama. Serikali ipo imara kulinda uhai wa wananchi wake kwa gharama yoyote,” amesema.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi akiwa kwenye pikipiki baada ya kuzungumza na makundi mbalimbali ya wajasiriamali mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha, amewataka wananchi kutojihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama, akisema Serikali haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayehatarisha maisha au mali za watu wengine.
“Mtu yeyote atakayehatarisha usalama wa wananchi au mali zao, Serikali itamchukulia hatua kwa mujibu wa sheria. Hakuna mtu atakayekuwa juu ya sheria,” amesisitiza.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahmoud amewataka madereva bodaboda, bajaji, maguta na wafanyabiashara wadogo kuwa mabalozi wa amani na kuepuka kushiriki au kutumika katika migogoro.
Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kujaribu kuhusisha bodaboda na matukio ya uvunjifu wa amani, jambo alilosisitiza halina uhalisia kwa walio wengi.
“Hii sekta ni ya watu wanaotafuta riziki halali. Haiwakilishi uhalifu. Tuwalinde na tuendelee kuwa sehemu ya kulinda amani,” amesema.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Machinga Taifa, Steven Lusinde amesema wajasiriamali hao hawapo tayari kushiriki maandamano, akisisitiza kuwa wataendelea na shughuli zao na kulinda amani ya nchi.
“Sisi hatutakubali kuvuruga amani. Tutafanya kazi zetu kama kawaida na Polisi waimarishe ulinzi,” amesema.
Katibu wa Shirikisho la Waendesha Bodaboda Dar es Salaam, Michael Riganya amesema lengo la mkutano huo ni kuimarisha ushirikiano kati ya makundi hayo na Serikali katika kulinda amani.
Amesema bodaboda wanatambua mchango wa Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara hiyo na wameomba kuunganishwa kwa mifumo yao ya kidijitali na ya Jeshi la Polisi ili kuboresha ufuatiliaji na usalama.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Waendesha Bodaboda, Said Kachenja amesema zaidi ya waendesha bodaboda 600,000 wako Dar es Salaam na takriban milioni tatu nchini kote na wote wapo tayari kulinda amani na kuendelea na shughuli zao.
“Tunasema hatutaki maandamano. Tunataka kufanya kazi zetu kwa amani. Julai 7 tunaomba turuhusiwe kufanya shughuli zetu kama kawaida,” amesema.