Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Katambi agusia tena mikutano ya hadhara, masharti nyumba za kulala wageni

Muktasari:

  • Siku chache baada ya agizo la matumizi ya Kitambulisho cha Taifa kuzua mjadala, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amefafanua kuwa si Nida pekee inayoweza kutumika kusajili wageni wa hoteli na nyumba za kulala wageni.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi amesema kitambulisho cha Taifa (Nida) si nyaraka pekee itakayotumika kusajili wageni katika hoteli na nyumba za kulala wageni, akifafanua agizo lake lililozua mjadala.

Ametaja vitambulisho vinavyoweza kutumika kimojawapo ni Kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha mpiga kura, leseni ya udereva, namba ya Nida, hati ya kusafiria (passort) au cheti cha kuzaliwa.

Rejea ya kauli ya Waziri huyo iliyoibua gumzo aliwaelekeza wamiliki wa nyumba za wageni, Airbnb na loji kote nchini kuhakikisha wageni wote wanasajiliwa kwa Nida, huku akionya hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka maelekezo hayo.

Mbali na kutoa ufafanuzi huo, Katambi amesema anashangazwa na wanaodai hana mamlaka ya kuzuia mikutano ya hadhara, akisisitiza hatua aliyoitangaza haihusiani na kutangazwa kwa hali ya hatari, ambayo kikatiba ni mamlaka ya Rais.

Ufafanuzi huo unakuja siku chache baada ya Waziri huyo, Juni 26, 2026, akijibu mwongozo bungeni jijini Dodoma kutoa maelekezo hayo ikiwemo marufuku ya mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Katika maelekezo yake kwenye agizo hilo, alimwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillius Wambura kusitisha utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa kwa kipindi hicho, akieleza hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama na kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza.

Amesema Serikali imebaini uwepo wa matishio ya kiusalama, ikiwemo watu wanaodaiwa kukamatwa wakiwa na silaha na mafuta ya petroli pamoja na mipango ya kufanya vitendo vya uhalifu, hivyo vyombo vya ulinzi na usalama vimeagizwa kuongeza ulinzi katika maeneo yenye viashiria vya hatari.

Kuhusu matumizi ya Nida, baadhi ya wataalamu wa sheria na wamiliki wa nyumba za kulala wageni walieleza kuwa utekelezaji wa agizo hilo ni mgumu kwa sababu si Watanzania wote wana Kitambulisho cha Taifa. Wengine wamepata namba za Nida pekee, huku wengine wakiwa hawajapata kabisa vitambulisho hivyo.


Tutumie nyaraka hizi

Akizungumza Juni 29, 2026 kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Waziri Katambi amesema Nida ilipewa kipaumbele kwa sababu ni kitambulisho ambacho hakiwezi kughushiwa kirahisi.

Hata hivyo, amesema pale ambapo hakipatikani, wamiliki wa nyumba za kulala wageni wanaweza kutumia nyaraka nyingine rasmi.

Vitambulisho na nyaraka hizo ni Kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha mpigakura, leseni ya udereva, namba ya Nida, hati ya kusafiria na cheti cha kuzaliwa.

Pia Waziri Katambi amesema mwenyeji anatakiwa pia kuchukua namba ya simu ya mgeni kwa ajili ya utambuzi.

"Lengo letu ni kufuatilia (tracking) kwamba huyu mtu aliyelala kwako tujue ni raia wa Tanzania. Hatutaki kujua amekuja kufanya nini wala kuingilia mambo yake binafsi kwa kuwa tuna Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022," amesema.

Waziri Katambi amesema endapo mtu hatakuwa na nyaraka hizo, anaweza kutumia cheti cha kuzaliwa au nyaraka nyingine rasmi zinazoweza kuthibitisha utambulisho wake.

"Ukiona mtu hana vyote hivyo, basi jitafakari, anaweza kutumia cheti cha kuzaliwa au nyaraka nyingine yoyote inayoweza kuthibitisha utambulisho wake," amesema.

Amesema kama mtu ni Mtanzania, anapaswa kuwa na angalau moja ya nyaraka hizo kwa kuwa baadhi yake hutolewa bila malipo.

"Kama ni mgeni, hana shida kwa sababu ana hati ya kusafiria, hawezi kuingia nchini bila kufuata taratibu. Tusifanye siasa kwenye masuala ya ulinzi na usalama. Wakati mwingine uhalifu unaongezeka kwa kupuuza taarifa muhimu za kiusalama," amesema.


Mikutano ya hadhara

Akizungumzia ukosoaji wa agizo lake la kusitisha mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, Waziri Katambi amesema anashangazwa na wanaodai hana mamlaka ya kutoa maelekezo hayo.

Amesisitiza hatua hiyo haihusiani na kutangazwa kwa hali ya hatari, ambayo Kikatiba ni mamlaka ya Rais.

Katambi amesema mamlaka ya Rais kuhusu kutangaza hali ya hatari ni tofauti na wajibu wa kila wizara katika kusimamia sekta iliyo chini ya dhamana yake.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameunda Serikali na kuzipa wizara majukumu ya kusimamia sekta mbalimbali, hivyo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina wajibu wa kusimamia masuala ya ulinzi na usalama.

Akinukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema Ibara ya 3 inaitambua Tanzania kuwa nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia, huku Ibara ya 8(1) (b) ikiitaka Serikali kuhakikisha ustawi na usalama wa wananchi.

Waziri Katambi amesema yapo matishio ya kiusalama yanayolazimu Serikali kuchukua tahadhari.

Amedai kuna watu wanaotuma ujumbe mfupi na wengine hufika ofisini kwake kutoa taarifa kuhusu mipango ya kufanya vurugu katika tarehe iliyotajwa ya Juni 7, 2026.

"Mimi ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Nimepewa jukumu hili kwa kiapo mbele ya Mungu, hivyo nina wajibu wa kuhakikisha nchi inakuwa salama. Kutofanya hivyo ni kushindwa kutekeleza wajibu wangu," amesema.

Amesema kwa sasa kuna vipeperushi vinavyosambazwa na kauli mbalimbali zinazochochea vurugu.

"Wanaharakati wamesikika wakihamasisha maandamano, baadhi ya viongozi wa dini wameonekana kuunga mkono, cha kusikitisha zaidi ni kuona viongozi wa dini wakimpinga Katambi wakati lengo ni kuzuia umwagaji wa damu, kwa sababu vurugu hazina macho; zinaweza kuathiri Serikali na raia kwa pamoja," amesema.

Akitoa wito kwa vijana, Waziri Katambi amesema yupo tayari kupokea hoja za mtu yeyote mwenye malalamiko na kuzifikisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili zipatiwe ufumbuzi kwa njia ya amani.