Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Katambi aeleza utaratibu wa maandamano, mikusanyiko ya hadhara

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Julai 2, 2026 kuhusu misingi na taratibu zinazopaswa kufuatwa kwa mujibu wa Katiba na sheria katika uandaaji wa mikutano ya hadhara, maandamano na mikusanyiko. Picha na Michael Matemanga.

Muktasari:

  • Juni 26, 2026 akiwa Bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Patrobas Katambi alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillus Wambura kusitisha utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Dar es Salaam. Baada ya wadau mbalimbali kukosoa hatua ya Serikali kusitisha mikutano ya kisiasa ya hadhara, Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, amefafanua utaratibu unaopaswa kufuatwa kwa mujibu wa Katiba na sheria kuhusu maandamano na mikusanyiko ya hadhara.

Julai 26, 2026, akiwa Bungeni jijini Dodoma, Katambi alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura, kusitisha utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara.

Hatua hiyo alitaja ililenga kuimarisha usalama na kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza baada ya Serikali kubaini kuwepo kwa viashiria vya tishio la usalama.

Tamko hilo lilizua mjadala na kukosolewa na wanasheria, wanasiasa na wanaharakati, akiwemo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambacho kilitangaza nia ya kumfungulia kesi mahakamani Waziri Katambi kikidai amevunja Katiba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 2,2026 jijini Dar es Salaam, Waziri  Katambi amesema usimamizi wa maandamano na mikusanyiko ya hadhara unaongozwa na Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, Sura ya 322, kwa kuzingatia vifungu vya 42, 43, 44, 45 na 46.

Amesema Kifungu cha 42 kinalipa Jeshi la Polisi mamlaka ya kusimamia na kuratibu mikusanyiko ya aina yoyote nchini.

"Kifungu cha 43 kinaelekeza kuwa mtu au waandaaji wanaokusudia kufanya mkusanyiko au maandamano katika eneo la umma wanapaswa kuwasilisha taarifa ya maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa eneo husika (Kamanda wa Polisi wa Wilaya) angalau saa 48 kabla ya tukio," amesema Katambi.

Amesema taarifa hiyo inapaswa kueleza mahali na muda wa mkusanyiko, madhumuni yake pamoja na taarifa nyingine zinazohitajika kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa Katambi, baada ya taarifa kuwasilishwa waandaaji wataendelea na maandalizi isipokuwa pale Mkuu wa Polisi wa eneo husika akitoa amri ya kuuzuia mkusanyiko huo.

Amesema amri hiyo inatolewa endapo kutakuwa na sababu za msingi zinazoonyesha mkusanyiko au maandamano yanavunja amani, kuhatarisha usalama wa umma, kuathiri utulivu wa jamii au kutumika kwa madhumuni yasiyo halali.

Aidha, amesema Kifungu cha 44 kinaipa Jeshi la Polisi mamlaka ya kusimamisha au kuvunja mkusanyiko au maandamano ikiwa kuna sababu za msingi za kuamini kuwa kuendelea kwake kutavunja amani.

Katambi amesema Kifungu cha 45 kinaelekeza kuwa watu wawili au zaidi watakaokataa kutii amri halali ya kutawanyika iliyotolewa chini ya vifungu vya 43 au 44, mkusanyiko wao utahesabika kuwa si halali kisheria.

"Ni muhimu umma ukafahamu tofauti kati ya kutoa taarifa na kuomba kibali, kifungu cha 43 kinazungumzia utoaji wa taarifa kwa Jeshi la Polisi, huku sheria hiyo hiyo ikilipa Jeshi la Polisi mamlaka ya kuzuia mkusanyiko endapo kutakuwa na sababu zinazohusu usalama na masilahi ya umma," amesema.

Amesisitiza kufanya mikutano ya hadhara ni haki ya kikatiba, lakini utekelezaji wa haki hiyo unaambatana na wajibu wa kuzingatia sheria na mipaka iliyowekwa.

Hata hivyo, katika mkutano huo Waziri Katambi hakuruhusu waandishi wa habari kuuliza maswali.

Akizungumzia ufafanuzi wa Waziri, mchambuzi wa masuala ya siasa, Noel Shao, amesema hatua hiyo inalenga kuweka uwiano kati ya haki za wananchi na wajibu wa Serikali wa kulinda amani.

"Bado kuna sintofahamu kuhusu mipaka ya mamlaka ya Serikali katika kuzuia mikutano ya kisiasa. Hali hiyo inaonyesha umuhimu wa tafsiri ya sheria kufanywa kwa uwazi na kwa kuzingatia haki za msingi za wananchi," amesema Shao.

Naye mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, Magabilo Masambu, amesema Serikali inapaswa pia kuwazuia watendaji wake kutumia mikutano ya hadhara kuwakejeli wapinzani, akisema hali hiyo inaweza kuchochea hisia za kutokuwapo kwa usawa katika utekelezaji wa sheria na kuongeza mvutano wa kisiasa.