Makubaliano CCM, ACT kuundiwa chombo cha kuratibu utekelezaji
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi akiwa kwenye picha na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa Othman Masoud Othman baada ya kushuhudia utiaji saini wa ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili kwa ajili ya kufanyiwa kazi kufuatia Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar Julai 9, 2026.
Chombo maalumu kitakachoratibu na kusimamia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT- Wazalendo, kitaundwa chini ya sheria ili kufanikisha jambo hilo.
Hayo yamebainishwa leo Julai 9, 2026 mjini Unguja, Zanzibar wakati wa hafla ya utiaji saini wa tamko la pamoja baina ya vyama hivyo baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa takribani miezi minane, chini ya uongozi wa marais wastaafu, Amani Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein.
Akiwasilisha tamko hilo, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ambaye pia ni katibu wa kamati ya mazungumzo hayo, Mansura Mossi Kassim amesema hatua ya mwanzo ya mazungumzo hayo imekamilika na itafuatiwa na hatua nyingine.
“Baada ya kukamilika kwa hatua ya mwanzo, inafuatiwa na hatua hii ya kutolewa kwa tamko hili na kufuatiwa na hatua nyingine kadhaa ikiwamo mazungumzo kama ilivyopangwa katika ratiba iliyokubaliwa na pande zote mbili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi, Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa Othman Masoud Othman pamoja na viongozi mbalimbali kwenye hafla ya uwasilishaji wa Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar Julai 9, 2026.
Amesema tukio hilo linaainisha azma ya pande hizi mbili kuendelea kufanya kazi pamoja ili kupata ufumbuzi wa kudumu na endelevu wa changamoto zinazoikabili Zanzibar kisiasa, kijamii na katika uendeshaji wa shughuli za umma.
“Kwamba, tamko hili la pamoja linaambatana na ajenda zilizokubaliwa na kutiwa saini na pande zote mbili na ajenda hizo zitajadiliwa katika kamati ya pamoja itakayoshauri juu ya mfumo, taratibu na upeo wa utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa hatua kwa hatua.”
“Katika kufanikisha hili, chombo maalumu kitaundwa chini ya sheria ili kuratibu na kusimamia utekelezaji wa makubaliano haya,” amesema Mansura wakati akisoma tamko hilo la pamoja baina ya vyama hivyo.