Dhana hasi matumizi gesi asilia kwenye magari

Dar es Salaam. Matumizi ya gesi asilia kwenye magari yanamuondolea mmiliki takribani nusu ya maumivu ya bei ya mafuta pamoja na mawazo juu ya mabadiliko ya bei hizo yanayofanyika kila wakati.

Watumiaji hawa hawana mawazo ya bei ya upatikanaji wa nishati wanayotumia kwa sababu wanatumia Sh1,550 pekee kwa kilo moja ya gesi wakati wote.

Changamoto iliyopo sasa ni foleni wakati wa kujaza gesi, gharama kubwa ya kubadilisha mfumo wa mafuta kuwa wa gesi, lakini kubwa zaidi ni hofu ya usalama wa magari baada ya kuweka mfumo huo.

Mmoja wa madereva teksi mtandao aliliambia gazeti hili kuwa licha ya maumivu ya bei za mafuta, bado hayuko tayari kubadili gari lake kuingia katika mfumo wa gesi.

Alisema anasita kubadili mfumo wa gari lake kwenda matumizi ya gesi, kwa kuwa kuna dhana kuwa kubadili mifumo ya gari huifanya gari kukosa nguvu.

“Siyo kwamba sina hela maana kuna kampuni zinakopesha mifumo sasa hivi, lakini wafungaji wengi wa kubadili hii mifumo Tanzania bado nina wasiwasi nao, maana endapo watafanya si kwa kiwango cha ubora unaotakiwa unaweza kufanya gari ikose nguvu,” alisema Hassan.

Mawazo ya Hassan wanayo wamiliki wengi wa magari na yaliungwa mkono na Martin Minja, ambaye bila kutaja sehemu aliyowahi kufungiwa mfumo huo kwenye gari lake, alikiri kuwa liliwahi kumletea shida.

“Nikawa kama silielewi, kuna wakati nikiendesha linaishiwa nguvu, linazima, unabadili kurudi kwenye mafuta, nikaona nitafute usaidizi, nikapeleka sehemu nyingine ambayo wanafunga mifumo hiyo.”

Alipoulizwa juu ya suala hilo, mmoja wa watoa huduma katika kampuni inayobadili mifumo ya gari kwenda kwenye gesi, alisema kabla hawajamfungia mteja humuelezea mabadiliko anayoweza kukutana nayo baada ya kuanza kutumia mfumo mpya.

Wanafanya hivyo ili kuhakikisha mteja akiona tofauti katika gari lake isimpe mshtuko na kuhisi kama ameharibu gari, badala ya kupata ahueni aliyokuwa akiitafuta.

"Unajua unapobadili mfumo wa gari lako hakuna matatizo kama watu wanavyodhani kuwa linakosa nguvu, si kweli, kinachobadilika ni pale unapowasha tu, gari litachelewa kuchanganya tofauti na ulivyokuwa ukitumia mafuta, lakini baada ya hapo nguvu ni sawa na ile ya kwenye mafuta," alisema fundi huyo.

Alisema moja ya vitu wanavyozingatia katika ufungaji huo ni kuhakikisha hawaathiri mfumo wa umeme katika gari, ili kumfanya mteja afurahie anachokifanya.

"Hata matengenezo ya gari mteja atakuwa anafanya katika sehemu alizozoea, kama ana gereji yake sawa, ila tunamshauri kila baada ya miezi sita afanye ‘service’ kwenye mfumo wake wa gesi, ili aendelee kufurahia," alisema.

Meneja wa mradi wa kuunganisha mfumo wa gesi asili katika magari (CNG) katika Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Dk Esebi Nyari alishauri ili kuepukana na hali hiyo ni vyema wamiliki wa magari kuhakikisha ubadilishaji wa mfumo huo unafanywa na watu wazoefu.

“Akiwa si mzoefu anaweza kufanya gari lisifanye kazi vizuri, kuna namna unatakiwa kuhakikisha uimara wa gari unaendelea kubaki sawa kama ilivyokuwa ikitumia mafuta,” alisema Nyari.

Alisema kutokana na kutambua hali hiyo, DIT walianza kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo mafundi wanaotengeneza mifumo, ili isilete shida kwa watumiaji baadaye.

“Tulishapokea kesi nyingi za aina hii, tuliwasaidia na gari zikawa sawa, unajua hiki ni kitu kipya, ndiyo maana DIT tuliona tuanzishe kozi hii ya kujenga huu uwezo wanaofanya shughuli hizi, kwani jukumu letu ni kuhakikisha watu wanakuwa na uwezo wa kufunga mifumo hiyo vizuri,” alisema Dk Nyari.

DIT ni taasisi ya Serikali ambayo ilianza kutoa huduma za kubadili mifumo ya magari kutoka mafuta kwenda gesi asilia, kabla ya kampuni mbalimbali kuingia sokoni kuleta ushindani.

Ushindani huo umezidi kukua zaidi na wengine wameenda mbali badala ya kuwataka watu kulipia fedha taslimu, sasa wanawakopesha wamiliki na kutakiwa kulipa kidogokidogo.

Hata hivyo, mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude alisema kadiri muda unavyokwenda na matumizi ya gesi kuongezeka na kutengeneza soko la uhakika anaamini uingizaji wa magari yaliyo na mifumo ya gesi moja kwa moja utaanza.

Hiyo itaondoa ulazima wa watu kubadili mifumo yao kutoka kwenye mafuta kwenda kwenye gesi unaofanyika sasa ambao kwa kiasi umekuwa na maoni tofauti, ikiwemo watu kudai magari yao yanakosa nguvu.

"Kama tutaamua kwenda katika mfumo wa gesi na kufanya uwekezaji wa kutosha, nafikiri baada ya muda fulani kama nchi itaanza kuagiza magari ambayo tayari yametengenezwa kwa mfumo wa gesi, tofauti na sasa ambapo watu wanabadili mifumo hii ambayo inafanya baadhi ya watu kudai kuwa ubadilishaji huo unafanya magari yao nguvu kupungua," alisema Mkude.


Elimu changamoto

Wakati wengine wakiwa na wasiwasi juu ya mabadiliko hayo ya nishati ya kuendesha magari yao, Grace Mollel alisema changamoto inayomfanya asihamie kwenye nishati ya gesi ni elimu juu ya mfumo huo.

"Nipewe elimu kuhusu matumizi yake nitafanya maamuzi, ila kwa sasa sina uelewa,” alisema.

Mollel aliungwa mkono na Tunu Msika, aliyesema kwa upande wake haelewi chochote kuhusu matumizi ya CNG kwenye magari.

"Sijui chochote kuhusu mfumo huo, nashindwa hata niseme nini, ila nikipewa elimu basi najua nini cha kufanya," alisema Msika.

Aidha, Mkuu wa kitengo cha uhusiano na mawasiliano ya umma cha TPDC, Maria Mselem alisema elimu inatolewa na inaendelea kutolewa kwa jamii na ni endelevu.

“Tunatoa elimu labda ambao hawajaipata watakuwa bado hawajafikiwa, ila watafikiwa kwa kuwa elimu inatolewa kuanzia kwenye luninga, redio, kwenye makongamano hadi kwenye magazeti,” alisema Mselem.

Aliongeza kuwa elimu hiyo inatolewa hata kwenye maonyesho ya kitaifa na majukwaa mengine. “Hata waandishi wanaandika sana faida za gesi asilia, jinsi gani mtu anaweza akaokoa hela, vyote vinafanyika na ni elimu endelevu,” alisema.