EAC, EU kuwekeza Sh84 bilioni kwenye soko la kidijitali Afrika
Kaimu Mkuu wa Ushirikiano wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na EAC, Paola Trevisan, akizungumza katika uzinduzi wa program ya kidigitali Afrika
Muktasari:
- Lengo la uwekezaji huo ni kuongeza biashara kati ya Afrika na Ulaya na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wote wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Arusha. Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya wanatarajia kuwekeza Euro 28 milioni (Sh84 bilioni) katika kuimarisha soko la kidijitali la Afrika.
Lengo la uwekezaji huo ni kuongeza biashara kati ya Afrika na Ulaya na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wa Ukanda wa Afrika Mashariki.
Uwekezaji huo unatekelezwa kupitia programu ya EU-EAC Digital Economy, E-Commerce, E-Payments and Public E-Services (DEEP), inayolenga kuharakisha ujumuishaji wa kidijitali, kuimarisha biashara ya mipakani na kuongeza ushindani wa Afrika Mashariki katika uchumi wa kidijitali duniani.
Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika leo Jumanne, Juni 23, 2026, jijini Arusha kwenye Jukwaa la EAC la Teknolojia ya Kidijitali D4D 2026 lenye kaulimbiu isemayo; “Kutoka Mkakati hadi Utekelezaji: Kujenga Soko Moja la Kidijitali.”
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kaimu Mkuu wa Ushirikiano wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na EAC, Paola Trevisan, amesema lengo kuu la programu hiyo ni kujenga soko moja la kidijitali la Afrika lenye uendelevu na kuharakisha biashara kati ya Afrika na Ulaya.
Amesema programu hiyo inajikita katika maeneo matano muhimu ambayo ni utawala wa kidijitali, biashara mtandaoni, malipo ya kidijitali, huduma za umma za kidijitali na usalama wa mifumo ya mtandao.
Kwa mujibu wa Trevisan, mpango huo pia utaunga mkono utekelezaji wa mikakati ya kidijitali ya EAC na Umoja wa Afrika pamoja na kuchangia utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Aidha, hatua hiyo inakuja wakati biashara kati ya Afrika na Ulaya kwa sasa inakadiriwa kufikia Euro 355 bilioni (Sh1,065 trilioni) kwa mwaka, huku Afrika ikisafirisha bidhaa zenye thamani ya Euro 196 bilioni (Sh588 trilioni) kwenda Ulaya na kuagiza bidhaa zenye thamani ya Euro 165 bilioni (Sh495 trilioni).
Akizungumza katika jukwaa hilo, Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Forodha, Biashara na Masuala ya Fedha, Annette Ssemuwemba, amesema uchumi wa kidijitali ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya EAC 2050, Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika na Eneo Huru la Biashara la Afrika.
Amesema mabadiliko ya kidijitali yana uwezo wa kuongeza biashara na uwekezaji, kuboresha huduma za umma na kuunda ajira mpya hasa kwa wanawake na vijana.
“Uchumi wa kidijitali wa Afrika unatarajiwa kufikia Dola 712 bilioni za Marekani (Sh1,780 trilioni) ifikapo mwaka 2050, hivyo huu ni wakati ambao hatuwezi kuupoteza,” amesema.
Amesema EAC tayari imeandaa mikakati mbalimbali ikiwemo Mkakati wa Mabadiliko ya Kidijitali, Mkakati wa Biashara Mtandaoni na Mpango Mkuu wa Malipo ya Simu wa Kuvuka Mipaka.
Amesisitiza kuwa wakati umefika kwa nchi wanachama kuondoka kwenye mipango na kuanza utekelezaji wa vitendo ili kuhakikisha wananchi wananufaika na uchumi wa kidijitali.
Ameeleza kuwa wafanyabiashara wa mipakani hasa wanawake watanufaika kupitia mifumo ya malipo ya kidijitali itakayorahisisha miamala, kupunguza gharama za ubadilishaji fedha na kucheleweshwa kwa malipo.
Changamoto zilizotajwa ni tofauti za mifumo ya sheria na kanuni, ukosefu wa muingiliano wa mifumo ya kidijitali, hatari za usalama wa mtandao na pengo la kidijitali.