Gigy Money ahojiwa Basata

Friday April 02 2021
gigymoneypic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Msanii wa Bongofleva, Gift Stanford maarufu  Gigy Money amehojiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) baada ya kwenda nchini Kenya kufanya shughuli za sanaa wakati baraza hilo limemfungia kujihusisha na sanaa ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miezi sita.

Januari 5, 2021 Basata walimfungia msanii huyo kwa maelezo kuwa akiwa katika tamasha la Wasafi ‘Tumewasha Tour’ lililofanyika jijini Dodoma katika uwanja wa Jamhuri, alipanda jukwaani kwa ajili ya kutumbuiza na kuvua gauni (dela) na kubakia na vazi ambalo lilikuwa linaonyesha maungo yake ya mwili.

Akizungumza leo Ijumaa Aprili 2, 2021 kaimu katibu mtendaji wa baraza hilo, Matiko Mniko amesema, “ni kweli baada ya Gigy kurudi nchini tulimuita na kumuhoji, ukizingatia kuwa hakuwa na ruhusa ya kufanya kazi ya sanaa kwa adhabu aliyopewa Januari mwaka huu lakini nini tumeamua kitajulikana hapo baadaye.”

Machi 10, 2021 Gigy alikuwa mmoja wa wasanii walioshiriki kipindi cha msanii wa vichekesho nchini Kenya, Erick Mondi na kwa mujibu wa Mniko baada ya kumuona msanii huyo kwenye kipindi hicho walisubiri arudi ili wamhoji.

Advertisement