Halmashauri yasitisha usafirishaji mpunga nje

Katavi. Baraza la madiwani wa halimashauri ya Mpimbwe limesitisha usafirishaji mpunga kwa wafanyabiashara wa nje badala yake wasafirishe mchele ili kuviwezesha viwanda vya uchakataji vya ndani kupata mali ghafi ya kutosha.
Mwenyekiti wa halmashauri hilo, Silasi Ilumba kwaniaba ya madiwani amebainisha hayo kwenye kikao cha robo ya nne cha kujadili utekelezaji wa miradi na mengineyo leo Augosti 2, 2023.
Amesema wameridhia mapendekezo ya mabadiliko hayo yanayolenga kubadilisha pia bei ya ushuru wa kusafirisha gunia la mpunga nje ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.
"Mpunga ulikuwa unanunuliwa kwa wingi na wafanyabiashara wa nje, wawekezaji wa ndani wenye viwanda vya kuchakata wanalalamikia kukosa malighafi na ajira," amesema.
"Kwa utaratibu huu utasaidia hata vijana wetu kupata ajira viwandani na mapato yetu yataongezeka wote kwa pamoja tumeridhia,"
Awali akiwasilisha taarifa hiyo kwa niaba ya Mkurungezi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Andrew Gregory ambaye ni Mwanasheria amesema kupitia kikao cha kamati ya fedha, uongozi na mipango walikubaliana suala hilo.
"Timu ya menejimenti kupitia kikao kimependekeza ushuru kwa gunia moja la mchele utakaosafirishwa nje ya halmashauri lilipiwe Sh3,500," amesema.
"Awali gunia moja la mpunga lilipiwa Sh1,500 Kama ilivyo kwenye sheria ndogo ya ada na ushuru za halmashauri ya Mpimbwe ya 2019 kupitia tangazo la serikali namba 342," amesema.
Nao baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kuchakata mpunga, Pius John mkazi wa Usevya amesema utaratibu huo utakuwa na tija kwao.
"Mwandishi unaona ghala lipo wazi siyo kwamba mpunga hakuna upo, isipokuwa unanunuliwa na wafanyabiashara wa nje wanaenda kukoboa kwingine,"
"Ilituathiri kwa sababu tumewekeza viwanda kwa mitaji mikubwa, lakini tunakosa malighafi japo kwa sasa tutafanya kazi usiku na mchana na vijana watapata ajira," amesema.
Mfanyabiashara wa mchele Amina Ally mkazi wa Usevya amesema utaratibu huo una faraja kubwa kwao kwasababu watapata mpunga kwa urahisi zaidi na wataongeza faida.
"Tutanunua mpunga mwingi na kuwauzia wafanyabiashara wa nje ambapo awali tulikuwa tunauza kwa wateja ndani ya halmashauri pekee," amesema.
Wakati utaratibu huo ukiungwa mkono na wamiliki wa viwanda na wafanyabiashara wa ndani, wafanyabiashara kutoka nje ya halmashauri wanadai hiyo hali itawaathiri.
"Tutatumia muda mrefu Sana kufikisha sokoni, na viwanda vya kuchakata havitakidhi kiwango, umeme unakatika mara kwa mara mzunguko wa biashara utatumia muda mrefu sana," amesema Maico Ernest mfanyabiashara wa mpunga kutoka Mwanza.
Halmashauri ya Mpimbwe inazalisha asilimia 60 ya mpunga wa Mkoa wa Katavi ukidaiwa kuwa na ubora kuliko maeneo mengine.