Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatari kuruhusu mtu atumiwe fedha kupitia akaunti yako

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa sheria za Tanzania za kupambana na utakatishaji fedha, mtu anayepatikana na hatia ya kosa hilo anaweza kuhukumiwa kifungo jela pamoja na faini.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewaonya wananchi dhidi ya kuruhusu akaunti zao za benki au huduma nyingine za kifedha kutumika kupokea au kuhamisha fedha zisizojulikana chanzo chake.

Imeeleza jambo hilo linaweza kuwaweka katika hatari ya kujihusisha na utakatishaji fedha na kukabiliwa na hatua za kisheria.

Akizungumza jana Jumamosi, Julai 11, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), mchambuzi wa BoT, Huuere Naniya aliwataka wananchi kuwa makini na kuepuka miamala yenye viashiria vya utata, hususan pale wanapoombwa na watu wengine kutumia akaunti zao kuweka au kutoa fedha bila kufahamu chanzo chake.

“Wananchi wanapaswa pia kuwa waangalifu na kuepuka kuruhusu magari au mali nyingine kusajiliwa kwa majina yao wakati hawajui fedha zilizotumika kuzinunua zimetoka wapi,” amesema.

Ameonya kuwa hata kama mtu hakushiriki moja kwa moja katika uhalifu, kuhusika katika miamala yenye viashiria vya utata au isiyoeleweka kunaweza kumuweka katika hatari ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania za kupambana na utakatishaji fedha, mtu anayepatikana na hatia ya kosa hilo anaweza kuhukumiwa kifungo jela pamoja na faini.

Ili kukabiliana na suala hilo, Naniya amesema benki hiyo inaendelea kuelimisha umma kupitia majukwaa mbalimbali kuhusu hatari za utakatishaji fedha na namna wananchi wanavyoweza kujilinda dhidi ya kuingizwa katika shughuli haramu za kifedha bila kujua.

“BoT inaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa kuhusu hatari zinazohusiana na utakatishaji fedha na kuwasaidia wananchi kujikinga dhidi ya vitendo vinavyoweza kuwaingiza katika makosa ya kifedha,” amesema.

Amesema Tanzania imepiga hatua katika kuimarisha mfumo wa kupambana na utakatishaji fedha huku wadhibiti wa sekta ya fedha na taasisi nyingine zikiendelea kushirikiana kuhakikisha sheria na kanuni zinazodhibiti sekta hiyo zinafuatwa.

Kwa mujibu wa Naniya, kampeni za uhamasishaji zinaendelea kufanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu utakatishaji fedha na makosa mengine ya kifedha.

“Wadhibiti wa sekta ya fedha hukusanya taarifa, kufanya ukaguzi na kutoa maelekezo kwa taasisi zilizo chini ya usimamizi wao ili kuhakikisha zinazingatia matakwa ya sheria za kupambana na utakatishaji fedha,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa waliotembelea banda la BoT katika maonyesho ya Sabasaba, Amina Lwania amesema elimu hiyo imekuja kwa wakati kwani watu wengi, hasa vijana hupewa fedha ili kutumia akaunti zao bila kujua madhara yake.

“Wapo watu wanaodhani ni njia rahisi ya kupata fedha za haraka, lakini hawafahamu kwamba wanaweza kujikuta wanahusishwa na uhalifu wa kifedha. Elimu kama hii inapaswa kutolewa mara kwa mara ili wananchi wajue hatari zilizopo,” amesema.