Hatifungani za halmashauri kuanza kuuzwa mwaka huu

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji (katikati) akiwa na mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), John Mduma (kulia) na kaimu ofisa mtendaji mkuu wa mamlaka hiyo, Nicodemus Mkama (kushoto) wakionyesha mkataba wa huduma baada ya kuuzindua jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Ericky Boniphace
Muktasari:
Kwa mpango huo unaoanza kutekelezwa mwaka huu wa fedha, halmashauri zenye vyanzo imara vya mapato zitakuwa na uwezo wa kukopa fedha wazitakazo na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dar es Salaam. Baada ya Serikali kulitumia vyema Soko la Hisa, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imetangaza kuanza kutoa hatifungani za halmashauri.
Kwa mpango huo unaoanza kutekelezwa mwaka huu wa fedha, halmashauri zenye vyanzo imara vya mapato zitakuwa na uwezo wa kukopa fedha wazitakazo na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mkakati huo umebainishwa na mwenyekiti wa CMSA, Dk John Mduma alipokuwa akiwatunuku vyeti wahitimu 60 wa kozi ya utendaji katika masoko ya mitaji.
“Moja kati ya mikakati ya mamlaka kwa mwaka wa fedha 2018/19 ni kusaidia uanzishwaji na utoaji wa hatifungani za serikali za mitaa. Mpango huu unatarajiwa kuimarisha masoko ya mitaji kwa kuzileta pamoja sekta zote muhimu hivyo kuchochea maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisema.
Kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo, mhadhiri mwandamizi wa uchumi wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory alisema si halmashauri pekee zitajazoweza kukopa bali hata taasisi nyingine za umma.
“Kitu kizuri ni kwa wawekezaji kupata fixed rate (riba isiyobadilika kwa muda wote wa uwekezaji). Kinachozingatiwa ni uwezo wa taasisi husika kulipa kiasi husika kwa wakati,” alisema.
Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, naibu waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji aliwataka CMSA kuhakikisha uwapo wao unaonekana kwa kushawishi wawekezaji wengi zaidi kujiunga soko la hisa ili kuongeza ukwasi kufanikisha utekelezaji wa miradi ya muda mrefu.