JICA yawekeza kuinua uchumi wa vijana, wanawake
Ofisa Maendeleo ya Jamii katika Kata ya Kihesa, mkoani Iringa, Masahiko Konishi (kushoto), akionyesha moja ya bidhaa zilizobuniwa kupitia mpango wa ubunifu wa jamii wakati wa Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Saba Saba).
Muktasari:
- Fursa hiyo ni sehemu ya mafanikio yanayoadhimishwa katika miaka 60 ya ushirikiano kati ya Tanzania na Japani kupitia Jica
Dar es Salaam. Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (Jica) limesema mafunzo ya vitendo yanayotolewa na vijana wake wa kujitolea yamewasaidia Watanzania wengi, hususan wanawake na vijana, kujiajiri na kuongeza kipato kupitia shughuli za ujasiriamali.
Mafunzo hayo yanahusisha utengenezaji wa sabuni, urejelezaji wa taka za plastiki na ushonaji wa bidhaa mbalimbali, huku yakifungua fursa mpya za biashara kwa jamii.
Fursa hizo ni sehemu ya mafanikio yanayoadhimishwa katika miaka 60 ya ushirikiano kati ya Tanzania na Japani kupitia Jica.
Katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), vijana wa kujitolea kutoka Japan na Tanzania wanaendelea kuwapatia Watanzania mafunzo ya vitendo yanayolenga kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuanzisha biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwenye maonyesho hayo jana Jumanne, Julai 7,2026, Ofisa wa Maendeleo ya Jamii wa Jica, Masahiko Konishi amesema baadhi ya bidhaa zinazooneshwa na kufundishwa katika maonyesho hayo ni sabuni zinazotengenezwa kwa mikono, mapambo ya nywele yaliyofumwa kwa uzi na hereni zinazotokana na urejelezaji wa vifuniko vya chupa za plastiki.
Konishi amesema amekuwa akishirikiana na wanafunzi kutengeneza sabuni, huku mapato yanayotokana na mauzo yakitumika kuboresha mazingira ya shule zao.
"Tunatengeneza sabuni pamoja na wanafunzi na fedha zinazopatikana kutokana na mauzo hutumika kuboresha maeneo yao ya ujifunzaji," amesema.
Mbali na mradi huo, Konishi amesema Jica pia inawafundisha vijana ujasiriamali katika Shule ya Sekondari Mkwawa mkoani Iringa, kwa kuwajengea uwezo wa kusimamia biashara ndogo, kufanya masoko, kupanga gharama na kutunza hesabu za msingi.
Amesema ushiriki wa wanafunzi katika uzalishaji unawapa uzoefu wa moja kwa moja wa biashara huku ukiwawezesha kuchangia maendeleo ya shule zao.
Mkufunzi katika Kata ya Kalenga mkoani Iringa, Yona Itohara amesema kazi kubwa anayoifanya kupitia Jica ni kuwapa wanawake mafunzo ya kutengeneza mapambo ya nywele kwa kutumia uzi na sindano.
Itohara amesema amebaini wanawake wengi tayari walikuwa na ujuzi wa kufuma na kushona walioupata tangu wakiwa shuleni, lakini hawakuwahi kuutumia kama fursa ya kujiingizia kipato.
"Ninaamini wanawake wengi hawatambui thamani ya ujuzi wao. Wanaweza kuutumia kuboresha maisha yao na familia zao. Ni muhimu wanawake kutambua thamani ya vipaji walivyonavyo na kuvitumia kama njia ya kujikwamua kiuchumi," amesema.
Ofisa wa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Aisha Lugendo amesema miradi ya ujasiriamali umewawezesha wanawake kutumia malighafi zinazopatikana kwa urahisi, ikiwamo uzi, sindano na plastiki zilizorejelewa, kutengeneza bidhaa zenye thamani ya kibiashara.
"Bidhaa hizi zimepokewa vizuri sokoni na wanawake wengi wanazipenda, lakini changamoto yetu kubwa bado ni kupata masoko endelevu," amesema.
Lugendo amesema bidhaa hizo kwa sasa zinaoneshwa na kuuzwa katika Sabasaba kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya huduma za kujitolea za Jica nchini.
Kwa miaka 60, Jica imeendelea kupanua shughuli zake za maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania.