Juhudi za Rais Samia kuondoa mafuriko bonde la Mto Msimbazi zazaa matunda

What you need to know:

  • Baada ya miaka mingi ya usumbufu uliosababisha maafa na hasara kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, mkakati wa kuliboresha Bonde la Mto Msimbazi kuwa eneo la uwekezaji umekamilika na kuanzia Aprili mwakani utekelezaji huo unatarajiwa.

Baada ya miaka mingi ya usumbufu uliosababisha maafa na hasara kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, mkakati wa kuliboresha Bonde la Mto Msimbazi kuwa eneo la uwekezaji umekamilika na kuanzia Aprili mwakani utekelezaji huo unatarajiwa.

Utekelezaji wa maboresho hayo unatokana na kuhitimishwa mchakato uliodumu kwa miaka sita sasa kwa watendaji wa Serikali kujadiliana na Benki ya Dunia ili upata fedha za kufanikisha lengo hilo.

Baada ya bodi ya wadhamini wa Benki ya Dunia kuidhinisha mkopo nafuu kiasi cha dola 260 milioni za Marekani (Sh463.98 bilioni) mapema Septemba, wiki iliyopita Serikali ilitiliana saini na Benki ya Dunia kuidhinisha mkopo wa dola 535 milioni, sawa na Sh1.2 trilioni unaojumuisha dola 335 milioni (Sh777.17 bilioni) kwa ajili ya kuendeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).

Maboresho ya bonde hilo yanakusudia kutoa suluhisho la kudumu kwa mafuriko yanayotokea kila mara mvua zinaponyesha jijini Dar es Salaam na maji kujaa eneo la Jangwani kiasi cha kusimamisha shughuli kwa muda.

Adha hizo ambazo ziliwaumiza zaidi wanafunzi, wafanyabiashara na kuwachelewesha wafanyakazi wenye ofisi katikati ya mji, ziliwalazimu watendaji wa Serikali kuwashirikisha wadau kupata dawa ya kudumu.

Ingawa juhudi za kuujenga mradi huo zilianza mwaka 2017 zikisimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo kipindi hicho ilikuwa chini ya Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais kwa sasa, kikao cha kwanza cha wadau kujadili namna ya kuyadhibiti mafuriko yanayokuwa yanatokea mara kwa mara kiliitishwa Januari 2018.

Kutoka kwenye kikao hicho, ilihitimishwa kuwa kinahitajika kikosi kazi cha kuratibu jitihada zinazopangwa na Serikali kutoa mwongozo wa kujikinga na mafuriko na namna ya kutunza mazingira.

Mchakato huu uliojulikana kama Msimbazi Basin charattee ulianza kutekelezwa ukiratibiwa Ofisi ya Rais chini ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Mwaka 2019, Benki ya Dunia ilitoa ripoti ya mradi huo inayojulikana kama Msimbazi Opportunity Plan iliyotoa mrejesho Ofisi ya Makamu wa Rais kuhusu mapendekezo yaliyowasilishwa mwaka 2017 katika juhudi za kutafuta suluhisho la mafuriko ya mara kwa mara yanayotokeza jijini Dar es Salaam, hasa Bonde la Mto Msimbazi.

Ripoti hiyo ilisema mradi ulianza kufanyiwa kazi kwa kuwashirikisha wadau muhimu kuanzia Januari mpaka Agosti 2018, hivyo ulitengenezwa na wadau wanaoguswa na adha na athari zake. Timu ya zaidi ya watu 200 kutoka taasisi 59 pamoja na raia wa kawaida ilihusika katika uratibu wa mradi huo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Rogatus Mativila anasema kinachofanyika kwa sasa ni kutangaza zabuni kumtafuta mkandarasi atakayelijenga bonde hilo ili kuanza kuwanufaisha wananchi.

“Kwa kawaida zabuni hufanyika ndani ya miezi mitatu, kwa hiyo tunatarajia ujenzi uanze Aprili mwakani na ufanyike ndani ya miaka miwili hadi mitatu,” amesema Mativila.

Katika maboresho hayo, Tanroads imesema itajenga daraja lenye urefu wa mita 390 na kimo cha mita saba. 

Kinachotarajiwa kufanywaIngawa Mto Msimbazi ulikuwa unatiririka mwaka mzima, mabadiliko ya tabianchi na shughuli za binadamu zimeufanya uwe wa msimu kwa sasa, huku ukiacha hatari kipindi cha masika unajaa na kufurika.

Mradi unaotarajiwa kutekelezwa utafanya vitu vinne vya msingi ambavyo ni kutatua changamoto iliyopo kwa kupunguza mafuriko yanayotokea, kuwalinda watu wanaoathirika na mafuriko hayo pamoja na mali zao, kisha kulibadili bonde hilo kuwa City Park, yaani bustani ya jiji itakayosheheni maduka makubwa, sehemu za kupumzika, kumbi za starehe, hoteli na vikorombwezo vingine katika eneo la mto huo na maeneo jirani ambako tayari wananchi wamehamishwa kuupisha mradi.

Jambo la nne litakalofanyika ni usimamizi wa shughuli zote zilizopangwa kuanzia kipindi cha ujenzi mpaka kukamilika kwa mradi zinazohusisha maendeleo ya mji na kulilinda bonde hilo ili kudhibiti ujenzi wa makazi holela yaliyokuwa yanafanywa, hivyo kuchangia mafuriko kutokana na kuzibwa kwa njia za maji.

Mradi huo utakaotekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 57, unatarajiwa kuwa na nyumba 14,500 za ukubwa na matumizi tofauti kulingana na eneo husika.

Nyumba zitakazojengwa zitakuwa kwa ajili ya ofisi za Serikali na sekta binafsi pamoja na biashara za aina tofauti, hivyo kubadili mwonekano wa eneo hilo kutoka hasara na kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Makadirio ya Benki ya Dunia yanaonyesha nyumba zitakazojengwa zitaingiza wastani wa dola 900 milioni (Sh2.07 trilioni kwa mwaka).

“Kwa makisio ya mapato yatakayotokana na shughuli zote zitakazofanyika eneo la mradi, gharama za uwekezaji zitarudi ndani ya miaka 12,” imesema Benki ya Dunia.

Utekelezaji wa mradi unatarajiwa kuhusisha kuongeza kina cha mto na kutanua upana wake. Vilevile, zitajengwa ngazi zitakazosaidia kupunguza kasi ya maji yanayosababisha mafuriko pamoja na mmomonyoko wa udongo.

Ngazi hizo zitajengwa kwa malengo mawili, kwanza ni kutoa nafasi kwa mto kutiririka bila kusumbuliwa na kulitumia eneo la mafuriko kwa uwekezaji. 

Wananchi wafurahiaKupokelewa kwa mkopo huo utakaobadilisha mandhari ya Bonde la Mto Msimbazi kumewafurahisha wananchi wa Jiji la Dar es Salaam walioeleza kero zitakazoondolewa pindi utakapokamilika.

Yasin Abdul, mfanyabiashara wa Kariakoo anasema ilikuwa kero kubwa kipindi cha masika, kwani halikuwa jambo la kushangaza kusikia Barabara ya Morogoro imefungwa hivyo wananchi kutakiwa kutafuta njia mbadala ya kufika makwao kutoka mjini.

“Matokeo yake foleni ilikuwa ndefu kwenye barabara zote zinazoingia mjini wa sababu magari yalilazimika kuzitumia njia zinazobaki. Ujenzi unaosubiriwa utaongeza fursa kwa wafanyabiashara wengine kuhamia huku,” anasema Abdul.

Mkazi wa Kinondoni, Yasinta Edward anasema mradi huo utalipendezesha jiji, kwani makazi holela yaliyokuwapo yataondoka na nyumba nzuri na za kisasa zitajengwa.

“Kila mwaka, watu walikuwa wanalia kutokana na mafuriko yaliyokuwa yanajaa ndani ya nyumba zao. Wengi walikuwa wanahamia msikitini kwa muda na kuilazimu Serikali na jamii kwa ujumla kuwapa msaada wa vyakula hata mavazi. Haya yote yatabaki historia,” anasema Yasinta.

Pamoja na usumbufu waliokuwa wanaupata wakazi wa bonde hilo, wengi hawakuwa tayari kuhama hata walipopewa viwanja eneo la Mabwepande na Serikali.