Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge wazuia ujenzi hoteli Ngorongoro

Wabunge walipotembelea Ngorongoro

Muktasari:

Serikali imetakiwa kumtafutia eneo lingine mwekezaji huyo anayedaiwa kubebwa na vigogo serikalini.

Ngorongoro. Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, imetangaza kupiga marufuku mpango wa ujenzi wa hoteli ya kutalii eneo la Layanai jirani na Kreta ya Ngorongoro, ili kulinda mazingira ya eneo hilo ambalo ni mapito ya Faru.

Mwenyekiti wa Kamati wa Bunge, Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, alitangaza uamuzi huo jana baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wataalamu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na wananchi wanaoishi ndani ya mamlaka hiyo, kuhusiana na shinikizo kubwa kutoka serikalini la ujenzi wa hoteli hiyo.

“Kuanzia sasa kamati ya Bunge inatangaza rasmi hakuna hoteli ambayo itajengwa eneo hilo la Kreta, kwani kuna maeneo mengi ambayo yanaweza kujengwa hoteli hapa, hawa wanaotaka hilo eneo wapelekwe pengine,” alisema Lembeli.

Hoteli hiyo, inashinikizwa kujengwa eneo hilo na mfanyabiashara mmoja maarufu wa Arusha ambaye anamiliki hoteli ya kitalii (jina linahifadhiwa), anayeungwa mkono na vigogo kadhaa wa Serikali.

Kamati hiyo licha ya kupiga marufuku ujenzi wa hoteli hiyo, imeitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, kusitisha mara moja mpango wake wa kutaka magari ya watalii kuruhusiwa kuingia ndani ya hifadhi, kutoka na baadaye kurejea (double entre) kwa kulia mara moja.

“Huu ni mpango wa kifisadi unalenga kunufaisha kampuni za utalii na utapunguza mapato zaidi ya nusu ya NCAA na hifadhi nyingine za taifa nchini,” alisema Lembeli.

Lembeli alisema kamati hiyo, itakutana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kumweleza juu ya uamuzi wao kwani wanaamini kuna watu wanatoaka kuipotosha Serikali kwa manufaa yao.

Hata hivyo, wajumbe wa kamati hiyo, walielezea kuridhishwa na hatua ya NCAA kukamilisha miradi ya ujenzi wa madarasa na Mabweni Sekondari ya Nainokanoka kama walivyoagiza.

“Pia, tumeridhishwa kuanza vizuri mradi wa kuboresha mifugo ya wafugaji wa Tarafa ya Ngorongoro, ila tunachoagiza ni kuimarishwa uhusiano baina ya wakazi wa tarafa hii na watendaji wa NCAA,” alisema Lembeli.

Alisema hatua hiyo itaongeza ushirikiano ambao umeanza kujengwa kati ya mamlaka na wananchi na kwamba, itasaidia kulinda wanyamapori na mazingira ya eneo hilo.

Wabunge hao walikagua baadhi ya miradi inayoendeshwa na mamlaka kwenye kata hiyo, lengo likiwa ni kuangalia maagizo waliyotoa kwa NCAA kama yametekelezwa.