Kizungumkuti cha mbolea nchini

Muktasari:
Upatikanaji wa mbolea ya ruzuku nchini unaelezwa kuwa wa kusuasua huku baadhi ya maeneo yakiwa na msururu mrefu wa wakulima wanaoifuata mjini.
Dar/Mikoa. Upatikanaji wa mbolea ya ruzuku nchini unaelezwa kuwa wa kusuasua huku baadhi ya maeneo yakiwa na msururu mrefu wa wakulima wanaoifuata mjini.
Serikali ilitangaza utaratibu wa kutoa mbolea ya ruzuku katika bajeti ya mwaka 2022/23 ili kuwapa unafuu wakulima baada ya pembejeo hiyo kupanda bei kuanzia soko la dunia kutokana na kinachoelezwa kuwa athari za vita kati ya Russia na Ukraine.
Kufanikisha upatikanaji wa mbolea hiyo, kuanzia wakulima, mawakala hata waagizaji wanasajiliwa kumwezesha mkulima kupewa kiasi anachostahili kulingana na mahitaji yake.
Kilio cha wakulima sasa ni kutumia muda mwingi kufuatilia mbolea hiyo huku baadhi wakilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda wilayani kuifuata. Wengine hawapati kiasi cha kutosha kwa madai kwamba vitambulisho vyao tayari vimetumika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk Stephan Ngailo anasema mfumo unaotumika ni mpya hivyo una changamoto zinazoshughulikiwa.
Alisema changamoto kubwa ni wasiwasim wa wananchi kwamba mbolea itakwisha hivyo kulazimika kuipata kwa bei ya zamani jambo alilosema ipo ya kutosha na kila mkulima ataipata kwa wakati.
“Utaratibu tulioanzisha una changamoto tunazoendelea kuzitatua kadri zinavyojitokeza. Zilionekana Tarime, Muleba na maeneo mengine lakini tumeshazitatua,” alisema Dk Ngailo.
Mkurugenzi huyo amewahakikishia wakulima kwamba kutakuwa na mbolea wakati wote na wanaendelea kutatua changamoto zilizojitokeza ikiwamo kupeleka mbolea vijijini ili wakulima waipate katika maeneo yao.
“Tunazidi kupambana kwenye maeneo ambayo hayana mawakala, kinachotakiwa ni kutupa taarifa kupitia madiwani au halmashauri za wilaya kisha wazilete kwetu,” alisema mkurugenzi huyo.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema wanazifahamu changamoto zilizojitokeza zikichangiwa na uhitaji mkubwa uliojitokeza.
“Mpaka sasa mawakala waliosajiliwa ni 1,325 na kuanzia Agosti 15 mpaka Oktoba 15 mbolea iliyouzwa ni tani 36,368 sawa na ongezeko la asilimia 35 ya matumizi kwa kipindi kama hicho mwaka jana,” alisema Waziri Bashe.
Alisema Serikali inaongeza mawakala wengine 525 kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa ikiwamo mikoa ya Morogoro, Kigoma, Ruvuma, Kagera, Geita na Mara na itaitumia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchamganyiko na halmashauri kuuza mbolea maeneo ambako sekta binafsi haipo.
“Kumeibuka uhitaji hata kwa wakulima ambao kiutamaduni walikuwa hawatumii mbolea ya viwandani mfano maeneo ya kanda ya ziwa. Changamoto kubwa ni kwamba mawakala wengine wanashindwa kuuza kwa kuwa mfumo tuliouweka umewaondoa makanjanja wengi waliotaraji tutatumia mfumo vocha kama zamani ambao ulipelekea mbolea hewa,” alisema na kuongeza:
“Changamoto zipo nyingi kutokana na mtandao wa usambazaji ulioleta uhitaji mkubwa baada ya ruzuku kutangazwa. Mwezi ujao tutafungua vituo vipya maeneo yenye upungufu wa mawakala.”
Hali ilivyo mikoani
Baadhi ya wakulima wameeleza kero wanazopitia kuipata mbolea hiyo. Baadhi ya wakulima mkoani Ruvuma wameulalamikia mfumo wa kuipata mbolea hiyo wakisema una ucheleweshaji na wanajiweka hatarini kwa kutembea na fedha za kuinunua.
Wameliambia Mwananchi kwamba mfumo wa ugawaji unasababisha msongamano wa wakulima waliojiandikisha hivyo kupendekeza wasogezewe huduma za benki kwenye maghala ili kuepusha uwezekano wa kuibiwa fedha zao kabla ya kulipia.
“Mfumo huu unatugharimu kwa sababu tumetoka Zomba kwa nauli hadi hapa lakini hatupati mbolea kwa wakati,” alisema Edwin Gama, mkulima kutoka Kijiji cha Muungano Zomba aliyefuata mbolea aina ya Urea, SA, CAN.
Gama alisema unakuta mkulima anahitaji mbolea hizo tatu ila anapewa mbili na akiifuata iliyobaki anaambiwa kitambulisho chake kimeshatumika.
Bonface Haule alisema usalama wao uko shakani kutokana na mfumo wa malipo kuhitaji fedha taslimu huku wakichukua muda mrefu kusubiri mbolea.
“Mtu unatembea umebeba hela kwenye begi kwa siku nne hadi tano kusotea mbolea, huwezi kujua nani ni mwema au mbaya. Huu mfumo ungekuwa mzuri iwapo kila mkulima angechukua mbolea eneo aliloandikishwa kwani tunateseka kusafiri umbali mrefu, tunatumia gharama kubwa kulala na kukodi magari tunaomba Serikali itusaidie,” alisema.
Akizungumzia kero zilizopo, Mkurugenzi wa kampuni ya Export Trading Group, Vishnu Vishnu alisema wanaendelea kutoa huduma kwa kufuata miongozo na ikitokea mfumo unasumbua wanatoa taarifa kwa mamlaka husika.
Mkoani Songwe nako upatikanaji wa mbolea hiyo ya ruzuku unasuasua tofauti na ilivyotarajiwa utaratibu ulipoanza Agosti 15.
Baadhi ya wakulima wamesema utaratibu wa kumfikia mkulima si mzuri hali inayowalazimu wakae muda mrefu kusubiri hivyo kuingia gharama za ziada za chakula na nauli ya kwenda na kurudi.
Asajile Kamendu, mkulima wa Kijiji cha Sumbaluwela wilayani Mbozi alisema ni kilio cha muda mrefu kutaka ruzuku kwenye pembejeo lakini upatikanaji wake umekuwa mgumu na wenye kero kutokana na mawakala wanaoisambaza kupatikana mijini tu.
“Kikwazo kingine ni kufuatilia mara kadhaa kwa mawakala lakini tunaikosa ambapo tumekuwa tukiambiwa haipo au hakuna stika za kubandika (QR-Code) na hata vitu hivyo vikiwepo unakuta mbolea iliyopo ni chache isiyotosheleza idadi ya watu waliopo kwenye foleni,” alisema Kamendu.
Mmoja wa wauzaji wa pembejeo mjini Vwawa wilayani humo, Sailas Mpembela alisema mpango wa ruzuku ni mzuri lakini kuna urasimu unaochelewesha mzunguko wa biashara.
“Kwa mfanyabiashara tunaona bora upate faida ya Sh200 kwa mzunguko wa haraka kuliko hali ilivyo ambapo ukipata mbolea leo utasubiri tena muda fulani kukamilisha utaratibu ndio upate mzigo mwingine hali inayotukwamisha. Nashauri hali hii irekebishwe ili huduma iwe ya kasi,” alisema.
Imeandikwa na Peter Elias (Dar), Joyce Joliga (Ruvuma), Mwanja Ibadi (Lindi), Mussa Mwangoka (Rukwa) na Stephano Simbeye (Songwe).