Madini ya Sh34 bilioni yauzwa Arusha tangu Desemba 2019

Muktasari:

Madini ya Sh34.5 bilioni yameuzwa katika soko la madini mjini Arusha kuanzia Januari hadi Desemba 2019

Arusha. Madini ya Sh34.5 bilioni yameuzwa katika soko la madini mjini Arusha kuanzia Januari hadi Desemba 2019.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Januari 15, 2020 na naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, kubainisha kuwa kati ya fedha hizo, Serikali imepata mrabaha wa Sh1.2 bilioni na Sh350 milioni za ada ya ukaguzi.

Nyongo alieleza hayo wakati akifungua mkutano uliomhusisha balozi wa China nchini Tanzania, balozi wa  Tanzania nchini China, wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kujadili fursa za kupata masoko ya madini  China.

Nyongo amesema katika soko la dhahabu  wilayani Karatu, madini ya Sh198 .5 milioni yameuzwa.

Amesema kati ya fedha hizo, Serikali umepata mrabaha wa Sh11.9 milioni na Sh1.6 milioni za ada ya ukaguzi.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Arusha, amesema mkutano huo umeandaliwa ili kutafuta masoko mapya ya madini.

Amesema Tanzania kuna madini mengi lakini  mchango wa madini katika pato la Taifa ni mdogo ambao ni asilimia 5.7 huku utalii ukichangia asilimia 17.5.

Mwenyekiti wa chama cha wauzaji madini (Tamida),  Sammy Mollel ameomba kuondolewa vikwazo kwa wauzaji wa madini, na kutaja kodi na kukamatwa bila sababu za msingi.

Balozi wa Tanzania nchini China,  Mpelwa Kairuki  amewataka wauzaji wa madini kushiriki maonyesho ya Shanghai nchini China Novemba 5 hadi 15, 2020 kwa maelezo kuwa nchini humo kuna soko kubwa la madini.