Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madini ya Sh4.9 bilioni yakamatwa yakitoroshwa

Muktasari:

  • Katika kipindi cha Juni hadi Julai 2026 pekee, madini yenye thamani ya takribani Sh1.6 bilioni yamekamatwa mkoani Kagera kupitia operesheni zilizofanywa na vyombo vya dola.

Bukoba. Serikali imesema madini yenye thamani ya zaidi ya Sh4.9 bilioni yamekamatwa katika operesheni mbalimbali za kudhibiti utoroshaji wa madini, huku Mkoa wa Kagera ukitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyorekodi mafanikio makubwa katika operesheni za hivi karibuni.

Akizungumza leo Julai 13, 2026 mkoani Kagera, Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa amesema kuwa kati ya Julai 2025 na Machi 2026 madini yenye thamani ya Sh3.3 bilioni yalikamatwa yakitoroshwa katika matukio 55 yaliyotokea katika maeneo mbalimbali nchini.

Dk Kiruswa ametoa taarifa hiyo katika ziara yake mkoani Kagera inayolenga kutoa tamko la Serikali kuhusu matukio ya utoroshaji wa madini ya dhahabu na vito yaliyobainika hivi karibuni mkoani humo.

Dk Kiruswa amesema katika kipindi cha Juni hadi Julai 2026 pekee, madini yenye thamani ya takribani Sh1.6 bilioni yamekamatwa mkoani Kagera kupitia operesheni zilizofanywa na vyombo vya dola.

Akifafanua kuhusu operesheni hizo, Dk Kiruswa amesema Juni 29, 2026 ilifanyika operesheni katika eneo la Benako, Wilaya ya Ngara, ambako askari walikamata viroba 20 vya madini ya vito vyenye uzito wa kilo 627.2, vilivyokuwa na thamani ya Sh10.9 milioni. Amesema madini hayo yalipaswa kulipiwa kodi ya Serikali ya Sh1 milioni.

Amesema watu wanne wamekamatwa katika tukio hilo, akiwamo Petro Kihiga, ambaye alikuwa na leseni ya udalali wa madini iliyotolewa Mei 25, 2026 mkoani Lindi.

"Mtuhumiwa huyo alikuwa amepewa kibali cha kusafirisha madini yenye uzito wa gramu 273, lakini kiwango halisi kilichokamatwa kilikuwa kilo 627.2. Kwa mujibu wa Kanuni za Madini (Ufililishaji wa Makosa) za mwaka 2022, alikiri kosa na kulipa faini," amesema Dk Kiruswa.

Ameongeza kuwa Julai 1, 2026 askari walimkamata mtuhumiwa mwingine aliyekuwa akisafiri ndani ya gari la International Transit (IT) akiwa na dhahabu yenye uzito wa gramu 4,434.66 yenye thamani ya Sh1.3 bilioni. Amesema dhahabu hiyo ilipaswa kulipiwa kodi ya Serikali ya Sh125.8 milioni.

Kwa mujibu wa Dk Kiruswa, mtuhumiwa huyo amekamatwa katika eneo la Benako karibu na mpaka wa Tanzania na Rwanda.

Aidha, amesema Julai 4, 2026 mshirika wa mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na dhahabu yenye uzito wa gramu 453 yenye thamani ya Sh144.2 milioni, huku kodi iliyopaswa kulipwa ikiwa Sh12.6 milioni.

Amesema watuhumiwa wa kesi za dhahabu wamefikishwa mahakamani na mashauri yao yanaendelea katika hatua ya kutajwa, lakini hakutaja majina yao wala mahakama husika kutokana na sababu za kipelelezi.

Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Kagera, Christofa Laurian amesema kukamatwa kwa wanaotorosha madini ni ishara kuwa Serikali imeimarisha ulinzi wa rasilimali za Taifa.