Mahitaji makubwa ya maziwa fursa iliyo wazi nchini

Dodoma. Kila mwaka Tanzania hutumia Sh20 bilioni kwa ajili ya kuagiza lita za maziwa 20 milioni ili kukabiliana na upungufu wa maziwa nchini.

Uzalishaji wa maziwa kwa sasa ni lita 3.6 bilioni kwa mwaka, ambazo ni pungufu ya lita 9 bilioni zinazohitajika.

Upungufu huo umesababisha kwa mwaka 2022/2023 viwanda tisa vikubwa na vidogo vya kusindika maziwa kufungwa, huku vinavyoendelea kufanya kazi vikipata asilimia 30 tu ya mahitaji.

Vituo vya kukusanyia maziwa takriban 50 vimetajwa kutofanya kazi kutokana na upungufu huo.

Mwandishi wa Mwananchi, Mainda Mhando akifanya mahojiano na Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk George Msalya ofisini kwake jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Akizungumza na Mwananchi, katika mahojiano maalumu na Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini, Dk George Msalya anasema unywaji mdogo wa maziwa ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kuwapo kwa upungufu huo.

Anasema sababu za wananchi kutokufikia lengo la kunywa maziwa angalau lita 200 kwa mwaka linalopendekezwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) ni upungufu wa maziwa uliopo nchini.

“Maziwa yanayozalishwa kwa sasa ni robo ya mahitaji yetu, kwa hiyo bado uzingatiaji wa ulaji ni kidogo sana, kwa sasa kwenye ulaji tupo wastani wa lita 62 kwa mwaka kwa mtu mmoja.

Malengo yetu ndani ya kipindi cha 2025 tuwe tumefikia lita 64 kutoka lita 62 iliyopo sasa na angalau lita 100 ifikapo mwaka 2030,” anasema Dk Msalya.

Pia, Dk Msalya anasema hali hiyo inachangiwa na uzalishaji duni wa maziwa kwa sababu asilimia 97 ya ng’ombe wanaofugwa nchini hufugwa kwa njia za kienyeji, hivyo kutoa maziwa kidogo.

Hata hivyo, anasema hadi sasa nchi ina idadi ya ng’ombe milioni 1.5 wa kisasa wanaotegemewa kutoa maziwa kwa wingi, hivyo idadi hiyo ni ndogo kwa uhitaji wa kiwanda kimoja kupata lita 250 kwa siku.


Mkakati wa Serikali

Hivi sasa jitihada zinafanywa ili kufikia lengo la kila mtu kunywa maziwa kwa mwaka angalau lita 65 kufikia mwaka 2025 sanjari na kufufua viwanda vilivyokufa kwa sababu ya kukosa malighafi hiyo.

Dk Msalya anasema Wizara kwa kushirikiana na wadau wa mifugo nchini wanaendelea kutoa elimu kwa wafugaji kufuga kisasa ili kuleta mazao yenye tija, ikiwemo maziwa.

Anasema ili kuhakikisha upatikanaji, ukusanyaji na usindikaji wa maziwa nchini unaongezeka, Serikali ilitenga Sh4 bilioni mwaka 2022/23 na mwaka 2023/24 kwa ajili ya kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo vya kukusanyia maziwa.

“Kwa upande wa uhimilishaji, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha ng’ombe wanafugwa kisasa ili kufikia kuzalisha lita 5 bilioni kufikia mwaka 2030,” anasema.

Dk Msalya anasema jitihada hizo zinafanywa na Serikali ili kuokoa fedha nyingi zinazotumika kuagiza maziwa kutoka nje na badala yake fedha hizo zitumike kwenye uzalishaji mali.

Aidha, Dk Msalya anasema bodi kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo inaendelea kuungana na wadau wa ndani na nje ya nchi kuimarisha upatikanaji wa maziwa, hasa katika jamii za pembezoni mwa miji.

Kuhusu suala la unywaji maziwa shuleni, Dk Msalya anasema bodi hiyo inazunguka maeneo tofauti nchini kuadhimisha siku hiyo ili kuwajengea uwezo wa kuendeleza programu ya unywaji maziwa.

Anasema Waziri wa mifugo amepewa dhamana ya kuteua mtu mmoja katika kila Halmashauri kusimamia sehemu zenye uhitaji wa maziwa shuleni kwa uharaka ili kupatiwe ufumbuzi.

Dk Msalya anatoa wito kwa wazazi, hususan katika shule za umma kuungana kwa pamoja kufanikisha programu ya unywaji maziwa shuleni ili kuondoa udumavu, njaa na kuongeza ari ya kujifunza na ufaulu shuleni.


Unywaji maziwa shuleni bado

Kwa kutambua mchango wa lishe na wingi wa vitamini vinavyopatikana katika maziwa, Serikali ilianzisha siku ya unywaji maziwa shuleni mwaka 1996, lakini mwaka 2000 ndio utekelezaji ulianza rasmi.

“Ilipofika mwaka 2005 utekelezaji wake ulianza kwa kasi kwa sababu chombo rasmi cha kusimamia kilikuwa tayari kimeanzishwa na tangu hapo tunapiga hatua na lengo ni kufika nchi nzima,” anasema.

Hata hivyo, siku ya unywaji maziwa shuleni ambayo inatekelezwa kila Jumatano ya mwisho wa mwezi, Septemba au Septemba 27 imeonekana kutofanya vizuri hasa katika shule za umma.

Dk Msalya anasema shule binafsi zinaendelea kufanya vizuri kwenye utekelezaji kwa sababu hutumia njia ya kuchangia kwa wazazi kununua maziwa kwa kipindi fulani shuleni, ukilinganisha na shule za umma ambazo zinategemea wafadhili.

Kwa mujibu wa bodi hiyo, ni mikoa sita tu yenye halmashauri 10 ambazo zinatekeleza utaratibu wa unywaji maziwa katika shule 55.

“Kwa upande wa shuleni tumeona fursa za kuwaongezea watoto hawa kasi ya ukuaji na kuondoa udumavu kwa sababu mtoto anapokuwa amedumaa inasababisha ukuaji, uelewa wake ni hafifu,” anasema.