Mapato yatokanayo na madini yaongezeka kwa asilimia 113.34
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, akizungumza na menejimenti ya Tume ya Madini, wakaguzi wasaidizi wa madini pamoja na watendaji wa wizara na taasisi zinazosimamia sekta ya madini katika kikao kazi kilichofanyika mkoani Morogoro leo Juni 24. Picha na Hamida Shariff.
Muktasari:
- Asilimia 40 ya makusanyo hayo ya Sh. 1.36 yanatokana na mchango wa wachimbaji wadogo ambapo katibu mkuuwa wizara ya madini mhandisi Yahaya Samamba amesema Serikali inayo mikakati mbalimbali ambayo ipo tayari inafanya kazi katika kudhibiti utoroshaji wa madini lakini pia kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogo.
Morogoro. Serikali imekusanya Sh1.36 trilioni kutoka sekta ya madini hadi Juni 23, 2026, kiwango kinachozidi lengo la Sh1.2 trilioni kwa asilimia 113.34, mafanikio yanayotajwa kuchangiwa na ushirikiano kati ya Wizara ya Madini, Tume ya Madini na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amesema leo Juni 24, 2026 katika kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa Tume ya Madini, wakaguzi wa madini na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuwa asilimia 40 ya makusanyo hayo yametokana na wachimbaji wadogo.
“Mafanikio haya yametokana na ushirikiano mzuri wa wadau wa sekta ya madini. Leo tumekutana kufanya tathmini ya utekelezaji wa mwaka wa fedha 2025/26 na kujiandaa kufikia lengo jipya la kukusanya Sh1.4 trilioni katika mwaka wa fedha 2026/27,” alisema Samamba.
Amesema Serikali imepeleka pendekezo bungeni la kuruhusu asilimia 10 ya mapato yatokanayo na madini kubaki ndani ya wizara ili kusaidia shughuli za utafiti wa madini nchini.
Kwa mujibu wa Samamba, hadi sasa utafiti wa kina wa madini umefanyika katika asilimia 16 ya eneo la nchi, huku Serikali ikilenga kuongeza kiwango hicho kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuharakisha utafiti wa rasilimali za madini.
“Sisi tunaamini nchi ikifanyiwa utafiti kwa kiwango kikubwa zaidi, mapato yatokanayo na madini yanaweza kuongezeka maradufu na kuwa chanzo kikubwa cha kuchangia bajeti ya Serikali,” alisema.
Katibu Mkuu huyo pia aliwataka watendaji wa sekta ya madini kuhakikisha fedha zinazotengwa na Serikali zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuendelea kujenga imani ya Serikali kwa taasisi za sekta hiyo.
Kuhusu udhibiti wa utoroshaji wa madini, Samamba amesema Serikali imeweka mifumo ya kisera, kisheria na kiutendaji inayowezesha kufuatilia mnyororo mzima wa biashara ya madini kuanzia uchimbaji hadi mauzo.
Amesema pamoja na kuwepo kwa kikosi kazi maalumu cha kudhibiti utoroshaji wa madini, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogo kwa kuwajengea mifumo rasmi ya masoko inayowawezesha kuuza madini yao kwa uwazi na kwa kufuata sheria.
“Kwa sasa wachimbaji wadogo wanajua maeneo rasmi ya kuuza madini yao na hali hiyo imeongeza uwazi pamoja na makusanyo ya Serikali,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Dk Janet Lekashingo, amesema taasisi hiyo itaendelea kusimamia sekta ya madini kwa weledi na uwajibikaji huku ikitekeleza maelekezo na miongozo ya Wizara ya Madini kwa lengo la kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa.
Amesema kikao hicho kimetoa fursa ya kutathmini mafanikio na changamoto za mwaka wa fedha 2025/26 na kuweka mikakati ya kuanza mwaka wa fedha 2026/27 kwa mwelekeo mpya wa kuongeza ufanisi wa sekta hiyo.
Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Dk Abdulrahman Mwanga, amesema ushirikiano kati ya Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) unaendelea kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya sekta ya madini nchini.
Amesema taasisi hizo zina jukumu la kusimamia udhibiti, uwekezaji na utafiti wa madini, mambo ambayo ni msingi wa ukuaji endelevu wa sekta hiyo na uchumi wa Taifa kwa ujumla.