Mashine kusaidia uuzaji vinywaji bila muuzaji

Muktasari:
- Mashine hiyo inawezesha watu kujihudumia, huku muuzaji akiwa na uwezo wa kufanya hadi biashara nne kupitia mashine moja pekee.
Dar es Salaam. Ili kuweka urahisi wa ufanyaji wa biashara pasipo uwepo wa watu, mbinu mpya na rahisi imebuniwa itakayofanya biashara kujiendesha kidigitali.
Mbinu hiyo inaweza kuwa ahueni kwa wauzaji wa vinywaji ikiwemo juisi, bia, maziwa au maji katika maeneo mbalimbali nchini.
Hiyo ni baada ya kutengenezwa kwa mashine mfumo wa ‘ATM’ ambayo mtu anaweza kujihudumia mwenyewe.
Mashine hiyo imebuniwa na Kilavo Hassan, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kuletwa katika maonyesho ya 49 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea jijini hapa.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 1, 2025, Hassan amesema sasa mtu atakuwa na uwezo wa kusimika mashine hizo katika maeneo mbalimbali anayotaka kufanyia kazi na kuacha watu wajihudumie.
“Mashine hii inampa mtu chaguo za aina tatu kwa ajili ya kulipia, ya kwanza ni sarafu, ya pili ni noti na ya tatu ni lipa namba. Lipa namba ni rahisi zaidi kwa sababu unakuwa na uwezo wa kuangalia utendaji wa biashara zako moja kwa moja kupitia eneo ulilopo,” amesema Hassan.
Akielezea mashine hiyo inavyofanya kazi, amesema ili mtu aweze kuhudumiwa anatakiwa kwenda na chombo cha kubebea kinywaji na maelekezo yote huwekwa.
“Tunaweka maelezo kuwa ukilipia kiasi kadhaa utapata ujazo kiasi gani kama ni kileo au kinywaji baridi, mtu anakuwa anajua anahitaji chombo kikubwa kiasi gani ili apate ujazo wa bei anayohitaji,” amesema.
Amesema uwepo wa mashine hiyo pia utawezesha uuzaji wa vinywaji kidogokidogo, hivyo kumfanya mtu kuwa na uwezo wa kumudu gharama zake.
“Kama ni maziwa ya Sh500, au juisi au kileo cha Sh500 mtu anaweza kujihudumia. Mashine hii huweza kuuza hadi bidhaa aina nne bila kuchanganyikana kwa sababu kila bidhaa itakuwa na koki yake maalumu ambayo ina maelekezo kuwa ukitaka maji utapata koki hii, maziwa koki hii, pombe koki hii,” amesema.
Amesema ndani yake, hufungwa matanki yenye ujazo kuendana na mahitaji ya mteja, lakini yapo ya kuanzia lita 18 na huweza kuongezwa kulingana na mahitaji ya mteja.
“Mtu akihitaji hii bei hubadilika kulingana na mahitaji yake, lakini huanzia Sh14 milioni,” amesema huku akisema hadi sasa wameshapokea oda za wateja mbalimbali.
Akizungumzia usalama wa uendeshaji wa biashara hiyo, Hassan amesema mtu anaweza kuijengea kibanda cha nondo kama ambavyo inafanywa na wafanyabiashara wenye majokofu yanayokaa nje.
Mfumo ouliwavutua watembeleaji ambapo baadhi walidai kuwa nafuu ukilinganisha na kufungua eneo la kuuza bidhaa hizo.
“Hii itapunguza sana kuibiwa na wafanyakazi wasiokuwa waaminifu, kelele na mivutano isiyokuwa na sababu na badala yake unakuwa na kijana mmoja mwaminifu au wewe mwenyewe ambaye utakuwa ukijaza biddhaa kila inapokwisha ili watu wasipate tabu,” amesema Yasin Salum mkazi wa Buza.