UDSM yaja na bajaji inayotumia maji na mafuta

Muktasari:
- Uwepo wa mfumo wa maji katika bajaji unatajwa kuwa moja ya njia inayoweza kupunguza gharama za uendeshaji, kwani injini inapopoa hutumia mafuta kidogo.
Dar es Salaam. Wakati biashara ya usafirishaji ikiendelea kukua nchini, watu wanaendelea kubuni njia rahisi zitakazowawezesha kufanya shughuli zao kwa urahisi na kuwapunguzia gharama za uendeshaji.
Hilo limeonekana kwa Andrew Mmbanga kutoka Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia (CoET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye amebuni bajaji inayotumia maji na mafuta.
Amesema kwa mara ya kwanza alitengeneza bajaji ya aina hiyo mwenyewe, lakini alipoambiwa aipeleke Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ifanyiwe marekebisho, ilibainika kuwa imekaa muda mrefu kabla ya kufanyiwa vipimo.
Amesema hayo alipozungumza na Mwananchi leo Julai 1, 2025, katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyoanza Juni 28 na yanatarajiwa kukamilika Julai 13 mwaka huu.
“Hivyo ilibidi tuanze upya kwa kushirikiana na wahandisi wa chuoni hapo, kitu kimoja baada ya kingine hadi tulipoikamilisha inavyoonekana leo,” amesema Mmbanga.
Akielezea inavyofanya kazi, Mmbanga amesema bajaji hiyo ina mfumo wa kuingiza maji kwa ajili ya kupoza cylinder zisipate moto, na maji huwekwa katika tanki maalumu.
“Maji hayo huja kwenye injini yakiwa ya moto, huingia katika rejeta na ile feni iliyopo katika rejeta inafanya maji yapoe na kuanza mzunguko mpya. Hilo linafanya injini ipoe muda mwingi, hali inayosababisha mafuta kidogo kutumika ukilinganisha na mfumo huo usipokuwepo,” amesema.
Amesema maji yanayotumika ni safi isipokuwa yasiyo na chumvi, na hufanya kazi kwa wiki moja, ambapo mtu anatakiwa kuyabadili endapo anafanya kazi kila siku.
“Ukiacha yachafuke sana, yataziba matundu ya rejeta, kwa sababu maji yanapozidi kuwa ya moto sana, yanatengeneza povu. Sasa povu likiendelea kukaa ndani ya rejeta, na ikiwa ni maji ya chumvi, ndiyo kabisa yanaziba matundu,” amesema.
Amesema bajaji za abiria za kawaida hazina mfumo wa maji, isipokuwa zile za mizigo, huku akisema lengo ni kufungua kiwanda cha kutengeneza bajaji.
“Tutakuwa tunatengeneza bajaji aina tatu--- ya kutumia gesi, bajaji za umeme jua, na bajaji za kutumia mafuta ya kawaida,” amesema Mmbanga.
Amesema wanatarajia kufanya biashara na watu wa ndani na nchi za jirani, na sasa anakiri yuko tayari kupokea oda za watu wanaotaka kutengenezewa bajaji hizo.
“Tukimaliza Sabasaba, tutakwenda Costech ili bajaji ithaminiwe, na baadaye itaingia katika majaribio rasmi barabarani. Baada ya uthamini, tutaweza kupanga bei ambayo mteja anaweza kulipia,” amesema.
Mmoja wa watembeleaji ambaye pia alikuwa akipata maelezo juu ya bajaji hiyo, John Julius, amesema uwepo wa bunifu kama hizo unasaidia kurahisisha shughuli za kiuchumi.
“Kama ni mafuta kidogo, mtu anakuwa na uhakika wa kipato. Hii itaimarisha uchumi wa familia nyingi, ukizingatia eneo hili limeajiri vijana wengi,” amesema.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Sabato Masanja, aliyetaka bunifu zinazoweka urahisi katika baadhi ya maeneo ziangaliwe kwa jicho la kipekee, ikiwemo mikopo au ufadhili.
“Kungekuwa na utaratibu wa kuhakikisha watu kama hawa ndiyo wanapewa fedha kwanza, ili waendeleze bunifu zao kusaidia wengine wanaowazunguka,” amesema.