Maumivu mfumuko wa bei sasa yazidi kung’ata nchini

Muktasari:

 Kupanda kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kumeongeza mfumuko wa bei wa Taifa juu zaidi na kuifikia rekodi iliyokuwapo miaka mitano iliyopita.


Dar es Salaam. Kupanda kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kumeongeza mfumuko wa bei wa Taifa juu zaidi na kuifikia rekodi iliyokuwapo miaka mitano iliyopita.

Taarifa mwaka ulioishia Oktoba 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha mfumuko huo umefika asilimia 4.9 kutoka asilimia 4.8 uliokuwapo Septemba 2022.

Kiwango hicho ni cha juu zaidi kwa miezi 60 iliyopita, kwani mara ya mwisho kushuhudiwa ilikuwa Oktoba 2017 kilipofika asilimia 5.1.

NBS imesema mfumuko wa bei mwaka huu umeongezeka kwa miezi minane mfululizo tangu Machi ulipokuwa asilimia 3.6, ukichangiwa na kupanda kwa bei za vyakula, hasa mchele uliopanda kwa asilimia 4.3, ulezi asilimia 0.6, mahindi asilimia 2.0, unga wa mahindi asilimia 3.2, kuku kwa asilimia 0.7, samaki wabichi kwa asilimia 0.4, dagaa wabichi kwa asilimia 8.9, dagaa wakavu asilimia 1.0, matunda asilimia 0.7, maharage asilimia 3.9, soya asilimia 5.1 na choroko asilimia 0.9.

Bidhaa zisizo vyakula zilizochangia mfumuko huo ni gesi asilimia 5.1 na kuni kwa asilimia 2.6.

Ukiacha takwimu za NBS, hata mwenendo wa bei za mazao zinazotolewa na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kila mwezi unaonyesha bei ya mchele, mahindi, mtama, ngano, maharage na viazi mviringo imepaa kwa mwaka mmoja uliopita.

Taarifa za wizara hiyo zinaonyesha bei ya mahindi imeongezeka kwa asilimia 120 kati ya Novemba 5 mwaka 2021 na Novemba 4 mwaka huu, ikitoka Sh48,366 kwa gunia la kilo 100 hadi Sh106,305.

Katika kipindi hicho bei ya mchele nayo ilifika Sh290,594 kutoka Sh173,824, wakati ile ya mtama ilipanda mpaka Sh127,500 kutoka Sh100,667, huku ngano ikifika Sh213,818 kutoka Sh133.182. Maharage yametoka Sh177,471 hadi Sh296,000 na viazi mviringo ni Sh91,781 kutoka Sh67,324.

Suala hilo linaongeza gharama za maisha, hivyo kuacha kilio kwa wananchi ambao wanalazimika kulipa zaidi kukidhi mahitaji yao muhimu kila siku.

Sasa hivi, wakazi wa Arusha wananunua mchele kwa Sh3,000 kutoka Sh1,800 iliyokuwapo miezi mitatu iliyopita, huku unga wa mahindi ukiuzwa Sh1,700 kutoka Sh1,000 kwa kilo moja.

Bei ya mtungi mdogo wa gesi wa kilo sita imepanda kutoka Sh20,000 hadi Sh23,000.

Jonas Mallya, mfanyabiashara katika Soko la Kilombero jijini Arusha alisema kupanda bei ya vyakula kumetokana na uzalishaji mdogo, huku kiasi kikubwa cha nafaka kikisafirishwa kwenda nje ya nchi.

Mjini Moshi nako, kilo moja ya mchele ni Sh3,400 ikipanda kutoka Sh1,500, huku unga wa mahindi ukiuzwa Sh2,000 kutoka Sh900.

Muuza vyakula katika Soko la Mbuyuni mjini hapa, Neema Mushi alisema bei zilianza kupaa baada ya mafuta kupanda.


Namna ya kuikabili hali

Akizungumzia hali iliyopo, Mtaalamu wa biashara na Uchumi, Dk Donath Olomi alisema njia pekee ya kudhibiti mfumuko wa bei ni kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi, yakiwamo mafuta.

“Tutumie nishati yetu kupunguza mfumuko wa bei siku zijazo, kama ni gesi tuongeze matumizi kwenye magari kwa sababu mafuta ndiyo yanapandisha mfumuko wa bei,” alisema na kushauri kuimarisha uzalishaji wa vyakula kwa kilimo kisichotegemea mvua.

Profesa Abel Kinyondo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema ni vyema kuangalia namna ya kuruhusu uingizaji wa baadhi ya vyakula ili kuziba pengo lililopo, kwani ukame umeathiri uzalishaji.

“Kwa kipindi hiki, tunaruhusu uingizaji wa bidhaa ili kuongeza wingi uendane na mahitaji. Haya yanatakiwa kuwa malengo ya muda mfupi, kwa muda mrefu tuimarishe uzalishaji kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji wa matone ili kuzuia upotevu wa maji,” alisema Profesa Kinyondo.

Jijini Mwanza, mchele umepanda kutoka Sh1,200 hadi Sh3,000, huku unga wa mahindi ukitoka Sh1,200 hadi Sh1,700. Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Soko Kuu jijini Mwanza, Ahmad Ncholla alisema maharage yameshuka bei kutoka Sh3,000 mpaka Sh2,800 na mafuta ya kula ambayo hivi sasa lita tano inauzwa Sh32,000 badala ya Sh35,000 iliyokuwa ikiuzwa awali.

Imeandikwa na Aurea Simtowe (Dar), Mussa Juma (Arusha), Saada Amir (Mwanza), Rehema Matowo (Geita) na Beldina Nyakeke (Mara).