Mauzo ya kahawa yaingiza Sh312 bil

Muktasari:

  • Bodi ya Kahawa nchini (TCB) imeuza tani 68,880 za kahawa safi katika msimu wa mwaka 2020/2021 katika mnada na kuliingizia Taifa Dola za Marekani 135.4 milioni (Sh312.8 bilioni).

Moshi. Bodi ya Kahawa nchini (TCB) imeuza tani 68,880 za kahawa safi katika msimu wa mwaka 2020/2021 katika mnada na kuliingizia Taifa Dola za Marekani 135.4 milioni (Sh312.8 bilioni).

Hayo yamebainishwa na Meneja mauzo na ubora wa kahawa wa TCB, Frank Nyarusi, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, baada ya kumaliza msimu wa kahawa na kufanya mnada wa mwisho.

Nyarusi alisema pamoja na kahawa ya Tanzania kutegemea soko la nje kwa zaidi ya asilimia 90, bei ya zao hilo haikuathirika katika kipindi hiki cha Covid-19 na kwamba katika mnada na moja kwa moja bei ipo juu ikilinganishwa na ile ya Soko la Dunia.

Alisema kwa kahawa ya Tanzania aina ya arabika, bei ilikuwa juu kwa asilimia 2.9, huku robusta ikiwa juu kwenye soko la dunia kwa zaidi ya asilimia 25.4, na kwamba hali hiyo imetokana na ubora wa kahawa inayozalishwa hapa nchini, ambacho ndio kigezo kikubwa cha mauzo.

“Kwa msimu huu ambao umefungwa, tumefanya minada 23 -- mbinga minada 6,Songwe minane na Moshi tisa, na katika minada hiyo tumeuza tani 68,880 za kahawa safi ambapo arabika zilikuwa tani 30,375 na robusta tani 38,505,” alisema.

Alisema pia katika msimu huu, mauzo yameongezeka kutoka tani 59,318 za msimu 2019/2020, ambapo waliingiza dola 112.8 milioni za Marekani hadi dola 135.4 milioni za Marekani, sawa na ongezeko la asilimia 13 ikilinganishwa na msimu uliopita.

Aidha Nyarusi alisema, kwa sasa wameanza maandalizi ya msimu mpya ambao unatarajiwa kuanza mwishoni mwa Mei, hivyo amewataka wakulima kuzingatia uzalishaji wa kahawa bora kwa kuwa ndicho kigezo cha kupata bei nzuri.

“Msimu ujao tunakusudia kuzalisha tani 65,000 (arabika tani 35,000 na robusta tani 30,000) na uzalishaji utashuka kwa sababu zao hilo linatokana na mti ambao uzalishaji wake unapanda na kushuka,” alisema.

Alisema kahawa ambayo inazalishwa Tanzania imekuwa na soko kubwa kwenye masoko ya Japan, Italy, Marekani,Ujerumani, Ugiriki na nchi nyingine na kwamba kwa sasa wameanza kuiuza kwenye masoko mapya ya Africa Kusini, Korea, China na nchi za Uarabuni.

Paulo Matemu, mkulima wa kahawa eneo la Kirua Vunjo Wilaya ya Moshi, alisema msimu unaokuja wanatarajia utakuwa mzuri na watapata bei nzuri zaidi ikilinganishwa na bei iliyopatikana katika msimu ulioisha ambapo wameuza kahawa kwa Sh4,000 kwa kilo.

Matemu aliomba vyama vya msingi viruhusiwe kutafuta masoko vyenyewe na visilazimishwe kwenda masoko fulani au kuwa chini ya chama kikuu cha ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU).