Mavunde akataa ukaguzi wa kudhalilisha migodini
Waziri wa Madini, Antony Mavunde, akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Bukombe, mkoani Geita.
Muktasari:
- Hatua hiyo inajiri kufuatia malalamiko ya wachimbaji kwenye mgodi wa Msasa uliopo wilayani Bukombe kulalamikia upekuzi mpaka sehemu za siri pindi wanapotoka duarani, hali inayotweza utu wao.
Geita. Waziri wa Madini, Antony Mavunde amemwagiza Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Mbogwe, kushirikiana na wasimamizi wa Mgodi wa Msasa uliopo Kata ya Runzewe Magharibi, Wilaya ya Bukombe, kuhakikisha wanaweka vifaa vya kisasa vya ukaguzi (scanner) ili kuondoa utaratibu wa upekuzi wa kizamani unaodaiwa kuvunja heshima na utu wa wachimbaji.
Waziri Mavunde ametoa agizo hilo leo Jumamosi, Julai 25, 2026, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Uyovu Runzewe, wilayani Bukombe, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Geita.
Hatua hiyo imekuja baada ya mchimbaji mmoja, Sebastian Aron kuwasilisha malalamiko kwa Waziri kwa niaba ya wachimbaji wa mgodi huo, akieleza kuwa wanakumbana na utaratibu wa ukaguzi ambao umekuwa ukiwakwaza na kuwafanya wajisikie kudhalilishwa.
Sebastian amesema mara wanapotoka eneo la uchimbaji, hukaguliwa getini na wakati mwingine kufanyiwa upekuzi hadi maeneo ya siri, jambo alilodai linawavunjia heshima na utu wao.
"Unatoka duarani unafika getini unasachiwa. Unaambiwa vua gumboot, unasachiwa mpaka sehemu za siri. Sasa sielewi hizo taratibu wanazotumia wakati mtu hana mfuko, ametoka duarani akiwa amechoka, lakini bado anakaguliwa kwa namna hiyo," amesema.
Baada ya kupokea malalamiko hayo, Waziri Mavunde amemtaka Ofisa Madini Mkazi kushirikiana na uongozi wa mgodi huo kutafuta suluhisho la kisasa litakalowezesha ukaguzi kufanyika bila kutweza utu wa wachimbaji.
Amesema matumizi ya teknolojia kama scanner yanaweza kusaidia kubaini kama mtu amebeba madini bila kulazimika kutumia njia zinazoweza kuathiri utu wa mtu.
"Lazima kuwepo na heshima na staha wakati wa ukaguzi. Tusitweze utu wa watu. RMO, nakuomba lisimamie hili. Mkakae na uongozi wa mgodi mtafute namna bora. Kama inawezekana kutumia scanner, iwekwe ili kama mtu ana jiwe litambulike bila kuanza kuingiza mikono," amesema.
Hata hivyo, Waziri Mavunde amewataka pia wachimbaji kuacha vitendo vya wizi wa madini na kuhakikisha wanafuata utaratibu na sheria zilizowekwa na waajiri wao.
"Lakini Sebastian na ninyi punguzeni ujanja, huo ndiyo ukweli. Kuna njia nyingi ambazo watu wanazitumia kuondoka na madini bila kugundulika. Kwa hiyo nanyi zingatieni taratibu na msivunje sheria," amesema.
Katika hatua nyingine ya ziara yake, Waziri Mavunde amekagua ujenzi wa soko na stendi ya mabasi katika Kata ya Katente, Tarafa ya Ushirombo, Wilaya ya Bukombe, na kumwagiza mkandarasi anayetekeleza miradi hiyo kukamilisha kazi kwa wakati kulingana na mkataba.
Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutafungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi na kuchochea shughuli za biashara katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Haruni Fashe, miradi hiyo inatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh22 bilioni na inatarajiwa kukamilika Desemba 2027.
Amesema kwa sasa utekelezaji wa mradi wa soko umefikia asilimia 46.