Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbalamwezi ilivyowaletea wavuvi wa dagaa nidhamu ya fedha

Mafundi wakiendelea kukarabati mtumbwi katika Mwalo wa Mswahili jijini Mwanza baada ya kusimama kwa uvuvi wa dagaa kwa siku 10 kupisha mbaramwezi. Picha na Saada Amir

Muktasari:

  • Kusitishwa kwa uvuvi wa dagaa kipindi cha mbalamwezi kulianza Januari, 2023 ili kukidhi Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003, na kanuni yake ya mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2029 na 2020.

Mwanza. Ingawa kusimamishwa kwa shughuli za uvuvi wa dagaa katika Ziwa Victoria kila unapotanda mwanga mkali kuwa pigo kwa wavuvi, kwa upande mwingine hatua hiyo imetajwa kuwaongezea nidhamu ya matumizi ya fedha.

Kila mwezi, mwanga mkali unapotanda juu ya ziwa hilo kutokana na mbalamwezi, shughuli za uvuvi wa dagaa husimama kwa siku 10.

Kwa wavuvi waliokuwa wamezoea kuingia ziwani kila usiku hatua hiyo awali iliibua taharuki na malalamiko, lakini kadiri muda ulivyopita mtazamo umebadilika na manufaa yake yameanza kuonekana.

Katika Mwalo wa Mswahili, wenye wachuuzi wa mazao ya uvuvi zaidi ya 100 na hutembelewa na zaidi ya watu 250 kwa siku, hali ya maisha hubadilika kipindi cha mbalamwezi.

Si Mswahili pekee, mialo maarufu ikiwemo Igombe, Kayenze kubwa na ndogo, ghana, Bezi, Kirumba, Mihama ambayo huwa na pilikapilika usiku kucha, taa za kuvutia dagaa zikimulika majini, na kelele za injini za mitumbwi, ghafla hutulia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Maeneo ya Fukwe (BMU) mwalo wa Mswahili, Lugo Fasheni anasema mwanzo wa utekelezaji wa utaratibu huo haukuwa rahisi kwa wavuvi wengi.

“Ilileta taharuki kidogo...watu hawakuelewa waliona kama wameonewa na Serikali. Lakini baadaye kila mmoja ameona umuhimu wake kwanza imejenga nidhamu ya matumizi ya fedha,” anasema.

Anaeleza kabla ya utaratibu huo, wavuvi wengi walikuwa hawana mpango wa matumizi ya kipato chao, wakipata fedha wanatumia siku hiyohiyo hadi iishe.

“Mvuvi alikuwa amezoea kila siku anaenda ziwani...akipata laki moja anatumia yote bila kujali kesho, lakini sasa anajua kuna siku 10 hatokwenda kuvua hivyo analazimika kupanga matumizi yake. Nidhamu imeongezeka sana,” anaongeza.

Hali ilivyo baada ya shughuli za uvuvi wa dagaa kusimama kupisha mbaramwezi katika meza za wachuuzi wa dagaa katika Mwalo wa Mswahili uliopo jijini Mwanza. Picha na Saada Amir

Mbali na nidhamu ya fedha, Fasheni anasema utaratibu huo umeimarisha mahusiano ya kifamilia kwa wavuvi ambao awali walikuwa wanatumia muda mwingi mwaloni au kwenye maisha ya starehe.

“Wavuvi wengi walikuwa wanakesha mwaloni au wengine wakimaliza kazi wanaenda kulala kwenye vyumba vya wageni...lakini sasa wanarudi nyumbani, wanakaa na familia zao, wanashiriki majukumu ya nyumbani. Hili limeleta mabadiliko makubwa kijamii,” anasema.

Kwa upande wa uzalishaji, matokeo yake pia yameonekana wazi ambapo inaelezwa dagaa wanaovuliwa sasa ni wakubwa zaidi na wenye thamani sokoni ukilinganisha na hapo awali.

“Hapo mwanzo dagaa walikuwa wadogo sana, lakini sasa wanapata muda wa kukua, hivyo wanakuwa wakubwa na wanauzika kwa bei nzuri zaidi,” anasema.

Fasheni anasema kipindi hicho kinawapa wavuvi nafasi ya kufanya matengenezo ya zana zao za kazi ikiwemo mitumbwi na nyavu ili kuendelea na shughuli zao pindi mbalamwezi ikiisha.

“Kama nyavu zilikuwa zinavuja, wanazivuta juu na kuzitengeneza. Mitumbwi nayo inakarabatiwa, hii inasaidia kuongeza ufanisi wanaporudi kazini,” anaeleza.

Kwa wanawake wanaojishughulisha na biashara ya dagaa, kipindi hicho kimekuwa fursa ya ubunifu wa kiuchumi ambapo wiki moja kabla ya shughuli kusitishwa, wengi huandaa akiba ya dagaa kwa ajili ya kuuza wakati wa mbalamwezi.

Maisara Joseph, mchuuzi wa dagaa katika mwalo huo, anasema awali alikuwa na hofu kubwa kuhusu kipato chake, lakini baadaye akaanza kukausha dagaa ili auze kipindi hicho kikifika.

“Mwanzo nilikuwa na mawazo sana nilijiuliza familia yangu itaishije kwa siku hizo 10 kwa sababu nilitegemea kuuza dagaa mbichi tu.”

“Nilianza kuuza dagaa kavu pia. Wakati wa uvuvi nauza mbichi, lakini kipindi cha mbalamwezi nauza kavu ambazo zinakuwa na soko kubwa kwa sababu hakuna dagaa mbichi....hii imenisaidia sana,” anaeleza.

Kwa upande wa wavuvi, baadhi wanakiri kupata muda wa kufanya mambo mengine muhimu nje ya uvuvi baada ya shughuli zao kusitishwa kutokana na mbalamwezi.

Mvuvi wa dagaa, Henry Shibula anakiri ni kweli wanapata nafasi ya kufanya mambo mengine shughuli zikisitishwa ikiwemo kutembelea ndugu na marafiki, kukaa na familia zao pamoja na kuwa na nidhamu ya pesa, akiomba siku za kusitisha shughuli zao zipungue angalau ziwe tano.

"Mimi ni mvuvi lakini pia ni mmiliki wa mashine..nakodisha mashine kwa siku Sh10,000 kama tusipofanya kazi siku 10 inamaanisha napoteza Sh100,000,"anasema.

Mwenyekiti wa Mwalo wa Mswahili, Lugo Fasheni akionesha meza tupu zinazotumiwa na wachuuzi wa dagaa kinapofika kipindi cha mbaramwezi. Picha na Saada Amir


Walichokisema Tafu

Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi Tanzania (TAFU), Bakari Kadabi anasema utaratibu huo si mpya bali ni wa muda mrefu japo kwa kipindi fulani ulisitishwa.

“Huu utaratibu ulikuwepo tangu zamani. Wavuvi waliingia ziwani siku 10 na kutoka siku 10 kwa sababu dagaa wanategwa gizani. Lakini kadri watu walivyoongezeka, taratibu zilianza kupuuzwa,” anasema.

Anaeleza kurejeshwa kwa utaratibu huo kumesaidia kulinda rasilimali za uvuvi hasa dagaa na samaki wachanga.

“Katika siku hizo 10 dagaa wanapata muda wa kuzaliana na kukua, hii ni faida kwa kila mtu, mvuvi, mfanyabiashara na mlaji,” anasema.

Kadabi anaongeza kuwa baadhi ya wavuvi hutumia kipindi hicho kuhamia kwenye uvuvi wa samaki wengine kama sangara, huku wengine wakirudi nyumbani kupumzika.

Ofisa Uvuvi Mkoa wa Mwanza, Titus Kilo anasema utaratibu huo una msingi wa kisheria ambao kila mvuvi wa dagaa analazimika kuufuata.

“Utaratibu wa kusitisha uvuvi wa dagaa kipindi cha Mbalamwezi upo kisheria, kwa mjibu wa Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003, na kanuni yake ya mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2029 na 2020,

"Hii inatoa mwanya kwa dagaa kuzalia na kukua ili kuongeza wingi wa dagaa ziwani,"anasema.

Anasisitiza kuwa bila utaratibu huo, kuna hatari ya kupungua kwa rasilimali hiyo muhimu.

Mvuvi Elelath Mbugi anasema utaratibu huo una faida kubwa hasa kuhakikisha dagaa zinazaliana na kukua ambapo mwisho wa siku walaji na wafanyabiashara hiyo wananufaika.

Kusitishwa kwa uvuvi kipindi cha mbalamwezi kulianza Januari, 2023, kwa mujibu wa Kaimu Ofisa Mfawidhi Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda ya Ziwa, Laurent Mbunjiro zuio na aina hiyo litafanyika kila mwezi wakati wa mbalamwezi.