Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbunge ataka tozo mpya za simu kujenga barabara

Muktasari:

  • Kauli ya Kakoso imekuja katika kipindi ambacho wabunge wamekuwa wakipiga kelele kutaka Serikali ipunguze tozo na kodi kwenye eneo la mafuta ili kusaidia bei zisipande.

Dodoma. Mbunge wa Tanganyika (CCM), Seleman Kakoso amependekeza Serikali kuongeza tozo kwenye mawasiliano ya simu ili zisaidie kujenga miundombinu ya barabara.

Pendekezo hilo la Kakoso ni kama ambalo limewahi kutolewa mwaka 2021 na Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu la kuanzishwa kodi ya uzalendo itakayokatwa katika mitandao ya simu kwa kila Mtanzania.

Pendekezo la Zungu ambaye sasa ni Spika wa Bunge lilifanyiwa kazi ambapo kwenye bajeti ya 2021/22 Serikali ilianzisha kodi kwenye simu na Zungu akichangia bungeni Juni 17, 2021 alitetea uamuzi huo wa Serikali.

Alisema Tanzania ina watu milioni 55 lakini wanaolipa kodi hawafiki milioni tano, hivyo ili kuibeba nchi ni lazima Watanzania wote wajitoe mhanga. Alisisitiza tozo hiyo inamfanya mwananchi wa kawaida achangie mchango wake kwenye barabara, bima na afya.

Leo Jumatatu Aprili 13, 2026 wakati akichangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, Kakosa naye amesema mpango huo wa tozo unaweza kukusanya hadi Sh1 trilioni.

Taarifa zilizopo zinaonyesha mpaka sasa Tanzania inatoza kodi kwa takribani asilimia 40 katika huduma za simu nchini sehemu kubwa ikiwa ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru wa bidhaa (Excise Duty).

Kauli ya Kakoso imekuja katika kipindi ambacho wabunge wamekuwa wakipiga kelele kutaka Serikali ipunguze tozo na kodi kwenye eneo la mafuta ili kusaidia bei zisipande.

Kingine ni kilio cha Watanzania kwa muda mrefu wanaolalamikia gharama kubwa za mabando na muda wa maongezi wakitaka kampuni za mawasiliano kufikiria namna ya kuzipunguza.

"Mheshimiwa mwenyekiti, mimi nina mapendekezo mawili, kwanza Serikali iendelee kudhibiti mapato lakini tukubaliane kuanzisha chanzo kipya cha mapato kwenye muda wa maongezi katika simu zetu," amesema Kakoso.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ametaka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuweka tozo ya Sh100 kwenye muda wa maongezi ambayo itasaidia kukusanya zaidi ya Sh1 trilioni.

Amesema fedha hizo zikikusanywa zigawiwe katika mafungu mawili yaani Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kiasi alichoeleza kitakuwa msaada kwenye matengenezo ya miundombinu.

Kwa mujibu wa Kakoso mvua zilizonyesha katika msimu huu zilikuwa nyingi kiasi cha kuharibu miundombinu hata zikasababisha mikoa ya Kigoma na Katavi kuwa kisiwani.

Amesema hali hiyo inaweza kuzuilika ikiwa Serikali itakuwa na vyanzo vya uhakika wa kupata fedha kwa ajili ya kukarabati na kujenga miundombinu yake kila inapotokea uharibifu.