Mchele kicheko, viazi vyang’ata tena Mbeya wakulima
Muktasari:
- Mbeya ni mkoa maarufu kwenye kilimo ukijivunia mazao ya biashara na chakula ikiwa ni viazi, ndizi, mpunga na mengineyo ambapo kwa hivi karibuni bei ya bidhaa imekuwa ikipanda na kushuka.
Mbeya. Wakati wananchi jijini Mbeya wakichekelea kushuka kwa bei ya mchele, hali imekuwa tofauti kwenye viazi mviringo kufuatia kupanda kwake, huku wafanyabiashara na wakulima wakitoa mitazamo tofauti.
Kwa miezi kadhaa nyuma, bei ya mchele ilifika hadi Sh70,000 kwa ndoo ya kilo 20, ambapo kwa sasa imeonekana kushuka hadi Sh55,000 kwa bei ya juu, huku viazi vilivyouzwa Sh22,000 kwa ndoo kubwa ilishuka awali hadi Sh12,000 na sasa imepaa tena hadi Sh18,000.
Mwananchi imefika katika soko la Sido, ambapo bei ya mchele katika mashine za kusaga na kukoboa mpunga na kushuhudia bei ya mchele kuuzwa kati ya Sh32,000 hadi Sh45,000 kwa ndoo ya kilo 20.
Wafanyabiashara katika soko la Sido wakisaga na kukoboa mpunga katika mashine za mchele, ambapo kwa sasa bei imefika kati ya Sh 32,000 hadi Sh 45,000.
Kwa upande wa maduka, bei imekuwa tofauti ikiwa ni kati ya Sh38,000 hadi Sh55,000 kulingana na aina ya mchele na ubora wake, huku ikielezwa huenda bei ikazidi kushuka kutokana na wingi wa bidhaa hiyo shambani.
Wakizungumza leo Juni 24 baadhi ya wafanyabishara wamesema kushuka kwa bei ya mchele ni ahueni kwa wananchi na kilio kwa wakulima kutegemeana na malengo ya kila mmoja.
Diana Thadeo ambaye ni mkulima na mfanyabiashara wa mpunga amesema gharama za kilimo ni kubwa hivyo walitarajia wanapofika wakati wa mavuno wakute soko lina changamka kwa bei kubwa.
“Kwa maana hiyo mimi ambaye nategemea kilimo sioni nafuu kwa kuwa natumia gharama, nguvu na muda mwingi kuandaa shamba hadi kuvuna, nachotarajia ni kuuza kwa bei ya juu ili nipate faida”
“Ninapouza mchele kwa Sh30,000 ndoo kubwa kwangu ni hasara japokuwa mwananchi ambaye anasubiri kununua ndiye anafaidika, kwa sasa tunakubaliana kwakuwa msimu huu mchele umekubali shambani” amesema Diana.
Kwa upande wake, Christopher Mzanila amesema kwa sasa mpunga shambani ni mwingi na huenda bei ikaendelea kupungua kwa kuwa msimu ndio unaanza rasmi akieleza kuwa ni nafuu kwa wananchi.
“Hata hivyo, maisha yenyewe yamepanda gharama, Mungu ameona asaidie kupitia upande huu wa mchele watu wasife njaa, lakini kwetu wafanyabiashara ni hasara tunataka tukivuna tuuze kwa faida,” amesema Mzanila.
Naye Stella Funga mfanyabiashara wa viazi amesema kwa sasa bei ya bidhaa hiyo imepanda tena kufikia Sh18,000 ikilinganishwa na miezi mitatu nyuma ilipouzwa kwa Sh12,000 kwa ndoo kubwa.
“Kwa gunia tunanunua Sh 95,000 kwa sasa, hivyo kwa sokoni ndoo inauzwa Sh 18,000 ukumbuke lakini kati ya Desemba mwaka jana hadi kuja Machi na Aprili ilishuka hadi Sh12,000, sababu ni msimu unaelekea mwishoni,” amesema Stella.