Migogoro, ukosefu wa masoko vyatikisa ushirika Morogoro
Wafanyakazi wa vyama vya ushiriki vya akiba na mikopo wakiwa katika maandamano ya kuadhimisha siku ya ushirika duniani iliyoambatana na jukwaa la maendeleo ya ushirika yaliyofanyika Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
Muktasari:
- Wanaushirika Mkoa wa Morogoro wameiomba Serikali kuingilia kati migogoro ya wakulima na wafugaji pamoja na kutafuta masoko ya uhakika ya mazao wakisema changamoto hizo zinapunguza uzalishaji huku Mkoa ukijivunia vyama 212 vya ushirika vilivyosimamia mauzo ya mazao yenye thamani ya zaidi ya Sh134 bilioni.
Morogoro. Wakati Mkoa wa Morogoro ukiendelea kujivunia mafanikio makubwa ya sekta ya ushirika yaliyowezesha kusimamia mauzo ya mazao ya wakulima yenye thamani ya zaidi ya Sh134 bilioni, wanaushirika wameiomba Serikali kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji pamoja na kuhakikisha kunapatikana masoko ya uhakika ya mazao.
Changamoto hizo, zinaendelea kudhoofisha uzalishaji, kupunguza kipato cha wakulima na kuwakatisha tamaa baadhi yao kuendelea na kilimo cha biashara.
Akizungumza leo Juni 24, 2026 katika maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani kimkoa yaliyofanyika Ifakara, Wilaya ya Kilombero, Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro, Cesilia Sostenes amesema ushirika umeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa Mkoa kupitia usimamizi wa mazao, huduma za kifedha na uwekezaji.
Cesilia amesema maadhimisho hayo wameambatana na Jukwaa la Sita la Maendeleo ya Ushirika yakibeba kaulimbiu za "Ushirika kwa Dunia yenye Amani" na "Linda Ushirika, Chagua Uadilifu."
Amesema Mkoa wa Morogoro una jumla ya vyama vya ushirika 212, vikiwemo vyama vya msingi vya mazao 168, SACCOS 36, vyama vikuu vitatu na miradi ya pamoja mitano, huku idadi ya wanachama ikifikia 69,639, wakiwemo wanaume 38,767 na wanawake 30,872.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani kimkoa yaliyofanyika katika Mji Mdogo wa Ifakara, Wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
Cesilia amesema katika msimu wa 2025/2026 vyama vya ushirika vilisimamia mauzo ya kilo 21,408,497 za ufuta zenye thamani ya Sh53.9 bilioni, kilo 28,194,517 za mbaazi zenye thamani ya Sh28.2 bilioni, kilo 1,216,740 za kakao zenye thamani ya Sh17.4 bilioni na kilo 435,337 za korosho zenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni, huku wakulima wakilipwa kwa wakati fedha zao.
Aidha, amesema tani 495,000 za miwa zenye thamani ya Sh34 bilioni ziliuzwa katika viwanda vya Kilombero, Mtibwa na Mkulazi, huku zaidi ya Sh2 bilioni zikikusanywa kupitia ushuru na tozo mbalimbali kwa halmashauri zote tisa za Mkoa.
Alisema mafanikio mengine ni kuunganisha vyama 23 vya mazao na Saccos na taasisi za fedha ili viweze kupata mikopo, pamoja na kusaidia Serikali kupata takwimu sahihi za uzalishaji na biashara ya mazao mbalimbali.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Morogoro, Idadi Bilali, amesema pamoja na mafanikio hayo, migogoro ya wakulima na wafugaji pamoja na ukosefu wa masoko ya uhakika bado ni changamoto kubwa inayodhoofisha maendeleo ya wanaushirika.
Amesema migogoro hiyo imeathiri maeneo mbalimbali yakiwemo Bonde la Mbigiri na Mtibwa ambako wakulima wa mpunga, miwa na mazao mengine wamekuwa wakipata hasara kubwa, huku baadhi yao wakikata tamaa ya kuendelea na kilimo cha biashara.
Bilali amesema pia mazao kama mpunga, mahindi, maharage na mboga mboga yanaendelea kuuzwa kwa walanguzi kutokana na kukosekana kwa masoko ya uhakika, jambo linalowanyima wakulima faida stahiki.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya amesema Morogoro inapaswa kujifunza kutoka mikoa iliyofanikiwa katika kuendesha vyama vya ushirika ili kuongeza ufanisi, uwazi na maendeleo ya wanachama.
Amesema mafanikio ya ushirika yataongezeka zaidi endapo changamoto zilizopo zitapatiwa ufumbuzi, huku akisisitiza kuwa uadilifu, ushirikiano na amani ni msingi wa maendeleo ya sekta hiyo.
"Mkoa wa Morogoro una kila sababu ya kuwa kinara wa ushirika nchini, lakini hilo linawezekana iwapo tutaimarisha usimamizi wa vyama, kutatua migogoro na kuhakikisha wakulima wanapata masoko yenye tija kwa mazao yao," amesema Kyobya.