Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miradi ya umwagiliaji ulivyokwama baada ya ufadhili kukoma

Baadhi ya miradi ya umwagiliaji kwa kutumia umeme jua nchini Tanzania ilizinduliwa kwa matumaini makubwa ya kuinua kilimo, kuongeza uzalishaji na kupunguza utegemezi wa mvua.

Miradi hii ikiwa mingine ni ya ufadhili kutoka mashirika ya kimataifa ilionekana kama suluhisho la muda mrefu kwa changamoto za kilimo cha kutegemea mvua.

Hata hivyo, licha ya matarajio hayo, miradi hii imeshindwa kuzaa matokeo yaliyokusudiwa huku sababu kuu zikihusishwa na usimamizi duni na ukosefu wa ufuatiliaji endelevu.

Baadhi ya miundombinu ya umwagiliaji imebaki magofu bila matumizi huku mingine ikifanya kazi chini ya kiwango kilichokusudiwa huku ikiacha wakulima waliokuwa na matumaini katika sitofahamu huku baadhi wakirudi katika kilimo cha kawaida cha mvua hali inayorudisha nyuma juhudi za kuongeza uzalishaji na usalama wa chakula nchini.

Mwananchi ilifunga safari na kushuhudia baadhi ya miradi katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ikiwa haifanyi kazi kama inavyotakiwa huku wakulima wakionyesha kutonufaika nayo licha ya kuonekana kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa kutosha kusukuma maji kwenda kwenye mashamba.

Kutofanya kazi kwa miradi hiyo kuliifanya miundombinu iliyokuwapo kama Sola, matanki ya kutunzia maji kutekelezwa huku baadhi ya wakulima wakikumbuka ahadi walizokuwa wamepewa awali lakini hawaoni matunda yake.

Mussa Mshana mkulima kutoka kitongoji cha Kilimambogo wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro anasema kilimo hicho cha umwagiliaji kwa kutumia umeme jua kilitumia miaka miwili pekee lakini hakuna walichofaidika.

Kwa muda mrefu wamekuwa wakitegemea mvua na wakati mwingine mvua zilizokuwa juu ya kiwango walihifadhi maji katika Kware kwa ajili ya kuyatumia katika kilimo cha umwagiliaji jambo ambalo anakiri kuwa halikuwa likitoa ufanisi wa asilimia 100.

Hiyo ni kwa sababu maji hayo yalitosha kuhudumia wakulima wachache waliokuwa katika eneo hilo ambao waliweza kuufikiwa na maji kupitia kufunguliwa kwa kutumia kifereji.

“Hatujafaidika chochote kwa kweli, sasa hivi tu hautumiki imebidi tumuachie mlinzi awe anatumia katika kupanda mbogamboga zake kama sehemu ya malipo ya ulinzi anaofanya ili vifaa hivyo visiibiwe,” anasema Mshana.

Anasema wanahisi kuwa sola hizo hazina uwezo wa kusukuma maji licha ya matarajio yao ya awali kuwa ni kunywesha ekari 200 za mazao lakini sasa hata nusu ekari kwa siku inakuwa ni ngumu kuweza kumudu huku kukosekana kwa mtaalamu anayeweza kuangalia tatizo la mfumo huo kuwa changamoto nyingine.

Maneno yake yaliungwa na Aimtongga Minja ambaye ni mjumbe wa kamati wa shamba la umwagiliaji wa bonde la ubonyo lililopo kitongoji cha Kilimambogo ambaye anabainisha kuwa mradi huo ni kama umefeli kwani hawaoni dalili ya kupata matokeo waliyoahidiwa awali.

Mradi huo kwa mujibu wao ulikuwa wa shirika la Can Tanzania na ulibeba matumaini makubwa ya kubadilisha maisha lakini sasa wamerudi kusubiri msimu wa mvua ndiyo walime.

“Naweza kusema ni maumivu kwani kwa ukanda wetu huu mvua huwa inanyesha kidogo, haitoshi kufikisha mazao msimu wa mavuno. Yaani tunatamani hata serikali ingeangalia faida ya huu mradi ikatuma wataalamu ili watusaidie kunufaika na kile kilichokuwa kimepangwa awali,” anasema.

Kilio kichopo eneo hilo, kipo pia katika Kijiji cha Mkombozi ambapo pia walibahatika kupata mradi kama huo ambapo wakulima 80 walipangwa kuwa wanufaika lakini sasa imekuwa ni ndoto kutokana na utendaji kazi hafifu.

“Kadri walivyokua wamesema tulitarajia tutanufaika, tunaomba serikali iangalie namna ya kusaidia,” anasema Hussein Kheri kutoka Kijiji hicho.

Anasema kutokana na kutofanya kazi kama ilivyokuwa imekusudiwa, waliahidiwa kupewa betri ili kuwezesha usukumaji wa kiwango kikubwa jambo ambalo halikufanyika na baadaye likawekwa wazo la wakulima kuchangishwa ili kununua betri hilo ambapo sasa wanasubiri utekelezaji wake.

“Sisi mara zote tulikuwa tunatumia mifereji ya asili katika kumwagilia mashamba yetu, mifereji hii inaanzia eneo la Udoro na kumekuwa na zamu za kumwagilia, upande wetu ni siku za Ijumaa, wengine Alhamisi wengine Jumatatu,” anasema.

Batuli Munisi kutoka Kijiji hicho anasema walitumia mradi huo kwa takribani miaka miwili ukiwa ni utekelezaji wa mradi wa Shirika la Can Tanzania lakini hakuna hawajanufaika.

“Mradi ulipokuja tuliambiwa utatusaidia sisi wakulima lakini sasa hilo halipo na matokeo yake watu wanalima tu mbogamboga zisizowapa faida, tatizo ni pampu inayotoa maji kidogo sana,” anasema.

Selemani Hussein anasema mradi huo kwa siku sasa unaweza kumwagilia takribani nusu ekari huku akiiomba serikali ikiwa kuna namna ambayo inaweza kufanya iboreshwe ili uweze kuwa na uwezo wa kumwagilia mashamba yote.

Mwenyekiti na msimamizi wa mradi huo, Juma Ulomi anasema walipopelekewa wazo la mradi Kijiji kiliona nuru ndani yake hali iliyofanya walazimike kutafuta eneo ambalo mradi huo utawekwa na ndipo walipoamua kununua eneo.

Anasema kwa zaidi ya miaka mitatu tangu mradi huo umepelekwa hawajawahi kumwagilia zaidi ya nusu ekari kwa siku jambo ambalo liliua matumaini waliyokuwa nayo.

“Baada ya kuona malengo tuliyokuwa nayo hayafikiwi, tuliwaomba Can Tanzania wauboreshe lakini hatujawahi kuwaona tena. Tunaiomba serikali, hili eneo ni zuri kwa shughulii za umwagiliaji na wananchi ili waweze kujikwamua wanahitaji maji ya kutosha ndiyo maana mradi ulipo,” anasema.

Mwananchi ililitafuta shirika la Can Tanzania ili kuweza kujua mipango iliyopo katika kuendeleza miradi hiyo lakini iliambiwa kuwa hakuna mradi wa aina hiyo kwa sasa unaotekelezwa.

“Kwa sasa hatuna mradi kama huo,” mwandishi alijibiwa kwa ufupi kupitia ujumbe mfupi wa maandishi na Boniventure Mchomvu ambaye ni Mkuu wa Program wa shirika hilo.

Alipoulizwa ikiwa miradi tajwa awali wanaitambua alisema “Ndiyo maana nimesema kwa sasa hatuna miradi ya aina hiyo.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa miradi hiyo ilikuwa kitekelezwa kwa kipindi cha miama miwili (2021-2022) kupitia Shirika la Can Tanzania ikiwa ni ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ).

Lengo lake ilikuwa ni kuwawezesha wakulima wadogo na walio katika mazingira magumu katika vijiji vitatu vya Ngosero, Kilima Mbogo na Mkombozi vilivyopo wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo mwaka 2021 ulikuwa mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mradi huu.

Kutofanya kazi kwa miradi hii baada ya muda wa ufadhili kuisha kuliibua shauku ya kutaka kujua takwimu halisi za miradi ya ufadhili ya umeme jua iliyopo nchini na mingapi inayofanya kazi.

Kwa Bahati mbaya, hakukuwapo takwimu sahihi linaloonyesha hali halisi huku kila mmoja akimrushia mwenzake mpira.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Nishati Jadidifu Tanzania (Tarea), Dk Matthew Matimbwi alipoulizwa alisema “Hakuna usajili wa miradi. Kinachosajiliwa ni kupata vibali vya matumizi ya maji kutoka river basins,” aliandika kupitia ujumbe mfupi wa maandishi.


Wadau watoa neno

Wakati kutoendelea kufanya kazi kwa miradi hii baada ya muda kukionekana kuwa na mauumivu kwa wakulima, Meneja Programu kutoka Taasisi ya Elico, Adrian Mapunda kutoka taasisi ya Elico ambayo pia inatekeleza miradi ya umwagiliaji kwa kutumia umeme jua anasema ipo namna inayoweza kutumika ili miradi iendelee kuleta matunda hata ufadhili unapokoma.

Hiyo itawezekana kwa kuangalia namna mradi utakavyojiendesha baadaye na kuwekewa mikakati ikiwemo kutengeneza thamani ambayo itafanya wanufaika waweze kuendelea kuhudumia na hilo linaanza kuanzia kwenye kubuni mradi.

“Hii itaonyesha kuwa katika miaka mitatu mradi huu utakuwa na hali gani na itakuwaje, mingi inakuwa na mashine fulani sasa unajiuliza baada ya miaka miwili ikipata hitilafu nani anatengeneza au spea inapatikana wapi hivyo hili linaandaliwa kabisa kama ni mtu wa kijijini anafundishwa kutengeneza,” anasema.

Anasema kukosekana kwa mipango mizuri kumefanya baadhi ya miradi kufanya kazi kwa muda Fulani na kufa huku mingine baada ya muda inabadili maisha ya watu.

“Kama ilikuwa wanamwagilia kwa gharama kubwa inapungua kama ilikuwa ikitumia nishati chafu ya petroli sasa inamwagiliwa kwa kutumia nishati safi, hii baada ya mwaka inaboresha shughuli za mtu kwa kumuongezea kipato au kupunguza gharama,” anasema.

Hata hivyo anasema baadhi ya watu hubuni bila kufanya ushirikishaji au wengine wakifanya ofisini badala ya Kwenda kwa jamii jambo ambalo linaondoa ujumuishi.

“Ukishirikisha wananchi unakuwa wanajua wanataka nini na wewe unawapa, tofauti na kubuni mradi kwenye kompyuta na kupeleka kijijini mambo mengi yanaweza kutokea ikiwemo wao kutoupenda. Wakishirikishwa wanakuwa wanaona ni wao,” anasema.

Meneja Miradi kutoka ESAFF, Emmanuel Justine anasema umwagiliaji unaotumia nishati ya jua ni chanya sana muhimu kwa kilimo cha wakulima wadogo kwa kuwa unapunguza gharama za uzalishaji, unaondoa utegemezi wa mvua na nishati zisizo za uhakika na unamwezesha mkulima kulima kwa msimu mzima, hivyo kuongeza uzalishaji, kipato na usalama wa chakula.

Anasema ili miradi hii isife baada ya wafadhili kuondoka lazima ijengwe juu ya umiliki na usimamizi wa wakulima wenyewe, iwe sehemu ya mipango ya maendeleo ya vijiji na kata na ya serikali za mitaa.

“Pia isimamiwe kama uwekezaji endelevu badala ya mradi wa muda mfupi. Kuwe na mfumo wa usimamizi ambao uongozi wake ni wa wakulima wenyewe,” anasema.

ESAFF inasisitiza kuwa angalau asilimia 10 ya bajeti ya Taifa ielekezwe kwenye kilimo na fedha hizo zitumike kimkakati kuwekeza kwenye mifumo ya umwagiliaji, hususan inayotumia nishati ya jua kwa kuhakikisha inarudisha manufaa ya moja kwa moja kwa wakulima kupitia ongezeko la kipato, ajira vijijini na upatikanaji wa chakula cha uhakika.


Serikali

Wakati uwekezaji kwa kutumia umeme jua ukiendelea kupigiwa chapuo serikali imeendelea kuongeza miradi ya umwagiliaji inayotekelezwa ikiwemo kuchimba visima na mabwawa na sasa imetoka miradi 13 mwaka 2020/2021 hadi miradi 780 mwaka 2024/2025.

Miradi hiyo yenye ukubwa wa hekta 543,366 utekelezaji wake unakadiriwa kugharimu Sh1.34 bilioni. Kukamilika kwa miradi 780 inayoendelea kutaongeza eneo la umwagiliaji hadi kufikia hekta 1,270,647.