Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mitazamo ya wadau tozo mpya za bandari

Dar es Salaam. Wakati tozo mpya ya Ada ya Uendelezaji wa Miundombinu ya Bandari (PID) ya asilimia 4.5 ikianza Julai Mosi, 2026, wadau wa bandari wametoa mitazamo tofauti ikiwemo jinsi mikakati inavyopaswa kufanyika ili kuboresha miundombinu.

Tozo hiyo ambayo awali ilipangwa kuwa asilimia tisa ya kodi ya forodha, sasa imepunguzwa hadi asilimia 4.5 kufuatia mashauriano kati ya Serikali, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na wadau wa bandari.

Baadhi ya wadau wanaona hatua hiyo ni muhimu kwa mustakabali wa bandari za Tanzania huku wengine wakitaka ushirikishwaji mpana zaidi kabla ya utekelezaji wake kutokana na hofu ya kuongeza gharama za bidhaa kwa mlaji wa mwisho.

Sababu za kuanzishwa kwa tozo hizo kwa mujibu wa TPA ni kupata fedha za kuboresha zaidi miundombinu ya bandari zake ili iendane na mahitaji ya sasa na kuondoa msongamano bandarini na wa malori kwenye maeneo kadhaa ya Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Dk George Fasha anasema hatua hiyo inatokana na ongezeko la shehena linalotokana na juhudi za maboresho yaliyofanyika katika bandari za Dar es Salaam na Tanga zilizovutia watumiaji wa ndani na nje ya nchi.

Dk Fasha anasema awali ada hizo zilizokuwa zianze kutumika Januari mwaka huu zilikuwa asilimia tisa lakini baada ya kupokea maoni na ushauri wa wadau mbalimbali, TPA imezipunguza hadi asilimia 4.5 sawa na punguzo la asilimia 50.

Anatolea mfano, kwa mteja ambaye alipaswa kulipa Sh200,000 kama Ada ya Uendelezaji wa Miundombinu mipya ya Bandari, kupitia maboresho ambayo yamefanyika hivi sasa, mteja huyo atalipa Sh100,000 badala ya Sh200,000 kama ilivyokuwa hapo awali.


Mitazamo ya wadau

Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bandari Kavu Tanzania (CIDAT), Meleck Shange amesema lengo la tozo hiyo ni kusaidia ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya bandari nchini ili ziweze kuhimili ongezeko kubwa la shehena na ushindani wa kikanda.

“Awali tozo ilikuwa asilimia tisa lakini baada ya majadiliano ikashushwa hadi asilimia 4.5. Hii siyo kwa ajili ya Bandari ya Dar es Salaam pekee bali bandari zote nchini. Lengo ni kuhakikisha miundombinu inakuwa rafiki na ya kisasa,” amesema.

Amesema pamoja na kuwepo kwa wawekezaji wanaoendesha baadhi ya huduma bandarini, jukumu la kuboresha miundombinu bado lipo chini ya TPA.

“Kwa sasa tuna gati 12 wakati baadhi ya nchi jirani zina zaidi ya gati 24. Hivyo kuna haja ya kuongeza uwezo huo ili meli zisikae nje kusubiri kwa muda mrefu, jambo ambalo linaongeza gharama za usafirishaji,” amesema.

Kwa mujibu wa Shange, kuchelewa kwa meli bandarini huongeza gharama ambazo mwishowe hubebwa na mlaji wa mwisho kupitia kupanda kwa bei za bidhaa sokoni.

“Bandari ikifanya kazi kwa haraka na meli zikahudumiwa kwa wakati, hata gharama kwa mlaji wa mwisho zitashuka,” amesema.

Mbali na hilo, amesema maboresho ya bandari yatafungua ajira mpya kwa Watanzania katika maeneo ya usafirishaji, uhifadhi wa mizigo na huduma za bandari kavu.

Mwenyekiti wa Baraza la Wasafirishaji Shehena Tanzania (TSC), Clement Kamendu amesema sekta ya bandari haiwezi kuendelea bila uwekezaji mkubwa wa miundombinu.

“Tumepokea tozo hii kwa mtazamo chanya kwa sababu kama taifa tunahitaji kuboresha bandari zetu. Ukiangalia ukuaji wa biashara na shehena, maboresho haya hayaepukiki,” amesema.

Kamendu amesema uamuzi wa Serikali kupunguza kiwango cha tozo kutoka asilimia tisa hadi 4.5 pamoja na kusogeza mbele tarehe ya utekelezaji ni ishara ya usikivu kwa wadau.

“Wadau tuliomba muda wa kujiandaa na Serikali imesikiliza. Hilo ni jambo zuri,” amesema.

Amesema matarajio ya wadau ni kuona huduma bandarini zikiboreshwa sambamba na utekelezaji wa tozo hiyo ili kupunguza gharama za biashara na kuongeza ushindani wa Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Bandari ni mali ya taifa. Kama tunataka ziwe za kisasa lazima tuwekeze ndani yake kama nchi nyingine zinavyofanya,” amesema.

Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mawakala wa Meli Tanzania (Tasaa), Abel Uronu amesema maendeleo ya sekta ya usafirishaji duniani yamebadilisha aina ya meli zinazotumika, jambo linalolazimisha bandari nazo kubadilika.

“Zamani kulikuwa na meli zinazobeba kila kitu, lakini sasa kuna meli maalumu za makontena, magari na mizigo mingine maalumu. Huwezi kuleta meli ya kisasa kwenye bandari isiyo na uwezo wa kuihudumia,” amesema.

Amesema mamlaka nyingi za bandari duniani zimekuwa zikiwekeza kwenye mifumo ya kisasa na teknolojia ili kuendana na kasi ya biashara ya kimataifa.

“Kuna bandari sasa kila kitu kinafanyika kidijitali na watu wachache sana wanahitajika. Hivyo nasi lazima tuende na wakati,” amesema.

Kwa mujibu wa Uronu, tozo kama hiyo ni sehemu ya mikakati ya muda mrefu ya kuziwezesha bandari kukabiliana na ushindani wa kikanda na kimataifa.


Kauli ya TPA

Wakati wao wakiyasema hayo, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Dk George Fasha amesema mapato yatakayokusanywa kupitia ada hiyo yatawezesha TPA kugharamia miradi 13 ya kimkakati inayolenga kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya bandari ndani ya miaka mitano ijayo.

“Iwapo TPA itaendelea na mfumo wa sasa wa kukusanya fedha kidogo kidogo bila ada maalumu, inaweza kuchukua kati ya miaka mitano hadi 10 kutekeleza mradi mmoja tu kati ya miradi tuliyopanga,” amesema.

Amesema kuchelewa kwa uwekezaji wa miundombinu kunaweza kuwa kikwazo kwa ukuaji wa uchumi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya usafirishaji wa bidhaa na malighafi.

Kwa mujibu wa TPA, shehena inayopita bandarini inatarajiwa kuongezeka kutoka tani milioni 32.8 mwaka 2024/25 hadi tani milioni 62 ifikapo mwaka 2030/31.

Dk Fasha amesema ongezeko hilo linaonyesha umuhimu wa kuwekeza mapema katika bandari ili kuepuka msongamano wa mizigo na ucheleweshaji wa huduma.

Akifafanua ukubwa wa ongezeko hilo, amesema tani milioni 32.8 zinazohudumiwa sasa zingehitaji zaidi ya malori milioni 1.3 kama zingesafirishwa kwa wakati mmoja, huku tani milioni 62 zikihitaji takribani malori milioni 2.48.

“Hii inaonyesha ukubwa wa fursa na changamoto iliyopo mbele yetu. Tusipochukua hatua sasa, bandari zinaweza kuwa kikwazo cha biashara na maendeleo badala ya kuwa kichocheo cha uchumi,” amesema.

TPA inaamini maboresho ya bandari yataongeza mapato ya taifa, ajira na ushindani wa Tanzania katika kuhudumia nchi jirani zinazotegemea bandari zake kwa biashara ya kimataifa.

Mei 23, 2026 wakati Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilipotembelea Bandari ya Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa alisema Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kushirikisha sekta binafsi katika miundombinu ya bandari, reli na usafirishaji kwa ujumla ili kuongeza ufanisi na ushindani wa sekta hiyo.

“Matokeo ya ushirikiano huo yameonekana wazi ambapo uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam wa kushughulikia mizigo umeongezeka kutoka wastani wa kontena 61,000 hadi zaidi ya 110,000 kwa mwezi,” amesema.