TPA yapunguza ada mpya bandari, yaanika mpango wa trilioni 16.1
Muktasari:
- Hatua hiyo imekuja wakati mamlaka hiyo ikiweka wazi mpango wa uwekezaji wenye thamani ya Sh16.1 trilioni kwa ajili ya kupanua na kuboresha bandari.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetangaza kupunguza Ada ya Uendelezaji wa Miundombinu Mipya ya Bandari (PID) kutoka asilimia tisa hadi 4.5 ya kodi ya forodha, hatua inayolenga kupunguza mzigo kwa wafanyabiashara na wadau wa sekta ya usafirishaji.
Machi mwaka huu, TPA ilitangaza kuanza kwa ada mpya za mizigo ya ndani katika bandari nchini, iliyoibua malalamiko kutoka kwa wadau, wakisema inaongeza gharama za biashara.
Hata hivyo, ada hizo zilizokuwa zimeanza kutumika Machi 8, 2026, baadaye zikasitishwa. Hatimaye zimetangazwa upya zikipunguzwa kutoka asilimia tisa hadi 4.5.
Tayari, Chama cha Mawakala wa Forodha (Tacas), kilishaishauri Serikali kuachana na ada hiyo, kikipendekeza vitafutwe vyanzo vingine mbadala vya mapato.
Hatua hiyo kwa mujibu wa TPA, imekuja wakati mamlaka hiyo ikiwa na mpango wa uwekezaji wenye thamani ya Sh16.1 trilioni kwa ajili ya kupanua na kuboresha bandari mbalimbali nchini katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Akizungumzia punguzo hilo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Dk George Fasha, amesema uamuzi wa kupunguza tozo hiyo umetokana na maoni na ushauri wa wadau waliotaka mapitio ya kiwango hicho kipya.
“Tumepokea maoni ya wafanyabiashara, waingizaji na wasafirishaji wa mizigo na kuyafanyia kazi. Kutokana na maboresho hayo, ada hiyo imepunguzwa kutoka asilimia tisa hadi asilimia 4.5 ya kodi ya forodha,” amesema.
Amesema kiwango hicho kipya kitaanza kutumika rasmi Julai Mosi mwaka huu na kwamba kitapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za biashara bandarini.
“Kwa mfano, kama mteja alikuwa anatakiwa kulipa Sh200,000 chini ya kiwango cha zamani, sasa atalipa Sh100,000 tu,” amesema.
Kwa mujibu wa TPA, tozo hiyo imeanzishwa kusaidia upatikanaji wa fedha za miradi ya upanuzi wa bandari kutokana na ongezeko kubwa la shehena nchini.
Dk Fasha amesema bila kuwa na chanzo maalumu cha fedha, utekelezaji wa miradi ya kimkakati ungechukua muda mrefu zaidi na kuathiri ukuaji wa sekta ya usafirishaji pamoja na uchumi wa taifa.
Taarifa ya TPA inaonyesha kuwa kwa sasa wastani wa meli 20 husubiri nje ya Bandari ya Dar es Salaam kila siku kutokana na uhaba wa nafasi za gati, huku idadi ya malori yanayoingia na kutoka bandarini ikiongezeka kutoka 1,000 hadi 3,000 kwa siku ndani ya miaka mitano.
Kutokana na hali hiyo, TPA imeanza utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwamo ujenzi wa magati mapya, gati za mafuta, matenki ya kuhifadhi mafuta, bandari kavu pamoja na kuboresha reli na barabara.
Miradi mingine ni maendeleo ya Bandari ya Bagamoyo, Mwambani na bandari maalumu ya Kisiwa Mgao mkoani Mtwara.
Amesema katika miezi tisa ya mwaka wa fedha 2025/26, bandari zote nchini zilihudumia tani milioni 29.6 za shehena na makasha zaidi ya milioni moja kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania.