Hizi hapa bajeti za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda
Muktasari:
- Kenya yaongoza kwa kuwa na bajeti kubwa ambayo ni Sh97 trilioni, ikifuatiwa na Tanzania yenye bajeti ya Sh62.33 trilioni, Uganda (Sh58 trilioni), Rwanda (Sh13.9 trilioni) na Burundi (Sh6.2 trilioni).
Dar es Salaam. Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimewasilisha bajeti zao za Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27 huku baadhi zikiweka nguvu kwenye mapato ya ndani kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Mawaziri wa fedha katika nchi za Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi wamewasilisha bajeti katika mataifa yao, kwa mujibu wa makubaliano ya EAC, yanayotaka nchi hizo kuwasilisha bajeti zao siku moja.
Kenya imeongoza kwa kuwa na bajeti kubwa ambayo ni Sh97 trilioni, ikifuatiwa na Tanzania yenye bajeti ya Sh62.33 trilioni, Uganda (Sh58 trilioni), Rwanda (Sh13.9 trilioni) na Burundi (Sh6.2 trilioni).
Baadhi ya bajeti hizo zimepunguza kiwango cha kodi kwa wananchi wa kawaida kama chanzo kikuu cha mapato, badala yake zimejielekeza kwenye kutumia rasilimali zilizopo kuongeza mapato ya Serikali kwa ajili ya kufadhili bajeti.
Bajeti ya Kenya
Waziri wa Fedha wa Kenya, John Mbadi amewasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27 ambapo imepanga kukusanya na kutumia jumla ya KSh4.8 trilioni (Sh97 trilioni).
Bajeti hiyo inakwenda sambamba na maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027 katika michakato yake ya awali ikiwamo uandikishaji wapigakura.
Serikali imejizuia kuanzisha kodi mpya kutokana na athari za Muswada wa Fedha wa mwaka 2024 uliosababisha maandamano ya umwagaji damu, zinazoendelea kuathiri mikakati ya Serikali ya kuongeza mapato.
Kwa mwaka wa pili mfululizo, Waziri Mbadi ameweka matumaini yake katika kuimarisha ukusanyaji wa kodi na hatua nyingine za kiutawala ili kuongeza mapato ya serikali kwa KSh232 bilioni na kufikia KSh3.67 trilioni katika mwaka wa fedha 2026/27.
Hatua hizo zinajumuisha kuimarisha uthibitishaji wa matumizi kupitia mfumo wa Ankara za Kielektroniki wa Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA), unaojulikana kama eTIMS, kuunganisha mifumo ya KRA na jukwaa la eCitizen pamoja na mifumo mingine ya malipo ya kidijitali, na kufanya ukaguzi zaidi ili kuwafikia walipa kodi wengi kutoka sekta isiyo rasmi.
Serikali pia imefanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Mapato kwa kuanzisha kodi ya zuio kwenye ada za miamala ya kadi za malipo na huduma za wafanyabiashara.
Aidha, Wizara ya Fedha imependekeza marekebisho yatakayoweka kiwango cha chini cha asilimia 60 ya mapato ambayo kampuni haijagawanya kwa wanahisa wake kutambuliwa kama gawio la kubuniwa (deemed dividend), ambalo litatozwa kodi ya zuio.
Uganda na uchumi wa mafuta
Serikali ya Uganda imewasilisha bajeti ya USh84 (Sh58 trilioni) huku ikitarajia uchumi wake kukua katika miaka kadhaa ijayo huku ikitabiri ongezeko kubwa la shughuli za kiuchumi litakalochochewa na kuanza kwa uzalishaji wa kibiashara wa mafuta baadaye mwaka huu.
Akiwasilisha bajeti ya taifa ya mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi, Henry Musasizi amesema uchumi wa nchi hiyo unatarajiwa kukua kwa asilimia 10.2 katika mwaka huo wa fedha.
Iwapo makadirio hayo yatatimia, Uganda itakuwa imerejea katika ukuaji wa uchumi wa tarakimu mbili kwa mara ya kwanza tangu kipindi cha mageuzi ya kiuchumi ya miaka ya 1990.
Musasizi amesema ukuaji huo mkubwa wa uchumi utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kwa kuongeza ajira, kuinua kipato cha kaya na kupanua fursa za biashara.
“Jambo muhimu zaidi ni kwamba uchumi mkubwa zaidi utazalisha ajira nyingi, utaongeza mapato ya kaya, kupanua fursa za biashara na kuzalisha rasilimali zinazohitajika kuwekeza katika elimu bora, huduma za afya, miundombinu, usalama na huduma nyingine za umma zinazoboresha maisha ya wananchi wa Uganda,” amesema.
Waziri huyo amesema matarajio hayo yanatokana na mafanikio ya mkakati wa muda mrefu wa serikali wa kuwekeza katika sekta za usalama, miundombinu, uzalishaji mali na shughuli nyingine za kiuchumi.
Licha ya misukosuko ya biashara ya kimataifa na hali ya kutokuwa na uhakika katika uchumi wa dunia, Musasizi amesema matarajio ya uchumi wa Uganda yanaendelea kuwa mazuri.
“Uchumi uko imara. Ukuaji unaongezeka. Mfumuko wa bei uko chini. Kiwango cha ubadilishaji wa fedha kipo thabiti. Mauzo ya nje yanaongezeka. Uwekezaji unaimarika. Na imani kuhusu mustakabali wa Uganda inaendelea kuwa kubwa,” amesema mbele ya wabunge na wageni waliohudhuria hafla hiyo.
Kwa mujibu wa waziri huyo, wastani wa mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.8 katika mwaka wa fedha 2025/26, ikilinganishwa na asilimia 3.5 mwaka uliotangulia.
Musasizi amesema hali hiyo imechangiwa na uratibu mzuri wa sera za fedha na matumizi ya serikali, utulivu wa bei za vyakula pamoja na kuboreka kwa upatikanaji wa mafuta ya petroli.
Rwanda yagonga Sh13.9 trilioni
Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi wa Rwanda, Yusuf Murangwa amewasilisha bajeti ya taifa ya mwaka wa fedha 2026/27 bungeni, ambapo nchi hiyo imepanga kukusanya na kutumia Rwf7.8 trilioni (Sh13.9 trilioni).
Murangwa amesema uchumi wa nchi hiyo unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.8 mwaka 2026 na kwamba kiwango hicho cha ukuaji ni cha chini ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 9.4 uliorekodiwa mwaka 2025.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa bajeti hiyo, waziri huyo amesema makadirio hayo yanaonyesha kuwa uchumi wa Rwanda utaendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha licha ya changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazolikabili eneo la Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa bungeni, ukuaji wa asilimia 9.4 ulioshuhudiwa mwaka 2025 ulikuwa miongoni mwa viwango vya juu zaidi katika ukanda huo, huku ukichochewa na kuimarika kwa shughuli za uzalishaji, huduma na uwekezaji.
Hata hivyo, serikali imekadiria kuwa kasi ya ukuaji itapungua hadi asilimia 6.8 mwaka 2026, kiwango ambacho bado kinaonesha uchumi wa nchi hiyo utaendelea kuwa imara na kuhimili misukosuko ya kiuchumi ya kimataifa.
Murangwa alisema serikali itaendelea kutekeleza sera na mipango mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuimarisha uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kuongeza ajira ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaendelea kuwanufaisha wananchi.
Burundi kutumia Sh6.2 trilioni
Waziri wa Fedha, Bajeti na Mipango ya Uchumi wa Burundi, Dr Alain Ndikumana amewasilisha bungeni bajeti ya taifa ya mwaka wa fedha 2026/27 inayofikia Sh6.28 trilioni ikilinganishwa na Sh5.35 trilioni zilizotengwa katika mwaka wa fedha uliopita.
Kwa mujibu wa takwimu za bajeti hiyo, mapato ya serikali yanatarajiwa kufikia Sh5.5 trilioni huku matumizi yakizidi mapato kwa takribani Sh503 bilioni.
Nakisi hiyo ya bajeti inaonyesha kuwa serikali italazimika kutafuta vyanzo vya ziada vya fedha ili kuziba pengo kati ya mapato na matumizi yaliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Ongezeko la bajeti linaashiria dhamira ya serikali ya kuendelea kufadhili shughuli mbalimbali za maendeleo na utoaji wa huduma za umma, licha ya changamoto za kifedha zinazoikabili nchi hiyo.
Wachambuzi wa uchumi wanaeleza kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo utategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa serikali kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kupata msaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Kwa ujumla, bajeti ya mwaka 2026/27 ni kubwa zaidi kuliko ya mwaka uliotangulia, jambo linalodhihirisha matarajio ya serikali ya kuongeza uwekezaji katika sekta muhimu za uchumi na huduma za kijamii huku ikikabiliana na changamoto ya nakisi ya bajeti.