NHC kuzindua sera ushirikiano na sekta binafsi

Muktasari:

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), linatarajia kuzindua sera ya ubia ya ushirikiano na sekta binafsi itakayowezesha utakelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na uboreshaji wa majengo yenye hali ya mbaya yanayomilikiwa na shirika hilo.

Dar es Salaam. Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), linatarajia kuzindua sera ya ubia ya ushirikiano na sekta binafsi itakayowezesha utakelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na uboreshaji wa majengo yenye hali ya mbaya yanayomilikiwa na shirika hilo.

Hatua ya uzinduzi wa sera hiyo, itakayofanyika Oktoba 21 mwaka huu,  itatoa fursa kwa NHC kuingia ubia na sekta ya binafsi kwa ajili kujenga miradi ya maendeleo katika viwanja inavyovimiliki vilivyopo mkoa mbalimbali ukiwamo wa  Dar es Salaam mtaa wa  Samora Avenue na eneo la Bilcanas.

Pia, ubia huo utawezesha uboreshaji  majengo yenye hali mbaya ya NHC ya mitaa mbalimbali  ikiwemo ya Kariakoo na Upanga ambayo yatajengwa kisasa na kutoa fursa ya familia nyingi pamoja eneo kubwa la biashara.

Meneja wa Habari na Uhusiano wa  NHC,  Muungano Saguya amewaambia wanahabari leo Jumanne Oktoba 21, 2022 kwamba sera ya ubia inakwenda kufungua milango ya uwekezaji katika sekta ya nyumba.Akisema hatua hiyo inaungana mkono maelekezo ya Rais Samia Suluhu kuruhusu sekta binafsi kuwekeza mitaji ili kujenga uchumi wa Taifa.

" Sera ambayo tunawaalika Watanzania kushiriki ilianzishwa mwaka 1993 na kufanyiwa maboresho kadhaa kulingana na wakati husika.Maboresho yaliyofanyika mwaka 2022 yamezingatia uwekezaji kwa kuwa na yana maslahi kwa NHC na mwekezaji," amesema.

Saguya amesema takribani washiriki 600  wakiwamo wa taasisi  za Serikali na binafsi, vyama na bodi za kitaaluma, pamoja na wawekezaji binafsi wa nje na ndani ya nchi watahudhuria uzinduzi utakaofanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Mkurugenzi wa Uendelezaji na Biashara wa NHC, William Genya amesema baada ya uzinduzi huo shirika hilo litatoa matangazo kwenye vyombo vya habari ya kuwaita wawekezaji watakaohitaji kuwekeza katika maeneo yatakayoanishwa.