Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NMB, DSE walivyorahisisha ununuzi, uuzaji hisa kidijitali

Muktasari:

  • Huduma hiyo inawawezesha Watanzania kujisajili, kununua, kuuza hisa na kupata taarifa za soko kwa urahisi. Serikali imepongeza ubunifu huo kwa kusaidia elimu ya uwekezaji, ushirikishwaji wa kifedha na kukuza masoko ya mitaji nchini.

Dar es Salaam. Benki ya NMB kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), wamezindua ushirikiano wa kimkakati na wa kidijitali kwa ununuzi na uuzaji wa hisa za kampuni mbalimbali.

Hisa hizo ni zile zilizoorodheshwa DSE ambapo, kupitia aplikesheni ya NMB Mkononi, unaweza kupata huduma ya uuzaji na ununuzi wa hisa za DSE.

Ushirikiano huo ni matokeo ya ubunifu na ushirikiano wa muda mrefu kati ya NMB na DSE, uliounganisha rasmi mifumo miwili ya suluhisho za kidijitali, NMB Mkononi ya Benki ya NMB na Hisa Kiganjani ya Soko la Hisa Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo, Julai 10, 2025 jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema wanajivunia ushirikiano huo na DSE, uliozaa huduma hiyo inayowapa Watanzania na wawekezaji njia rahisi, salama na za kisasa za kushiriki uwekezaji.

“Huduma hii ya ununuzi na uuzaji wa hisa kupitia NMB Mkononi, ni matokeo ya ubunifu na ushirikiano baina ya NMB na DSE, uliounganisha mifumo na bunifu, hatua iliyowezeshwa kwa juhudi za wataalamu wa Tehama kutoka pande zote mbili.

“Kupitia huduma hii tunayozindua leo, wateja wa NMB wataweza kujisajili, kununua, kuuza hisa na kufanya malipo kupitia akaunti za NMB, kupata taarifa ya thamani ya uwekezaji wao, kuona bei za hisa zilizoorodheshwa DSE na kujua mwenendo wa soko la hisa.

“Hili ni jukwaa linalokwenda kuleta mapinduzi ya kweli katika ushiriki wa Watanzania kwenye sekta ya fedha, hususan masoko ya mitaji na dhamana, lakini pia ni kielezo na uthibitisho wa dhamira ya NMB kuwezesha ushirikishwaji wa kifedha kwa njia ya teknolojia,” amesema Zaipuna.

Kwa upande wake, akizindua huduma hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amezipongeza NMB na DSE kwa ubunifu wa kiwango cha juu unaokwenda kuisaidia Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika maeneo makuu manne muhimu kiuchumi.

Ameyataja maeneo hayo, aliyosema yamo katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo, kuwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, kusaidia kubadili mitazamo ya wananchi, kuelimisha jamii juu ya uwekezaji, na kuchagiza ushirikiano kwa taasisi za ndani.

“Hili linalofanyika hapa ni tukio zuri na la maana sana. Pongezi kwa NMB na DSE kwa huduma hii. Kwetu sisi kama Serikali, ni jambo kubwa, muhimu na la maana linalokwenda kutusaidia katika maeneo ambayo ni muhimu kwa ustawi na ukuaji wa kiuchumi.

“Moja, huduma hii inaenda kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi. Serikali tuna Mpango wa Maendeleo wa Taifa, ambao unataka ifikapo mwaka 2030, huduma zote za kiserikali zimfikie mwananchi popote alipo. Hili mnalozindua leo, mmetutangulia sana,” amesema na kuongeza;

“Pili, mnaenda kusaidia kubadili mitazamo ya wananchi walio wengi. DSE ni kongwe, ilipoanza ilikuwa ngumu kumwambia Mtanzania anunue hisa. Sasa hii huduma inakwenda kubadili mitazamo ya Watanzania juu ya hisa kwamba utajiri sio tu kuwa na magari, majumba na viwanda, bali hata hisa ni utajiri pia.

“Pia, katika eneo la tatu, huduma hii itakuza uelewa katika suala zima la uwekezaji. Kwa kweli huduma hii inaenda kuchochea uwekezaji miongoni mwa Watanzania. Inakwenda kubadili mitazamo hasi juu ya uwekezaji kwamba sio kwa ajili ya wageni tu, bali hata wazawa wanapaswa na wanaweza kuwekeza.

“Ili uchumi ukue, watu wanahitaji kuwekeza na hatua ya kwanza ni uwekaji akiba. Ili akiba izae, ndipo linapokuja suala la ununuzi wa hisa, ambao una faida kubwa. Eneo la nne ni ushirikiano mliokuja nao NMB na DSE. Ni taasisi za ndani zenye mafanikio, na mnapokuja na aina hii ya ushirikiano, mnachagiza wengine,” amebainisha Profesa Kitila.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela, amesema wanajisikia fahari, siyo tu kwa kuwa sehemu ya ushirikiano wa muda mrefu na NMB, bali pia kwa kufanikisha uzinduzi wa huduma bora ya kidijitali inayokwenda kutanua wigo wa ushiriki wa Watanzania katika masuala mazima ya uwekezaji kwa njia ya hisa.

“NMB ni taasisi inayoaminika, kinara wa ushirikishaji jamii katika huduma jumuishi za kifedha kwa Watanzania wa kada zote. Ushirikiano huu na huduma hii ni uthibitisho kuwa taasisi hizi mbili zina dhamira ya dhati ya kukuza maslahi na ustawi wa wananchi.

“Wito wetu kwa umma, hasa vijana, wawekeze si kwa sababu wana pesa nyingi, bali kwa sababu wanahitaji kuwa na kesho iliyo bora. Na sisi kwa upande wetu tunapambana kuondoa dhana hasi kuwa uwekezaji ni lazima uwe na mabilioni ya fedha, bali kwa kiasi chochote unaweza kuanza nacho uwekezaji,” amesema Nalitolela.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa Soko la Mitaji na Dhamana (CMSA), Alfred Mkombo, akimwakilisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama, ameitaja huduma hiyo kuwa ni hatua muhimu katika sekta ya fedha, hasa Soko la Mitaji na Dhamana nchini.

“Sisi CMSA, tukiwa wasimamizi wa mitaji, tuna jukumu la kusimamia huduma zote za Masoko ya Mitaji. Tunapongeza jitihada hizi za NMB na DSE kwa sababu ubunifu wao unaenda kutanua wigo wa masoko ya mitaji kuyafikia makundi yaliyoachwa nyuma katika hili.

“Huduma hii inayozinduliwa leo inaenda kuwa chachu ya wananchi wote kushiriki katika fursa za uwekezaji mijini na vijijini, hasa ukizingatia kuwa NMB Mkononi ina mtandao mpana unaojumuisha wateja zaidi ya milioni saba wa kada tofauti kote nchini,” amesema.