Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NMB kufadhili zana za kilimo

Muktasari:

  • Wakulima wanaweza kumiliki matrekta, zana za kusafirishia mazao na mashine nyingine za kilimo kwa utaratibu wa malipo ya awamu

Dar es Salaam. Wakati sekta ya kilimo ikiendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Tanzania na chanzo cha ajira kwa mamilioni ya wananchi, Benki ya NMB imeongeza nguvu katika ufadhili wa zana za kilimo ikiwemo matrekta.

Hiyo inalenga kutoa suluhisho za kifedha zinazolenga kuwawezesha wakulima, wanunuzi wa mazao, wachakataji na wafanyabiashara kupata mitaji na kumiliki vifaa vya kisasa vya kilimo.

Kupitia huduma hizo, wakulima sasa wanaweza kumiliki matrekta, zana za kusafirishia mazao na mashine nyingine za kilimo kwa utaratibu wa malipo ya awamu hatua inayolenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mitaji na kuongeza tija katika uzalishaji.

Akizungumza katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkuu wa Idara ya Kilimo kwa Wateja Wakubwa wa Benki ya NMB, Christopher Mwalugenge amesema benki hiyo imeweka mfumo wa mikopo unaozingatia mahitaji ya wadau wote waliopo katika mnyororo wa thamani wa kilimo.

Amesema mfumo huo unawahusisha wanaonunua mazao kutoka kwa wakulima kuyachakata na kuyapeleka katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Kwa sasa ni msimu wa mavuno kwa mazao mbalimbali ikiwamo kahawa, tumbaku, ufuta na pamba. Kupitia suluhisho zetu za kifedha, tunawawezesha wateja kupata mikopo ya kununua mazao kutoka kwa wakulima, kuyachakata, kuyauza na kurejesha mikopo kwa mfumo unaoendana na mzunguko wa biashara zao,” amesema Mwalugenge.

Amesema benki hiyo imeendelea kubuni huduma zinazolenga kupunguza changamoto za mitaji, kuongeza uzalishaji na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya ndani.

Katika kuimarisha uzalishaji wa kilimo, NMB imeendelea kuwawezesha wakulima kumiliki vifaa vya kisasa kupitia mpango wa ufadhili wa vifaa ambapo mkulima anaweza kuanza kwa kulipa asilimia 10 ya thamani ya kifaa na kuendelea kulipa kwa awamu kulingana na msimu wa uzalishaji.

Meneja Uhusiano wa Kitengo cha Kilimo kutoka Makao Makuu ya NMB, Elias Leasa amesema mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia mazingira halisi ya wakulima na namna wanavyopata mapato.

“Tumetengeneza utaratibu ambao unamwezesha mkulima kupata vifaa vya kilimo kwa urahisi. Mteja anatakiwa kuanza kwa kulipa asilimia 10 ya thamani ya kifaa, kisha anaendelea kulipa kulingana na msimu wa mavuno kwa muda uliokubaliwa,” amesema Leasa.

Amesema malipo yanaweza kufanyika mara moja, mara mbili au mara tatu kwa mwaka kulingana na aina ya zao analolima mkulima.

Amesema mwamko wa kutumia huduma hiyo umeongezeka katika maeneo mbalimbali nchini, hususan Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati na Kanda ya Kaskazini.

Mkulima Dustan Alan Bembati ambaye ni mnufaika wa mpango huo, amesema upatikanaji wa trekta utamsaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa zana za kilimo ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiathiri shughuli za uzalishaji.

“Changamoto kubwa tuliyonayo wakulima ni vifaa vya kilimo hasa wakati wa kulima. Matrekta yaliyopo kwa ajili ya kukodi hayatoshi, hivyo wakati mwingine mkulima anaweza kusubiri hadi wiki mbili bila kupata huduma. Kupata trekta hili kutanisaidia mimi pamoja na wakulima wengine wanaonizunguka,” amesema Bembati.

Amesema pamoja na changamoto ya matrekta, wakulima pia wanakabiliwa na uhaba wa mashine za kuvunia na maghala ya kuhifadhi mazao, hali inayowalazimu baadhi yao kuuza mazao baada ya kuvuna ili kuepuka gharama za usafirishaji na uhifadhi.