Taasisi zaalikwa soko la mitaji kuongeza uwekezaji
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Peter Nalitolela (wapili kushoto) akipokea tuzo maalumu ya kutambua mchango wake katika Sekta ya Fedha, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (kulia), katika hafla ya Maadhimisho ya Miaka 30 ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) iliyofanyika katika jijini Dar es Salaam. Picha na Mpigapicha Wetu
Muktasari:
- Waziri wa Fedha Hamisi Mussa Omar amezitaka taasisi za umma na binafsi kujiunga soko la mitaji, kwa kuwa ni fursa muhimu ya kuongeza uwekezaji na ukuaji wa uchumi.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imezitaka taasisi za umma, mashirika ya Serikali na kampuni binafsi ambazo bado hazijajiunga na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), kulitumia kikamilifu kama chanzo mbadala cha mitaji ili kuongeza uwekezaji, kupanua uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa Julai 3, 2026 na Waziri wa Fedha, Hamisi Mussa Omar, alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 30 ya DSE jijini Dar es Salaam, yaliyowakutanisha viongozi wa Serikali, wadau wa sekta ya fedha, wawekezaji na wafanyabiashara kujadili safari, mafanikio na mwelekeo wa soko la mitaji nchini.
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri Omar amesema Tanzania ina fursa kubwa ya mitaji inayoweza kutumika na taasisi mbalimbali kupitia soko la mitaji, hivyo ni muhimu kwa kampuni na mashirika kuachana na utegemezi mkubwa wa mikopo ya kibenki.
"Ninapongeza DSE na taasisi zote zilizotimiza miaka 30. Tumeona benki kubwa kama NMB na CRDB pamoja na kampuni maarufu kama Tanga Cement zikijiunga na soko hili na kunufaika. Nazitaka taasisi nyingine zijiunge na DSE ili nazo zipate fursa hizo," amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha sera za sekta ya fedha pamoja na kuongeza elimu ya fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ili kuwapa wananchi na taasisi uelewa mpana wa kutumia fursa zilizopo katika soko la mitaji.
"Tunao mtaji wa kutosha na uelewa wa wananchi unaongezeka. Fursa za hati fungani na bidhaa nyingine za soko la mitaji zinapaswa kutumiwa kikamilifu. Nazitaka taasisi zote na mashirika kuchangamkia fursa hizi ili kuongeza tija na kuharakisha maendeleo ya uchumi," amesema.
Waziri Omar amesema hatua ya taasisi nyingi kuingia katika soko la mitaji itasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya uwekezaji, sambamba na kuongeza ushiriki wa wananchi katika umiliki wa kampuni kubwa nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama amesema maadhimisho ya miaka 30 ya DSE ni fursa ya kutathmini safari ya soko hilo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, mafanikio yaliyopatikana na hatua za kuimarisha mazingira ya uwekezaji.
Amesema tangu kuanzishwa kwake, DSE ilisajiri kampuni ya kwanza mwaka 1998 na hadi sasa kampuni 28 zimeshaorodheshwa katika soko hilo, huku thamani ya soko ikifikia zaidi ya Sh72.4 trilioni.
"Hii ni safari ya miaka 30 yenye mafanikio makubwa. Tumeboresha mazingira ya uwekezaji kupitia miongozo takribani 19, inayolenga kurahisisha upatikanaji wa mitaji na kuimarisha ushiriki wa wadau," amesema.
Mkama amesema Serikali na CMSA zinaendelea kuhimiza taasisi zaidi kuingia sokoni ili kupanua wigo wa uwekezaji na kuongeza mchango wa soko la mitaji katika uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela amesema hadi kufikia Juni 2026, thamani ya kampuni zilizoorodheshwa imefikia zaidi ya Sh35 trilioni huku uwekezaji kupitia soko hilo ukizidi Sh2 trilioni.
Amesema maendeleo ya teknolojia yameongeza upatikanaji wa huduma za soko la mitaji na kuongeza idadi ya wawekezaji kufikia zaidi ya 870, hali inayochochea ukuaji wa kampuni na kuongeza ajira nchini.
"Niungane na Waziri wa Fedha kutoa wito kwa mashirika ya umma na kampuni binafsi kujiunga na Soko la Hisa la Dar es Salaam ili kunufaika na fursa zilizopo," amesema Nalitolela.
Amesema historia ya DSE imepitia hatua muhimu tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, ikiwemo kuorodhesha kampuni ya kwanza mwaka 1998, kampuni ya kwanza ya kigeni mwaka 2004, kuanza matumizi ya mfumo wa kisasa mwaka 2006, kuorodhesha benki ya kwanza ya biashara mwaka 2008, kampuni ya kwanza ya madini mwaka 2011 na kuzindua Enterprise Growth Market (EGM) mwaka 2013.
Kwa mujibu wa Nalitolela, mageuzi hayo yameifanya DSE kuwa soko imara la mitaji nchini, huku akisisitiza kuwa ushiriki mpana wa taasisi na wananchi ndio nguzo ya kuimarisha zaidi sekta ya masoko ya mitaji nchini.