Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NMB na mageuzi ya kidijitali kupitia simu ya mkononi

Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki ya NMB, Ruth Zaipuna (kushoto) akipata ufafanuzi katika banda la maonyesho la Nmb Kikundi kupitia NMB Mkononi, katika uzinduzi wa NMB Mkononi leo Jumanne Juni 16, 2026 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • NMB Mkononi Super App imeongezewa baadhi ya huduma zinazoweza kutumiwa na mtumiaji, ikiwemo kulipia bima, kukata tiketi za treni ya umeme (SGR), kupata mikopo, kufungua akaunti na kununua bando.

Dar es Salaam. Katika dunia inayoendeshwa kwa kasi kubwa ya mageuzi ya teknolojia, taasisi za fedha zimeanza kubadili mifumo ya utoaji huduma kutoka ile ya kawaida kwenda majukwaa ya kidijitali yanayokidhi mahitaji ya wateja wa kizazi kipya.

Ili kuendana na mabadiliko hayo, Benki ya NMB imezindua NMB Mkononi Super App, hatua inayotafsiriwa kama jibu la moja kwa moja la sekta ya benki kwa mabadiliko ya uchumi wa kidijitali unaozidi kukua nchini na duniani kwa ujumla.

Akizungumzia maboresho hayo leo, Juni 16, 2026, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema katika miaka ya hivi karibuni huduma za kidijitali zimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku, na watu wanaweza kununua bidhaa, kuagiza huduma, kufanya miamala na kuwasiliana kupitia simu za mkononi.

Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki ya NMB, Ruth Zaipuna akizungumza katika uzinduzi wa NMB Mkononi leo Jumanne Juni 16, 2026 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Amesema mabadiliko hayo yameongeza matarajio ya wananchi kutaka huduma za kifedha ziwe rahisi, haraka na zinazopatikana wakati wowote bila vikwazo vya kimfumo.

“Mfumo huu ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo wa kuendana na mageuzi ya teknolojia na kuchochea ushirikishwaji wa kifedha,” amesema.

Amesema NMB Mkononi si App ya kawaida ya benki, bali ni jukwaa la uwezeshaji linalounganisha huduma mbalimbali za kifedha katika mfumo mmoja, hatua inayolenga kumrahisishia mteja kufanya maamuzi ya kifedha kwa haraka na kwa ufanisi.

“Dunia imebadilika kwa kasi kubwa ya teknolojia. Leo huduma nyingi za maisha zinapatikana kupitia simu za mkononi na sisi tumelazimika kuhakikisha huduma za kifedha zinakwenda sambamba na mabadiliko hayo,” amesema Zaipuna.

Kwa mujibu wa benki hiyo, maboresho ya mfumo huo yamejengwa juu ya uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Sh232 bilioni uliotumika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya teknolojia, usalama wa taarifa na ubunifu wa huduma za kidijitali.

Uwekezaji huo, pamoja na mambo mengine yaliyofanyika, umeiwezesha NMB kuunda jukwaa linalounganisha huduma nyingi katika sehemu moja, ikiwemo akaunti za benki, mikopo, bima, uwekezaji, malipo ya biashara, vikundi vya kijamii na huduma za miamala ya kila siku.

“Moja ya faida kubwa za maboresho hayo ni kuongeza kasi ya upatikanaji wa mikopo ya kidijitali. Kupitia mfumo huo, wateja wanaokidhi vigezo wanaweza kupata mikopo ya haraka ya hadi Sh2 milioni kwa watu binafsi na hadi Sh5 milioni kwa wafanyabiashara wadogo bila kufika tawi la benki au kujaza makaratasi mengi,” amesema.

Kwa upande wa jamii, maboresho hayo pia yameboresha mfumo wa vikundi vya kijamii na kiuchumi (Vicoba), ambapo sasa wanachama wanaweza kusimamia michango, mikopo na uamuzi wa vikundi kwa njia ya kidijitali, jambo linaloongeza uwazi, uwajibikaji na usalama wa fedha.

Zaipuna amesema hayo yote yamefanyika kwa kuzingatia usalama wa taarifa na miamala, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha imani ya wateja inazidi kuimarika katika matumizi ya huduma za kidijitali.

“Benki hiyo itaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa, ikiwemo akili mnemba na mifumo ya hali ya juu ya usalama, ili kuboresha zaidi uzoefu wa wateja na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani,” amesema.

Mbali na hilo, pia watumiaji wa NMB Mkononi wataweza kupata huduma mbalimbali za bima, ikiwemo bima za majanga na hata mikopo ya bima iwapo wataihitaji, jambo linalolenga kumlinda mtumiaji dhidi ya hasara anazoweza kupata.

Ametumia nafasi hiyo kuwaambia vijana kuwa App hiyo pia imefungua fursa mpya za kuunganisha suluhisho zao na kuwafikia mamilioni ya Watanzania kupitia mfumo wa NMB.

“Msisubiri fursa ziwafuate, zifuateni. Anzeni leo kujenga ndoto zenu, kuwekeza katika maarifa, kutumia teknolojia na kuamini katika uwezo wenu. NMB itaendelea kuwa mshirika wa safari yenu kwa kuwapatia huduma, majukwaa na suluhisho zitakazowawezesha kufikia malengo yenu,” amesema.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia na Ubunifu wa NMB, Josina Njambi, amesema watu wanaotaka kufungua akaunti, hasa wale wanaoishi nje ya nchi, wanaweza kujihudumia kwa kutumia namba ya simu na Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN).