NMB kufungua matawi nchi za SADC, thamani ya hisa zapanda
Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akizungumza wakati wa mkutano wa 26 wa wanahisa wa benki hiyo uliofanyika leo Jumatano Juni 10, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Muktasari:
- Benki hiyo imesema uimara wa uchumi wa Tanzania na mafanikio yake ya kifedha yanaipa nguvu ya kuangalia fursa mpya za biashara ndani ya ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Dar es Salaam. Benki ya NMB imetangaza mkakati wa kutanua masoko yake katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ikilenga kutumia fursa za ukuaji wa biashara za kikanda na kuimarisha huduma kwa wateja wanaofanya shughuli za kuvuka mipaka.
Hatua hiyo imeelezwa wakati wa Mkutano Mkuu wa 26 wa Wanahisa wa benki hiyo uliofanyika leo, Juni 10, 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine, gawio la Sh610.14 kwa kila hisa lilipitishwa.
Mkurugenzi Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema mazingira imara ya uchumi wa Tanzania yameendelea kuifanya sekta ya benki kuwa na nguvu, hali iliyochangia NMB kuendelea kupata matokeo mazuri mwaka hadi mwaka.
Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akizungumza wakati wa mkutano wa 26 wa wanahisa wa benki hiyo uliofanyika leo Jumatano Juni 10, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Amesema kinachofanyika sasa ni kuangalia namna ya kufikia mahitaji ya soko katika nchi za jirani, ili kuhakikisha matawi yanapofunguliwa yanaendelea kuwa chachu ya utendaji mzuri wa benki na kuleta faida kwa wanahisa.
“Tunaangalia zaidi katika nchi za SADC, kwa mfano Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa sababu hata ujumuishaji wa huduma za kifedha katika nchi hiyo bado uko chini, na tunaamini tawi hilo litakuwa kati ya yale yatakayoleta mageuzi,” amesema.
Mbali na DRC, nchi nyingine zinazotazamiwa katika kutanua huduma hizo ni Uganda, Kenya na Rwanda.
Hili linafanyika wakati mwaka 2025 benki hiyo ilirekodi mapato ya zaidi ya Sh1.8 trilioni na faida kabla ya kodi ya Sh1.1 trilioni, na kuifanya NMB kuwa kampuni ya kwanza katika historia ya Tanzania kupata faida kwa kiwango hicho.
“Huu ni ukuaji mkubwa katika upande wa faida, kwa sababu mwaka 2020 tulitengeneza faida kabla ya kodi ya Sh296 bilioni na miaka minne baadaye tumetengeneza faida hii. Ni ukuaji mkubwa sana, tunawashukuru sana,” amesema.
Ukuaji huo umefikiwa wakati benki ikionesha ufanisi kupitia kushuka kwa uwiano wa gharama na mapato, ambao umeshuka kutoka zaidi ya asilimia 50 hadi asilimia 38 na kuifanya kuwa benki inayoongoza kwa ufanisi mkubwa Afrika.
Ufanisi huo umeonekana pia katika kuboresha kiwango cha mikopo kwa kudhibiti mikopo chechefu, na sasa imefikia asilimia 2.5 kutoka asilimia 7 iliyokuwapo mwaka 2020.
“Benki ya NMB imekuwa na mchango mkubwa kwa wadau wetu wote. Ndani ya miaka mitano ya utekelezaji wa mpango wa miaka mitano, tumeshatoa gawio la zaidi ya Sh700 bilioni. Ni gawio kubwa ambalo halijawahi kutokea,” amesema.
Thamani ya hisa
Hisa zinatajwa kuwa moja ya vichocheo vya ukuaji, huku bei ya hisa ya Benki ya NMB sokoni ikifanya thamani ya benki hiyo kuongezeka hadi Sh7.4 trilioni kutoka Sh1.2 trilioni mwaka 2020.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, David Nchimbi akizungumza wakati wa mkutano wa 26 wa wanahisa wa benki hiyo uliofanyika leo Jumatano Juni 10, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Amesema hayo wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa mpango mkakati wa benki hiyo katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia 2021 hadi 2025.
Amesema bei ya hisa ya NMB mwaka 2020 ilikuwa Sh2,540 na ilipofika mwaka 2021 ilishuka hadi Sh2,000.
“Yaani mwaka 2021 ungesema ninunue hisa 5,000 za NMB, ungetoa Sh10 milioni. Leo ungesema unaziuza hisa hizo, ungeziuza kwa Sh74 milioni. Kama ungekuwa na Sh100 milioni ukanunua hisa, leo ungeziuza kwa Sh744 milioni. Tumeleta thamani kubwa sana kwa wanahisa,” amesema.
Amesema bei ya hisa ya NMB sokoni pia imeendelea kupanda siku hadi siku. Mwaka 2025 bei ilikuwa Sh8,420 na wiki iliyopita ilikuwa Sh14,870 kabla ya kuongezeka na kufikia Sh15,170 leo Juni 10, 2026.
Mbali na hisa, benki hiyo pia imetambua mchango wa mawakala katika kufikisha huduma za kibenki katika maeneo ya vijijini. Jambo hilo linaendana na mkakati wao wa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na wakala ifikapo mwaka 2030.
“Mwaka 2020 tulikuwa na mawakala 8,400, lakini hadi mwaka 2025 tulikuwa na mawakala zaidi ya 76,000. Hii imesaidia kupeleka huduma za kibenki karibu na Watanzania, kwani zaidi ya mawakala 5,000 wako maeneo ya vijijini ikiwa ni utekelezaji wa lengo la kuwa na wakala katika kila kijiji Tanzania ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi,” amesema Zaipuna.
Mmoja wa wanahisa akizungumza wakati wa mkutano wa 26 wa wanahisa wa NMB uliofanyika leo Jumatano Juni 10, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Ili kuhakikisha watu wengi wanapata fursa ya kununua hisa, benki hiyo imependekeza kufanya mgawanyo wa hisa kwa uwiano wa moja kwa kumi (1:10) ili kuongeza ushiriki wa wawekezaji wadogo na kuboresha uuzikaji wa hisa zake katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Alichokisema Nchimbi
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, David Nchimbi, amesema pamoja na mafanikio makubwa ya hisa ya NMB sokoni, kupanda kwa bei ya hisa hiyo kumeanza kuwa kikwazo kwa baadhi ya wawekezaji wadogo kushiriki kikamilifu.
“Utendaji bora wa kifedha wa benki, uimara wa mizania, uwezo wa kuendelea kulipa gawio na imani kubwa kutoka kwa wawekezaji wa taasisi na washirika wa maendeleo vimeifanya hisa ya NMB kuendelea kupanda thamani,” amesema.
Bei ya sasa ya hisa imefanya baadhi ya wawekezaji wadogo kuona hisa hiyo kuwa ghali. Kwa mfano, mwekezaji mwenye Sh100,000 kwa sasa ana uwezo wa kununua takribani hisa saba tu za NMB, ikilinganishwa na kati ya hisa 37 hadi 111 katika baadhi ya benki nyingine zilizoorodheshwa katika masoko ya hisa ya Afrika Mashariki na Kati.
Baadhi ya wanahisa wakiwa katika mkutano wa 26 wa wanahisa wa NMB uliofanyika leo Jumatano Juni 10, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akifafanua mgawanyo huo, Nchimbi amesema uwiano wa 1:10 unamaanisha kuwa kila hisa moja iliyopo itagawanywa kuwa hisa 10 za kawaida, hatua ambayo haitabadilisha thamani ya uwekezaji wa mwanahisa, bali itapunguza bei ya kila hisa na kuongeza idadi ya hisa zinazopatikana sokoni.
“Ikiidhinishwa, idadi ya hisa zilizoidhinishwa itaongezeka kutoka milioni 625 hadi bilioni 6.25, huku hisa zilizoorodheshwa katika soko zikiongezeka kutoka milioni 500 hadi bilioni tano,” amesema.
Wanahisa wa Benki ya NMB wamepitisha na kuipa Bodi ya Wakurugenzi mamlaka ya kuidhinisha ununuzi wa taasisi nyingine za kifedha na kuanzisha kampuni tanzu, hatua inayolenga kuharakisha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Benki wa miaka mitano wa 2026–2030 unaojulikana kama Agenda 2030.
Kupitia mkakati huo mpya, NMB inalenga kuimarisha nafasi yake sokoni, kuongeza uwezo wa biashara na kutengeneza vyanzo vipya vya mapato kupitia uwekezaji wa kimkakati ndani na nje ya shughuli zake za kawaida za kibenki.
Matawi mijini
Katika mkutano huo, aliyekuwa mbunge wa Mvomero na mwanahisa wa benki hiyo, Suleiman Ahmed Sadiq, ameitaka NMB kuongeza matawi katika maeneo ya mijini ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Ametoa kauli hiyo katika kipindi cha maswali na majibu, akisema kwa sasa benki hiyo inaonesha jitihada za kuhakikisha inafikisha huduma katika maeneo ya vijiji, lakini ni vyema kuhakikisha matawi katika miji mikubwa inayoendelea kutanuka, ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma, yanaongezwa ili kuweka urahisi wa huduma.
“Mfano Morogoro, mtu akifika Msamvu ataanza kuuliza Benki ya NMB iko wapi. Ukiweka tawi pale karibu na Round About, unawawekea urahisi watu kupata huduma wakiwa safarini, kama wanapita kwenda mikoa mbalimbali, kupata huduma na kuendelea na safari yao badala ya kuanza kuulizia,” amesema.
Akijibu suala hilo, Zaipuna amesema wamekuwa wakiliangalia kwa karibu.
“Mfano, Soko la Kariakoo tuna matawi matano. Tuliona tukasema ni sehemu ambayo ina uchumi mkubwa sana, ni lazima tuongeze matawi. Hivyo tumepokea ushauri wako na tutaangalia katika miji uliyoitaja ili tuone mahitaji yalivyo na tuchukue hatua,” amesema Zaipuna.