NMB yashinda tuzo 18 za kitaifa, kimataifa

Muktasari:

  • Benki ya NMB imefanikiwa kushinda tuzo 18 ndani ya mwaka 2022 kutokana na ufanisi pamoja na ubora wa huduma wanazozitoa kwa wateja wake.

Dar es Salaam. Benki ya NMB imeshinda tuzo 18 za kitaifa na kimataifa ndani ya mwaka 2022, hii ni baada huduma bora walizozitoa kwa wateja wake ambazo zinaufanisi na ubunifu wa hali ya juu.

 Hayo yamesemwa leo Jumatano, Novemba 23, 2022 na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alipokuwa akizungumza katika hafla fupi iliyoandaliwa na uongozi wa benki hiyo, makao makuu ya benki jijijni Dar es Salaam.

Amesema hafla hiyo ni kwaajili ya kutangaza mafanikio makubwa ambayo NMB wamefanikiwa kuyapata.

"Tumefanikiwa kupata tuzo 18 za kitaifa na kimataifa kwa mwaka huu 2022, kutokana na huduma bora tunazoendelea kuzitoa katika nyanja mbalimbali," amesema

Zaipuna ameeleza miongoni mwa tuzo walizofanikiwa kunyakua ni pamoja na Tuzo ya mshindi wa jumla wa taasisi zinazolipa kodi kubwa na kwa kuzingatia misingi na kanuni bora za ulipaji wa kodi illiyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Nyingine ni Tuzo ya Benki bora kutoka Tanzania mwaka 2022 iliyotolewa na jarida la 'Global Brand Magazine'.

"Tuzo hizi zinaakisi mchango wetu katika maendeleo ya kijamii, ubora na uimara wa mifumo yetu ya kidigitali, pamoja na mchango endelevu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii," amesema.

Kadhalika, Zaipuna amesema tuzo hizo walizofanikiwa kupata ni muhimu kwa sekta nzima ya kibenki nchini Tanzania.

"Tuzo hizi zimeitambulisha NMB kitaifa, kimataifa na nchi yetu ya Tanzania kimataifa," amesema.

Hata hivyo, ameeleza  NMB wamevuka lengo walilodhamiria kwa mwaka 2022 la kufungua akaunti milioni moja kwa mwaka mzima.

"Tulidhamiria kufungua akaunti milioni 1 ndani ya mwaka huu, lakini hadi sasa tumeshafungua akaunti milioni 1,012,344,'' amesema

Kwa upande wake, mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa NMB, Benson Muhenya amesema kwao NMB mwaka 2022 ni mwaka wenye  mafanikio makubwa sana, kutokana na utendaji wao mzuri wakazi walioufanya hadi kunyakua baadhi ya tuzo hizo.

"Tumefanya kazi nzuri ndani ya mwaka huu, lakini tunatakiwa tusibweteke na ushindi huu, hivyo tuendelee kuchapa kazi ili mwaka mwingine tupate tuzo nyingine zaidi na zaidi," amesema