Nsekela atunukiwa Shahada ya Uzamivu, ataja umuhimu wa utawala bora kwenye benki
Wa kwanza mbele ni Dk Nsekela ambaye mehitimu shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA). Picha na Maktaba
Muktasari:
- Dk Nsekela amehitimu shahada hiyo baada ya kufanya utafiti uliochunguza uhusiano kati ya utawala wa kampuni na utendaji wa kifedha wa benki za Afrika Mashariki, huku ukiangazia athari za uvujaji wa taarifa katika ufanisi wa taasisi hizo
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Abdulmajid Nsekela ametunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA), hatua inayotajwa kuimarisha mchango wa taaluma katika uongozi wa taasisi za kifedha na biashara.
Dk Nsekela amehitimu shahada hiyo baada ya kufanya utafiti uliochunguza uhusiano kati ya utawala wa kampuni na utendaji wa kifedha wa benki za Afrika Mashariki, huku ukiangazia athari za uvujaji wa taarifa katika ufanisi wa taasisi hizo.
Utafiti huo unaonesha mifumo imara ya utawala, uwazi na uadilifu katika usimamizi wa taarifa ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuimarisha utendaji wa taasisi za fedha na kuongeza imani ya wawekezaji kwa muda mrefu.
Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo Juni 12, 2026, Dk Nsekela amesema safari yake ya kitaaluma imechochewa na hamu ya kujifunza na kuchangia maendeleo ya sekta ya fedha kupitia maarifa yanayotumika kwenye mazingira halisi ya biashara.
“Usimamizi makini wa kampuni si suala la nadharia pekee, bali ni msingi wa utendaji bora, mafanikio endelevu ya kifedha na kujenga imani kwa taasisi za fedha ndani ya ukanda wetu,” amesema.
Amesema viongozi wa taasisi mbalimbali wanapaswa kuendelea kujifunza na kujiongezea maarifa ili kuboresha uamuzi wanaoufanya na kuongeza ufanisi kwa taasisi wanazoziongoza.
“Kwa wakurugenzi na watendaji wakuu, kujifunza ni safari endelevu, tunapaswa kutenga muda wa kuongeza maarifa na ujuzi unaoweza kuimarisha uongozi wetu na kusaidia taasisi kufikia malengo yake,” amesema.
Mafanikio hayo ya kitaaluma yanaongeza orodha ya mafanikio ambayo Dk Nsekela ameyapata katika sekta ya fedha kwa zaidi ya miaka 20, akihudumu katika maeneo mbalimbali ikiwemo usimamizi wa vihatarishi, huduma kwa wateja wakubwa na uongozi wa taasisi za kifedha.
Tangu alipoteuliwa kuiongoza CRDB mwaka 2018, benki hiyo imeendelea kushuhudia ukuaji mkubwa katika viashiria mbalimbali vya biashara.
Takwimu za benki zinaonesha faida baada ya kodi imeongezeka CRDB kutoka Sh64.1 bilioni mwaka 2018 hadi Sh728.6 bilioni mwaka 2025, huku bei ya hisa ikiongezeka kutoka Sh95 mwaka 2018 hadi kufikia takribani Sh3,000 mwezi Juni 2026.
Katika kipindi hicho, gawio kwa wanahisa limeongezeka kutoka Sh8 kwa kila hisa mwaka 2018 hadi Sh90 kwa kila hisa mwaka 2025.
Pia, benki hiyo imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma, zaidi ya asilimia 98 ya miamala yote kwa sasa inafanyika kupitia majukwaa ya kidijitali.
Idadi ya wateja wa CRDB nayo imeongezeka na kufikia milioni 7.2 wanaohudumiwa kupitia mtandao wa matawi, mawakala, mashine za kutolea fedha na huduma za kidijitali.
Mbali na ukuaji wa ndani, benki hiyo imepanua shughuli zake katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kutoa huduma Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na kufungua ofisi ya uwakilishi Dubai kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa mitaji ya uwekezaji.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori amesema shahada hiyo ya uzamivu inaonesha namna elimu ya juu inavyoimarisha uwezo wa viongozi kusimamia taasisi za biashara.
Amesema utafiti wa Dk Nsekela unaendana na mafanikio ya CRDB imeendelea kuyapata chini ya uongozi wake, hususan katika maeneo ya utawala bora, uwazi na matumizi ya taarifa katika kufanya maamuzi.
“Utafiti wake unaonesha jinsi usimamizi makini wa kampuni na udhibiti wa uvujaji wa taarifa unavyoweza kuongeza ufanisi wa taasisi. Haya ni mambo ambayo yameonekana kwa vitendo ndani ya CRDB,” amesema Profesa Mori.
Amesema mafanikio ya Dk Nsekela yanapaswa kuwa mfano kwa viongozi wengine wa taasisi za biashara na fedha barani Afrika kwa kuunganisha taaluma, ubunifu na uongozi katika kuendesha taasisi zao.