Nyumba 800 nafuu kujengwa Dar, Moro

Ofisa Mtendaji Mkuu wa WHC, Dk Fred Msemwa.

Muktasari:

Zitakuwa za watumishi wa Serikali, lengo ni kufikia nyumba 50,000 nchi nzima.

Kampuni ya Nyumba za Watumishi (WHC), imeanza ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa makazi kwa watumishi wa umma.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa WHC, Dk Fred Msemwa alisema ujenzi huo ulioanza na miradi mitano yenye nyumba 800, unatekelezwa katika mikoa ya Morogoro, Mwanza na Dar es Salaam.

Dk Msemwa alisema nyumba hizo ni sehemu ya nyumba 50,000 zilizoanza kujengwa nchi nzima kwa awamu tano kuanzia mwaka 2014.

Mkurugenzi huyo alitaja idadi ya nyumba zitakazojengwa na maeneo zitakapojengwa kuwa ni Mwanza (Kisesa 56), Dar es Salaam (Gezaulole 400 Bunju na Mabwepande 190 pamoja na Magomeni Usalama 1,040 na Tanga (Pongwe 40).

Alisema kampuni hiyo inatekeleza haraka ujenzi wa nyumba kama ilivyoagizwa na Serikali, ili kuwapunguzia watumishi wa umma makali ya maisha yanayotokana na kupanga.

“Tumeanza kutekeleza falsafa ya Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’. Tutatangaza, kuchambua na kutangaza washindi wa zabuni za ujenzi wa nyumba hizi 800 ili kuharakisha wafanyakazi walengwa wazipate haraka,” alisema Dk Msemwa.

Aliongeza kuwa katika tafiti zenye lengo la kupatia ufumbuzi matatizo yanayokwamisha utekelezaji kwa wakati wa miradi ya Serikali iliyofanywa na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), ilibainika kuwa ucheleweshaji wa taasisi za umma kutoa uamuzi wa utekelezaji wa miradi umeliingizia taifa hasara ya fedha nyingi.

Wakazi wa Magomeni Issa Masoud na Rashid Masawe walisema ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya watumishi wa Serikali utasaidia kupunguza ugumu wa maisha.

“Serikali imefanya vizuri kuwajali watumishi,” alisema Masoud.