Pampu za jua zaleta suluhu kwa wafugaji Kongwa

Kongwa. Migogoro ya wafugaji na mateso ya kusafiri umbali mrefu kufuata maji ya kunywesha mifugo katika vijiji na vitongozi vya Kata ya Chitego vimepata suluhisho, baada kuwepo kwa pampu ya maji iliyofungwa kwenye visima kwa ajili ya mifugo.

Pampu hizo zinaendeshwa kwa umeme wa jua unaozalishwa kutoka gridi ndogo ya nishati ya jua iliyofungwa na Shirika la Elico Foundation kwa ajili ya wananchi wa kata hiyo.

Mbali na kupunguza umbali wa kufuata maji kwa ajili ya mifugo yao, wafugaji wamepunguziwa gharama walizokuwa wakitumia kwa ajili ya kunywesha mifugo, jambo ambalo lilikuwa ni changamoto yao kubwa kwa muda mrefu.

Vijiji walivyofungiwa mitambo hiyo na pampu katika visima ni Leganga na Ngutoto ambapo zaidi ya ng’ombe 13,000, mbuzi na kondoo 21,000 na punda 3,000 wanapata maji kwenye maeneo ya jirani na wanakotoka.

Kabla ya pampu hizo wengine walitembea zaidi ya kilomita 11 kufuata maji vijiji vya Chitego, Suwi au Zoisa walikokutana na makundi makubwa ya mifugo na kupelekea kuambukizana magonjwa lakini sasa wanatembea kilomita mbili hadi tatu.

Akizungumza na Mwananchi kwenye mlambo wa kunywesha mifugo katika Kijiji cha Leganga Wilaya ya Kongwa, Kiputwa Kanaya alisema mtambo wa umeme jua umemaliza matatizo waliyopata wafugaji pamoja na kuondoa manung’uniko ya kundi hilo kusahaulika.

“Huko nyuma ng’ombe mmoja tulimlipia Sh100, lakini kulikuwa na vurugu ya kugombania maji, leo ng’ombe anakunywa maji kwa Sh70 lakini ng’ombe wadogo hatutozwi fedha wala mbuzi, kwa hiyo tunaposema tumekumbukwa kwenye mafanikio siyo kosa,” anasema Kiputwa.

Kwa mujibu wa mfugaji huyo, umeme jua umekuwa tofauti na vyanzo vingine kwa madai kuwa, haukatikikatiki, hasa ikizingatiwa maeneo hayo kuna jua la kutosha na kwamba gharama wanazotumia ni ndogo ukilinganisha na vyanzo vingine kwa kiwango cha maji yanayotosheleza mifugo.

Mwananchi mwingine katika kata hiyo alisema mbali na kuwasaidia wafugaji, umeme huo umepeleka kicheko kijijini hapo kwa vijana wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji, uchomeleaji vyuma na huduma za saluni za kike na kiume ambayo kabla walipata mbali na hapo.

“Sasa hivi hata ukiingia madukani unakutana na vinywaji baridi kama ilivyo maeneo ya mjini, hatuna shida na wafugaji lakini hata nyama inayoliwa kwenye mabucha imekuwa na mvuto hata kwa macho, tofauti na mwanzo mifugo ilikonda sana kwa sababu ya umbali wa kufuata maji,” alisema Neema.

Msimamizi wa mradi huo katika Kijiji cha Leganga, Elikana Sehaba alisema wataendelea kufanya maboresho zaidi kulingana na matakwa ya wananchi sanjari na kuwafikia wengi zaidi.