Pikipiki ya NMB yatua Goba, mshindi afunguka

Muktasari:

Ukisikia bahati ndio hii sasa baada ya mkazi wa Goba, Dar es Salaam, Jeremiah Iranga kujishindia zawadi ya pikipiki ya miguu mitatu maarufu kama Toyo.

Dar es Salaam. Ukisikia bahati ndio hii sasa baada ya mkazi wa Goba, Dar es Salaam, Jeremiah Iranga kujishindia zawadi ya pikipiki ya miguu mitatu maarufu kama Toyo.
Iranga, ambaye ni mfanyabiashara ameshinda toyo hiyo kupitia droo ya nne ya promosheni ya Weka Akiba na Ushinde inayoendeshwa na benki ya NMB.
Toyo hiyo aina ya Skymark yenye thamani ya Sh4.5 milioni imekabidhiwa jana na Meneja wa NMB Tawi la Mlimani City, Deogratius Kawonga kwenye halfa ya makabidhiano ikifanyika Viwanja vya Stendi ya daladala ya Mawasiliano 'Simu 2000.'
Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi hiyo, Kawonga amesema NMB Bonge la Mpango ni kampeni ya miezi mitatu inayohamasisha utamaduni chanya wa kuweka akiba.
Kupitia kampuni hiyo kila wiki washindi 10 huzawadiwa pesa taslimu (Sh100,000) kila mmoja, huku wengine wawili wakitwaa pikipiki hizo kwa kila mshindi.
Promosheni hiyo itaendeshwa kwa wiki 12 ambazo zitazalisha jumla ya washindi 170 watakaozoa zawadi zenye thamani ya Sh237 milioni huku kigezo ikiwa ni kufungua akaunti na kuweka angalau Sh100,000 ama mteja mwenye akaunti kuweka akiba isiyopungua kiasi hicho.
Kawonga amewataka wateja kuendelea kujiwekea akiba ili kuongeza nafasi za kushinda zawadi hizo, huku akiwataka wasio na akaunti NMB kuchangamkia fursa hiyo.
Kwa upande wake, Iranga amekiri kufurahia zawadi hiyo ambayo kwake ni zaidi ya mtaji kwani, itampunguzia gharama za usafirishaji wa mazao ya biashara anayoifanya kwa sasa.
00000