Rais Mwinyi kushiriki mkutano wa jukwaa la kimataifa la uchumi

Muktasari:

  • Katika ziara yake, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameambata na watendaji mbalimbali wakiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Shariff Ali Shariff na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri.

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa jukwaa la kimataifa la tatu la uchumi utakaofunguliwa kesho Mei 23, 2023 mjini Doha, Qatar.

 Katika ziara yake, Rais Mwinyi leo Mei 22, 2023 amekutana na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Qatar, Muhamed Bin Ahmed Al-Kuwari na wadau kutoka sekta binafsi ya viwanda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dk Mwinyi aliwakaribisha wafanyabiashara hao wakubwa kuwekeza Zanzibar kutokana na fursa zilizopo pia aligusia eneo jipya la uwekezaji ambalo ni utalii wa kumbi za mikutano.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Shariff Ali Shariff ameeleza umuhimu wa kukutana kwa mabaraza ya uwekezaji ya Zanzibar na Qatar ili kuimarisha uhusiano zaidi.

Pia, ameelezea fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar zaidi kwa upande wa utalii kwani ujenzi wa hoteli kubwa za kifahari unahitajika kutokana na soko la utalii kuongezeka.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri ameainisha vivuvito vilivyowekwa na Serikali kusaidia kulinda mitaji ya wawekezaji kwa kipindi cha uwekezaji na kuongeza kuwa zipo fursa kwenye sekta za utalii, madini, ujenzi ikiwemo mji mkuu Dodoma, viwanda na huduma za kifedha na bima.

Kwa upande za Zanzibar, fursa nyingine zilizotajwa ni ukodishaji wa visiwa vidogo. Teri ameeleza kwamba fursa zilizopo katika sera ya uchumi wa buluu ambayo imewagusa zaidi wawekezaji hao hasa suala la uchimbaji wa gesi na mafuta.

Eneo jingine ni shamba la Makurunge Bagamoyo ambalo ni mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar linalofaa kwa utalii na hata kilimo.