Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Mbeya: Tiseza punguzeni gharama za usajili wa kampuni

Meneja wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Uchumi Tanzania (TISEZA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Fidelis Obanga (kulia), akimsikiliza mwekezaji wa mradi wa kilimo cha kahawa, Hans Faussler, wakati wa ziara ya TISEZA mkoani Mbeya iliyolenga kuhamasisha uwekezaji, kutangaza fursa za maeneo maalumu ya uwekezaji na kutoa elimu kwa wawekezaji.

Muktasari:

  • Tiseza Nyanda za Juu Kusini ilifanya ziara yake ya siku mbili mkoani Mbeya kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji, kutoa elimu na kuonesha fursa zilizopo kwenye uwekezaji na maeneo yaliyotengwa kwa uwekezaji.

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa ameishauri Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), kutafuta njia za kupunguza gharama za usajili wa kampuni ili kuwapa fursa zaidi wawekezaji, hususan vijana wanaohamasishwa kujiajiri.

Malisa amesema pamoja na Serikali kurahisisha huduma za usajili wa kampuni kwa njia ya mtandao, gharama zinazohitajika kukamilisha mchakato huo bado ni kubwa na zinaweza kuwa kikwazo kwa wawekezaji wengi.

Ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya viongozi wa Tiseza Kanda ya Nyanda za Juu Kusini walipomtembelea ofisini kwake mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa Malisa, gharama zisizokwepeka za usajili wa kampuni zinaweza kufikia zaidi ya Sh3 milioni, kiwango ambacho amesema si rafiki kwa vijana wanaotaka kuanzisha biashara na kujitengenezea ajira.

"Kwa mfano, kuanzia mtaji wa Sh10 milioni hadi Sh300 milioni kuna gharama ya usajili ya Sh300,000. Lakini ukijumlisha gharama nyingine zisizokwepeka, unaweza kuhitaji zaidi ya Sh3 milioni. Sasa tunamlenga kijana yupi? Lazima kuwe na uwiano ili sera zetu ziendane na uhalisia," amesema Malisa.

Ameitaka Tiseza kutathmini upya baadhi ya gharama hizo ili kuifanya mazingira ya uwekezaji kuwa rafiki zaidi kwa wazawa, hususan vijana.

"Mnapaswa kulifanyia kazi suala hili na kuangalia kama kuna namna ya kupunguza baadhi ya gharama. Hatua nzuri ambayo Serikali imeifanya ni kuondoa sharti la kulipa kodi kwanza ili kupata leseni na kufungua akaunti, jambo ambalo limeleta nafuu kwa wawekezaji," amesema.

Malisa amesema Mkoa wa Mbeya una fursa nyingi za uwekezaji zinazoweza kuendelezwa bila kuathiri shughuli za kilimo, akitaja sekta za elimu, madini, biashara, utalii, ufugaji, uvuvi na kilimo kuwa miongoni mwa maeneo yenye nafasi kubwa ya kuvutia mitaji.

Ameongeza kuwa mkoa huo pia unanufaika na rasilimali watu, taasisi za kifedha na hali nzuri ya hewa, huku Serikali ikiwa imetenga maeneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji, yakiwemo Tanganyika Packers, Chunya na maeneo ya taasisi za umma kama Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) pamoja na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

"Mbeya inavutia kwa uwekezaji kutokana na hali yake ya hewa na nafasi yake ya kijiografia. Tunataka uwekezaji unaokwenda sambamba na utamaduni wetu wa kilimo na maendeleo ya wananchi," amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa Tiseza Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Fidelis Obanga, amesema mamlaka hiyo ina jukumu la kutangaza fursa za uwekezaji, kuwezesha wawekezaji na kutoa ushauri katika sekta mbalimbali za uchumi.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2021, Tiseza imesajili miradi 63 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 5.8, ambayo imezalisha ajira 269.

Obanga amesema Mkoa wa Mbeya unaendelea kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji kutokana na fursa zilizopo katika sekta za madini, kilimo na biashara, pamoja na nafasi yake kama lango la biashara kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

"Mazingira ya biashara Mbeya ni mazuri. Mkoa huu ni lango la SADC na una soko kubwa kutokana na idadi ya watu. Tunawahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza ili wanufaike na fursa zilizopo," amesema.

Ameongeza kuwa kati ya miradi hiyo, 20 imesajiliwa na wawekezaji wazawa, huku mingine ikihusisha ubia kati ya Watanzania na wawekezaji wa kigeni pamoja na miradi inayomilikiwa na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Naye Msimamizi Mkuu wa City Park jijini Mbeya, Mhandisi God Msuya, amesema Tiseza inapaswa kuongeza juhudi katika kutoa elimu na kutangaza fursa za uwekezaji ili kubadili mtazamo wa wananchi kuwa uwekezaji si kwa wageni pekee.

"Niwaombe Watanzania, hususan wazawa wa Mkoa wa Mbeya, kutumia fursa hizi za uwekezaji. Wakati huohuo, Tiseza iendelee kutoa elimu na kutangaza fursa zilizopo ili kuondoa dhana kwamba mwekezaji lazima atoke nje ya nchi," amesema.