Rostam aruhusiwa kuwekeza gesi Kenya

Mfanyabisahara maarufu nchini Tanzania, Rostam Aziz.

Muktasari:

  • Mfanyabiashara Rostam Aziz hatimaye ameruhusiwa kufanya biashara nchini Kenya akitarajiwa kuwa mwekezaji mkubwa zaidi wa gesi Kenya, ambapo uzinduzu rasmi utaongozwa na Rais William Ruto.

Dar es Salaam. Baada ya kukwama mara ya kwanza hatimaye mfanyabisahara maarufu nchini Tanzania, Rostam Aziz anatarajia kuanza rasmi utekelezaji wa mradi wake wa gesi nchini Kenya huku akisifia mazingira bora ya uwekezaji katika nchini humo.

 Rostam kupitia kampuni yake ya Taifa Gas ameruhusiwa kutekeleza mradi wake ambao unatajwa kuwa na thamani ya Dola za kimarekani 130 milioni (Sh304 bilioni) hali itakayomfanya kuwa kampuni kubwa zaidi ya gesi katika nchini humo.

Katika mradi huo Taifa Gas itajenga mtambo wa tani 30,000 katika eneo maalumu la uwekezaji Dongo Kundu jirani na Bandari ya Mombasa, hivyo kuongeza ushindani kwa kampuni za Vivo, Rubis na Total pamoja na Africa Gas and Oil Limited (AGOL) zinazosambaza nishati hiyo.

Taarifa ya iliyotolewa na taifa gesi leo Alhamisi Februari 23, 2022 imeeleza uzinduzi rasmi wa mradi huo wa mabilioni ya Shilingi utafanyika Ijumaa, Februari 24 mwaka huu na utaongozwa na Rais William Ruto.

Mkurugenzi Mkuu wa Taifa Gas, Kenya, Veneranda Masoum amesema uamzi wa kampuni hiyo ya kuhifadhi na kusambaza gesi za kupikia majumbani kwekeza nchini Kenya unaonyesha imani yao kwa maendeleo katika nchi hiyo.

“Tunafurahi kuwa hivi sasa tuna mradi wetu wa kwanza Mombasa nchini Kenya, tumevutiwa zaidi na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo,” alisema Masoum.