Ruto: Tanzania itazivuka changamoto zake
Rais wa Kenya, William Ruto akizungumza na waandishi wa habari kufuatia ziara yake ya kitaifa, leo Mei 4, 2026Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Kauli hiyo inakuja miezi saba tangu zilipotokea ghasia nchini wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, mwaka jana, zilizosababisha mauaji ya watu na uharibifu wa mali.
Dar es Salaam. Rais wa Kenya, Dk William Ruto amesema ni imani yake kuwa Tanzania itavuka kipindi cha changamoto ya migawanyiko na kuungana kama Taifa, huku akimsifu Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuonesha uongozi katika nyakati hizo.
Kauli ya Dk Ruto, inakuja miezi saba tangu zilipotokea ghasia nchini wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, mwaka jana na kusababisha mauaji ya watu na uharibifu wa mali.
Kutokana na hilo, Rais Samia aliunda tume ya kuchunguza matukio hayo na ikawasilisha ripoti yake Aprili 23, mwaka huu, ikitaja mifumo ya uchaguzi, Katiba mpya na watu kutekwa na kupotea kuwa vyanzo vya ghasia hizo.
Katika maelezo yake aliyoyatoa leo Jumatatu Aprili 4, 2026, Rais Ruto amemsifu Samia, akisema ameonesha uongozi kwa kuunda tume ya kuchunguza mambo hayo na hilo limedhihirisha kuwa, mataifa ya Afrika Mashariki yanaweza kutatua changamoto zake ndani ya mipaka yake.
“Kwa niaba ya Afrika Mashariki, tunakupongeza kwa kuonesha uongozi kwa Tanzania na ukanda wetu na kuhakikisha kwamba, tunaweza kutatua matatizo yetu ndani ya mipaka yetu,” amesema Rais huyo wa Kenya.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na mgeni wake Rais Kenya, William Ruto wakishuhudia utiaji saini wa mikataba ya ushirikiano baina ya mataifa hayo katika sekta mbalimbali kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari, Ikulu Jijini Dar es Salaam
Amesema katika hilo atambue wanamuunga mkono kuhakikisha anatatua changamoto zote na hatimaye kuwa na nchi yenye amani na kutoa fursa kwa wote kufanya mambo muhimu hasa kwa vijana.
“Tunakuunga mkono na tuna dhamira ya kufanya hivyo pamoja. Nakwambia haya kwa uzoefu, tumeshapitia haya Kenya na nina uhakika kwamba Tanzania itavuka kwenye haya na itaungana kwa nguvu kama nchi,” amesema Rais Ruto.
Tunahitajiana
Katika mkutano huo, Rais Ruto amesema mataifa ya Kenya na Tanzania yanahitajiana, akisisitiza hakuna sababu ya kuwa na vikwazo, kwa kuwa havimnufaishi yeyote zaidi ya kujidhoofisha.
“Kenya inaihitaji Tanzania kama ambavyo Tanzania inaihitaji Kenya. Sisi ni wamoja na tuna hatima inayofanana. Kulikuwa na muda, biashara kati ya nchi zetu ilikuwa inaibeba Kenya, kwa sasa mambo ni tofauti, biashara inanufaisha pande zote,” amesema.
Amelieleza hilo huku akitolea mfano miaka miwili iliyopita, akisema Tanzania iliuza zaidi bidhaa zake Kenya, kuliko ambavyo Kenya imeuza kwa Tanzania, hiyo inamaanisha uhusiano wa nchi hizo una faida kwa pande zote.
“Tunahitajiana. Kwa kadri tulivyolitambua hili mapema na ndivyo tunavyoweza kuepuka vikwazo visivyo na umuhimu kati ya nchi zetu mbili, haimsaidii yeyote, inatufanya tuwe dhaifu,” amesema.
Amesema Tanzania ina kaka na dada nchini Kenya, wakati Kenya nayo ina kaka na dada nchini Tanzania, kwa sababu hiyo, mataifa yote hayo yanapaswa kudumisha uhusiano na ushirikiano.
EAC itumie rasilimali zake
Amesema ni muda wa jumuiya ya Afrika ya Mashariki kutumia rasilimali zake ikiwamo mafuta kama kichocheo kikuu cha maendeleo ya viwanda na uchumi.
Amesema upo umuhimu wa uwekezaji katika miundombinu ya nishati hasa mabomba ya mafuta kama kichocheo kikuu cha maendeleo ya viwanda katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesisitiza rasilimali za asili zilizopo katika nchi za ukanda huu zinapaswa kutumika ndani ya eneo hili ili kuchochea ukuaji wa uchumi, badala ya kusafirishwa nje kama malighafi.
“Ujenzi wa bomba la mafuta na miundombinu mingine ya nishati utawezesha usafirishaji wa mafuta ghafi na bidhaa zake kwa urahisi kati ya nchi kama Kenya na Tanzania. Hatua hii itafungua fursa kubwa za uwekezaji katika viwanda vya kusafisha mafuta, pamoja na viwanda vinavyotegemea bidhaa za petroli kama vile plastiki na kemikali,” amesema.
Amesema ukanda huo una nafasi ya kuwa kitovu cha uzalishaji na biashara ikiwa nchi wanachama zitaunganisha nguvu na kutumia rasilimali zao kwa pamoja.
Amesisitiza kuwa, si busara kuendelea kuuza malighafi nje kisha kununua bidhaa zilizokamilika kwa gharama kubwa, badala yake, nchi za Afrika Mashariki zinapaswa kujenga uwezo wa kuchakata rasilimali hizo ndani ya mipaka yao ili kuongeza ajira, kipato na maendeleo ya teknolojia.
Aidha, Rais Ruto amegusia umuhimu wa kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kama chombo cha kuleta mshikamano wa kiuchumi na kisiasa.
Amesema kupitia ushirikiano huo, nchi wanachama zinaweza kushindana kimataifa kwa ufanisi zaidi na kuvutia uwekezaji mkubwa.
Rais Samia
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Samia amesema wamezungumza kuhusu masuala ya kuimarisha ulinzi na usalama mipakani, kadhalika kukuza biashara na uwekezaji.
“Tumekubaliana kuondoa vikwazo vyote visivyo vya kikodi. Tumewapa watendaji wetu mwisho wa mwezi huu wa Mei wawe wamemaliza vikwazo vya kikodi,” amesema.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais wa Kenya, William Ruto, Ikulu Jijini, Dar es Salaam.
Amesema wamekubaliana tume za pamoja za ushirikiano zikae mara kwa mara ili kuzungumza na kukubaliana kwamba, vikwazo vipungue badala ya kuongezeka.
Rais Samia amesema wamekamilisha ujenzi wa njia ya kwanza ya umeme na sasa wanatarajia kujenga njia nyingine, kurahisisha uuzaji wa nishati hiyo.
Kuhusu ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa Kenya, Samia amesema wamekubaliana na mkataba umeshasainiwa.
Kingine walichokubaliana, amesema ni ujenzi wa Reli ya Kisasa itakayopita Arusha hadi Kenya, pia Rais Ruto ameomba kipande kingine cha SGR kijengwe kutoka Kenya hadi Singida.
Katika ulinzi, amesema wamekubaliana kuhusu mapambano ya ugaidi, dawa za kulevya, uhamiaji haramu na kuongeza ulinzi katika mipaka ili waovu wasivuke kufanya uovu pande zote.
Akizungumzia sekta ya anga, Rais Samia amesema wamepongezana kwa kufanya vizuri na wamekubaliana kuongeza juhudi.
Kuhusu kilimo, amesema amewaambia Wakenya kuwa Tanzania ni mzalishaji mzuri wa mahindi, hivyo wakati utakapofika Taifa hilo lije kununua nchini.
“Ikiwezekana tuwe na mpango wa Serikali na Serikali kuuziana ili tunufaike,” amesema Rais Samia.
Amesema wamekubaliana pia kuhusu ubunifu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) hasa kwa vijana kuwe na mnyororo mmoja wa mafunzo ili wote wakue kwa pamoja.
“Isiwe kama sasa hivi, ukiingia kwenye mitandao ya kijamii mheshimiwa Rais alalalalaa... wanatutukana wenyewe na mwisho wana-cross wanatukanana wenyewe kwa wenyewe,” amesema.
Mikataba iliyosainiwa
Kabla ya mkutano huo, Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Kenya, zimesaini mikataba minane ya makubaliano, ikiwamo hati ya makubaliano ya ushirikiano wa uendelezaji na usimamizi wa reli kati ya Serikali ya Tanzania na Kenya.
Mwingine ni mkataba wa uwili kati ya Serikali ya Tanzania na Kenya kuhusu upembuzi yakinifu wa ujenzi wa mradi wa gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, Kenya.
Mkataba mwingine ni wa usaidizi wa kisheria katika masuala ya jinai na hati ya makubaliano kuhusu masuala ya kilimo kati ya Serikali ya Tanzania na Kenya.
Mwingine ni utambuzi wa vyeti vya mabaharia kati ya Serikali ya Tanzania na Kenya. Pia, imesainiwa hati ya makubaliano kuhusu kuimarisha ushirikiano na usimamizi wa sekta ya usafiri wa njia ya maji kati ya Serikali ya Tanzania na Kenya.
Mkataba mwingine, ni hati ya makubaliano kuhusu ushirikiano kati ya Taasisi ya Viwango Zanzibar na Shirika la Viwango la Kenya na hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya vyuo vya utumishi vya Kenya na Tanzania kuhusu kujengeana uwezo wa utumishi wa umma.